• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 AM
SHANGAZI AKUJIBU: Amenitema eti miye nina umri kama wa mamake

SHANGAZI AKUJIBU: Amenitema eti miye nina umri kama wa mamake

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 40 na nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwenye umri wa miaka 28 ambaye nilidhani atanioa. Sasa amenishangaza kuniambia hanitaki tena eti mimi ni sawa na mama yake. Matamshi yake hayo yamenichoma moyo sana. Nashuku ameshauriwa hivyo na marafiki zake kwani wengi wao wananichukia. Nishauri.

Kupitia SMS

Hali kwamba wewe una umri mkubwa kumshinda haiwezi kuwa kikwazo kwenu kufunga ndoa na sielewi ni kwa nini mwenzako amebadilika kwani mmekuwa wapenzi akijua tofauti ya umri iliyopo kati yenu. Huenda ameshauriwa na marafiki zake kama unavyosema. Ukweli ni kuwa kama ameamua hivyo itabidi ukubali uamuzi wake.

 

Nilipomfumania na dume fulani akasema yangu naye yameisha

Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa. Juzi nilishangaa sana nilipomfumania katika maskani fulani ya burudani akiwa na mwanamume mwingine. Nilipomuuliza aliniambia wazi kuwa huyo ni mpenzi wake na papo hapo akaniambia kuwa uhusiano wetu umekwisha. Uamuzi wake huo umeniacha hali mbaya na ninahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini mpenzi wako ana sababu zake za kufanya uamuzi huo ingawa aliutekeleza kwa jinsi isiyofaa. Kama aliamua kuwa hataki muendelee na uhusiano angekuelezea mkiwa wawili badala ya kukushtua kwa kukuonyesha mpenzi wake mpya. Itabidi umsahau na kutafuta mwingine kwani yeye tayari amepata wake.

 

Hanipigii simu wakati tunaishi miji tofauti

Shangazi nina tatizo kuhusu mpenzi wangu. Tunaishi miji tofauti na inatuchukua muda mrefu kuonana. Lakini hashughuliki kunijulia hali na nisipompigia simu anaweza hata kumaliza wiki nzima bila kuwasiliana nami. Anadai ananipenda lakini nimeanza kumshuku. Nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana unajilazimisha tu kwa huyo unayemuita mpenzi wako. Kama kweli anakupenda hawezi kumaliza hata siku bila kuwasiliana nawe hasa kama anaishi mbali na hamuonani mara kwa mara. Labda amegundua hakupendi na anashindwa kukwambia. Tafuta wakati uzungumze naye ili ujue msimamo wake.

 

Nimeshindwa nguvu za kuwashibisha wake wangu wawili

Shangazi tafadhali naomba ushauri wako. Nimeoa wake wawili na ninawapenda sana. Tatizo ni kuwa siku za hivi majuzi ninashindwa kuwahudumia kikamilifu na wameanza kulalamika. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Umejitakia mwenyewe hayo na sijui unataka ushauri gani kutoka kwangu. Sababu ni kuwa uamuzi wa kuoa wake wawili ulikuwa wako wala hukulazimishwa. Sasa hilo litakuwa funzo kwako wakati mwingine ukiomba kazi ni lazima uwe na hakika kuwa unaiweza.

 

Ghafla ameanza kunywa pombe nami sipendi hivyo

Hujambo shangazi? Nina mpenzi ambaye nampenda sana. Tulipokutana hakuwa anakunywa pombe lakini siku za hivi majuzi ameanza uraibu huo na amekuwa akinishawishi nijiunge naye. Mimi nachukia sana sio tu kunywa pombe bali pia watu wanaokunywa pombe. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mwenzako huyo anajipenda sana na si vizuri. Ni makosa kwake kukulazimisha kunywa pombe eti kwa sababu yeye anakunywa. Isitoshe, pombe ina madhara na badala ya kukuingiza katika uraibu huo anafaa yeye mwenyewe kuacha. Kama hilo ni mojawapo ya masharti yake katika uhusiano wenu itabidi uamue iwapo utakubali umuoe na kama huwezi basi itabidi muachane atafute mlevi kama yeye.

 

Mpenzi wangu sasa anatongoza rafiki yangu, nimehamaki

Vipi shangazi? Nimevunjwa sana moyo na mpenzi wangu ambaye sikufikiria anaweza kunisaliti kimapenzi. Mwanamke rafiki yangu alionyesha jumbe za SMS ambazo mwanamume huyo amekuwa akimtumia akitaka wawe na uhusiano. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba mwanaume huyo amekosa adabu kiasi cha kumtongoza rafiki yako bila wasiwasi kwamba ni rahisi kwako kujua. Kuna usemi kuwa usiyemdhania ndiye kumbe siye; sasa umejua kuwa mpenzi wako ni laghai wa kimapenzi na huna budi kumtema.

You can share this post!

Kikosi kizima cha Bandari kuvinjari Afrika Kusini

AKILIMALI: Amepata tuzo mbalimbali kwa ufugaji bora wa mbuzi

adminleo