Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Anataka turudiane lakini tayari nishazoea upweke

November 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nilikuwa nimeolewa lakini tuliachana na mume wangu miaka mitano iliyopita tukiwa na watoto watatu. Kwa muda wote huo, nimekuwa nikiwalea watoto wetu peke yangu. Sasa ameanza kunipigia simu akitaka nirudi kwake. Mimi simtaki kwani tayari nimezoea maisha ya upweke na sijui amekuwa wapi wakati wote huo. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba mume wako amefikiria kukutafuta baada ya kutoweka kwa miaka mitano bila mawasiliano wala msaada wowote kwa ajili ya kugharimia malezi ya watoto wenu. Kama umezoea maisha ya kujitegemea kwa muda huo, ni heri uendelee hivyo. Una haki ya kuchagua kurudi ama kutorudi. Mwambie ukweli ili aondoe mawazo yake kwako.

 

Nimethibitisha sina shida ya uzazi lakini mume naye amegoma kupimwa, itakuwaje?

Kwako shangazi. Niliolewa nikiwa na mtoto niliyezaa na mpenzi wangu wa kwanza. Huu ni mwaka wa tatu na sijapata mwingine. Nilidhani mimi ndiye mwenye shida lakini nilipoenda hospitalini kupimwa nikapatikana niko sawa. Nilishauriwa nimwambie mume wangu aende akapimwe lakini amekataa, kila nikimwambia huzua vita. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Iwapo wewe ulipimwa ukapatikana uko sawa, bila shaka mume wako ndiye mwenye shida na labda anajua na ndiyo maana hataki kwenda hospitalini. Ninaamini kuwa ndoa yenu imetokana na mapenzi na ni bahati kubwa kwamba tayari una mtoto. Unaweza kuamua kutosheka na huyo mmoja kutokana na mapenzi yako kwa mume wako. Kiapo cha ndoa kinahitaji wawili kuvumiliana katika kila hali, ukiwemo upungufu wa kimwili na hata magonjwa.

 

Nasumbuka moyoni

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 24 na nina mpenzi. Kuna jambo linalonisumbua moyoni kumhusu mpenzi wangu. Kuna msichana jirani yake katika mtaa anamoishi ambaye nimempata naye mara kadhaa nikimtembelea nyumbani kwake. Nimemuuliza akasema ni jirani na pia ni marafiki. Lakini moyo wangu unaniambia kuna zaidi ya urafiki kati yao. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Una sababu ya kuwa na wasiwasi hasa kutokana na mazoea ya msichana huyo kuingia nyumbani kwa mpenzi wako bila wewe kuwepo. Huenda mpenzi wako hana nia yoyote kwake lakini yeye anataka kumnyakua kutoka kwako. Kama huo ndio mpango wake, itakuwa rahisi kwake kwa sababu ni jirani yake kwa hivyo ana nafasi nzuri ya kujipendekeza na kumshawishi. Ni muhimu umwelezee mpenzi wako kuhusu hofu yako ili mtafute suluhisho. Unaweza kuhamia karibu naye ama yeye ahamie karibu nawe ili kulinda uhusiano wenu.

 

Mume analewa sana na hurejea usiku wa manane, nimechoka

Kwako shangazi. Mpenzi wangu alinioa baada ya kuwa katika uhusiano kwa miaka miwili. Huu sasa ni mwezi wangu wa tano nikiwa katika ndoa na kuna tabia nimeona kwa mume wangu ambayo sikujua ako nayo na ningejua singekubali anioe. Analewa sana pombe karibu kila siku na mara nyingi huwa anarudi nyumbani baada ya saa sita usiku. Nampenda lakini sidhani nitaweza kuvumilia tabia yake hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Inaonekana mume wako alijaribu kuficha uraibu wake huo kwa muda ambao mlikuwa wapenzi na ndiyo sababu hukujua. Kwa kuwa sasa amekuoa na mnaishi pamoja, hawezi tena kuficha. Itakuwa vyema umwambie ukweli. Kwamba huwezi kuvumilia mume mlevi na ungejua ana uraibu huo hungekubali akuoe. Hakuna uraibu ambao mtu hawezi kuacha. Kama anakupenda ataacha. Kama hawezi kuacha nawe huwezi kuvumilia, basi hutakuwa na budi ila kutoka katika ndoa hiyo.

 

Awezaje kuongea hivi akijua vizuri nimezaa kabla ya kuolewa

Nina umri wa miaka 20 na nina mtoto ingawa sijaolewa. Kuna mwanamume tunayependana na anajua kuwa nina mtoto. Lakini amesema mara kadha kuwa hawezi kulea mtoto ambaye si wake na pia anapenda kuzungumza kuhusu wanawake wengine tukiwa pamoja. Nampenda sana, nishauri.

Kupitia SMS

Hata kama unampenda, nahisi kuwa mwanamume huyo hakupendi na wewe pia unajua hivyo. Sababu ni kuwa amekwambia wazi kuwa hawezi kulea mtoto asiye wake. Pili, unasema huwa anazungumza kuhusu wanawake wengine mkiwa pamoja. Ni wazi kuwa moyo wake hauko kwako na ukijaribu kujipendekeza kwake utakuja kujuta.