SHANGAZI AKUJIBU: Baba halisi anadai mtoto niliyelea miaka 3, ni haki?
Na SHANGAZI
KWAKO shangazi. Nilioa mwanamke ambaye alikuwa amezaa mtoto na mpenzi wake wa awali. Nilimkubali pamoja na mtoto wake na baadaye tukapata mwingine. Sasa aliyekuwa mpenzi wake anataka kumchukua mtoto waliyezaa pamoja ilhali nimegharamia malezi yake kwa miaka mitatu sasa. Hiyo ni haki kweli?
Kupitia SMS
Ingawa mwanamume huyo ndiye baba ya mtoto, walimzaa kutokana na uhusiano wa kimapenzi wala si ndoa. Kama wangekuwa wameoana, angekuwa na haki kwa mtoto huyo, lakini sasa hana haki kwa sababu uhusiano wao ulimalizika na akamuachia mtoto mwanamke huyo. Kama ulifuata utaratibu unaofaa kumuoa, mtoto huyo sasa ni wako kisheria.
Nilimuoa baada ya kuzaa naye na sasa nahisi simtaki tena, nifanye nini?
Hujambo shangazi? Kuna msichana tuliyekuwa wapenzi tukiwa shuleni na tukazaa mtoto pamoja. Nilijitolea kugharamia malezi ya mtoto wetu na baadaye nikamuoa kwani niliamini kuwa ninampenda. Tumekuwa pamoja kwa mwaka mmoja sasa na nimegundua sina hisia kwake. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Mapenzi ya dhati hayawezi kutoweka ghafla tu bila sababu. Hali hiyo mara nyingi hushuhudiwa katika uhusiano uliotokana na mambo mengine badala ya mapenzi ya dhati. Kama hiyo ndiyo hali yako, haina maana muendelee kupoteza wakati wenu katika ndoa ya kujilazimisha. Mwambie ukweli ili ajue la kufanya.
Anataka kukagua mzinga wa asali lakini mie naogopa mimba, itakuwaje?
Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 25 na nilimaliza masomo katika chuo kikuu mwaka uliopita. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye tumejuana kwa mwaka mmoja. Anataka nimpe mahaba lakini nahisi kuwa siko tayari. Sababu ni kuwa sijawahi kushiriki jambo hilo na pia naogopa kupata mimba kabla ya ndoa. Tafadhali naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Mtu aliye na mapenzi ya dhati anafaa kuwa na subira kwa mwenzake. Umeelezea sababu zako za kutoweza kumtimizia ombi lake na zinaeleweka. Iwapo hujamwambia, ni muhimu umwelezee. Kama kweli anakupenda ataelewa kisha angojee hadi utakapokuwa tayari.
Jamani amekatalia asali sasa nashuku kuwa ana mwingine
Hujambo shangazi? Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miezi sita sasa. Ajabu ni kuwa mpenzi wangu amekataa kabisa kunipa raha na hilo linanifanya nishuku kuwa ana mwingine. Nampenda sana na sitaki kumuacha. Nishauri.
Kupitia SMS
Hali kwamba amekunyima raha haina maana kuwa ana mwingine. Unasema mmejuana kwa miezi sita pekee na huo ni muda mfupi sana hata hamjafahamiana vyema. Nenda taratibu.
Lo! Nina umri wa miaka 36 na mwanamume hatoi mpango wowote kuhusu penzi letu!
Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 36. Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka minne sasa. Mwanamume mpenzi wangu hajaniambia chochote kuhusu ndoa na nahisi kuwa umri wangu umeenda sana, ninastahili kuwa na familia. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Uhusiano wa dhati wa kimapenzi unafaa kuzaa ndoa. Maelezo yako yanaonyesha wazi kuwa unampenda kwa dhati mpenzi wako na nia yako kwake ni kuishi pamoja. Muda wa kuchumbiana ambao mmekuwa pamoja unatosha kwa sasa mnafaa kuwa mmepanga ndoa. Ushauri wangu ni kwamba umuulize mwenzako kuhusu suala hilo ili ujue msimamo wake ndipo uweze kufanya uamuzi unaofaa.
Simuelewi, hapokei simu na hajibu SMS
Vipi shangazi? Nina mwanamume ambaye nampenda sana lakini nikimtumia ujumbe wa SMS hajibu na pia nikimpigia simu hataki kupokea. Nishauri.
Kupitia SMS
Inaonekana mwanamume huyo hana haja na wewe na haina maana uendelee kujipendekeza kwake. Hisia za kimapenzi zinafaa kutoka pande zote wala si mmoja.