Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke adai kuishiwa na hamu hataki hata kuguswa!

July 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina mke ambaye tumeishi katika ndoa kwa miaka 15. Tatizo ni kwamba siku za hivi karibuni inabidi nimlazimishe kunihudumia chumbani. Amekuwa akidai eti hana hamu, hata kumgusa huwa hataki kabisa. Sasa nafikiria kumuacha nitafute mke mwingine. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ni muhimu uelewe kuwa mwili huchoka jinsi umri unavyozidi. Masuala ya chumbani hutegemea hali ya kimwili na mawazo pia. Badala ya kutishia kumuacha ili utafute mwingine, unafaa umuelewe na kumvumilia mke wako. Miaka 15 ya ndoa ni muda mrefu sana na ninaamini kuwa amekuwa akikuhudumia vyema chumbani kwa muda wote huo.

 

Tumejaaliwa watoto watano, shida ni mume asiyepisha rinda

Habari zako shangazi? Nimeolewa na nina watoto watano. Hata hivyo, mume wangu amenizidi umri kwa miaka kadhaa. Tatizo pekee ni kwamba anapenda sana wanawake, hapendi kuona rinda likimpita. Tabia yake hiyo imekuwa kizingiti kwa ndoa yetu kwani tunagombana kila mara. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hali kwamba mmepata watoto watano na mume wako ni thibitisho kwamba mmekuwa katika ndoa kwa muda mrefu. Kulingana na maelezo yako, mume wako amekuwa na tabia hiyo kwa muda wala hakuanza jana. Kwa sababu hiyo, sielewi ni kwa nini umeamua kumvumilia kwa muda wote huo. Ndoa ikikosa uaminifu huwa si ndoa tena na kama mume wako ameshindwa kujirekebisha una haki ya kujiondoa. Changamoto pekee inaweza kuwa jinsi ya kugharamia maisha yako na watoto wako.

 

Nimemzalia watoto wawili sasa nimegundua ana mke, nifanyeje?

Kwako shangazi. Nimependana na mwanamume fulani na sasa tumezaa pamoja watoto wawili. Tulipokutana mara ya kwanza hakuniambia kuwa ana mke, nimegundua majuzi tu. Nifanye nini na sitaki kuolewa mke wa pili?

Kupitia SMS

Unafaa kujilaumu mwenyewe kwa kukubali kuzaa na mwanamume ambaye ni mpenzi tu wala hajakuoa. Isitoshe, hukujipa muda wa kutosha kumchunguza kikamilifu kabla hujamzalia watoto. Ungefanya hivyo ungejua mapema kuwa ana mke kisha uwachane naye. Sasa huna budi kubeba mzigo wako.

 

Nimeolewa na kibabu juzi nilijishindia rika langu, ila ni kupe!

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 32 na nimeolewa na mwanamume mzee sana. Nimepata mwanamume wa rika langu na nimempenda sana. Shida ni kuwa kila tunapokutana huwa anataka nitumie pesa zangu kugharimia kila kitu; hasa chakula na vinywaji. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Umemuona mume wako akiwa mzee sana na sasa umeamua kuwa na mpango wa kando? Siwezi kuunga mkono jambo kama hilo mimi. Ulimpenda mume wako huyo ukijua kuwa ni mzee na unamfaa kumkubali alivyo, kumheshimu na kuheshimu ndoa yenu. Kama hutaki ndoa hiy,o ni heri umwambie ukweli ili muachane badala ya kumcheza na wanaume wa pembeni. Kama huna habari, mwanamume huyo wa kando anahisi kuwa ana haki ya kutumia pesa zako kwa sababu wewe ndiye unayehitaji huduma zake zaidi.

 

Mchumba hataki kukutana na wazazi ili tuhalalishe ndoa

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na uhusiano na mwanamke fulani kwa miaka miwili sasa na tayari ana mimba yangu. Nimejitolea kumpeleka kwetu kumtambulisha kwa wazazi ili tuhalalishe ndoa yetu lakini hataki. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mwanamke huyo hayuko tayari kuolewa nawe na ndiyo maana hataki mipango ya ndoa. Keti chini naye mshauriane kuhusu jambo hilo ili ujue msimamo wake. Kama kweli hataki ndoa, itabidi muachane. Lakini ni lazima ukubali kuwajibika kwa malezi ya mtoto atakapozaliwa.