SHANGAZI AKUJIBU: Mke ananikosesha amani kwa kuwachukia wanangu
Na SHANGAZI
HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 59. Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu aliaga dunia na kuniacha na watoto wetu wanne. Baadaye nilimuoa mwanamke mwingine aliye na watoto watatu. Maisha yalikuwa mazuri katika miezi michache ya kwanza ya ndoa yetu. Lakini miaka miwili baadaye mambo yamebadilika, maisha yamekuwa balaa tupu. Mke wangu huyo hapendi kabisa kuwaona wala kusikia nikiwataja watoto wangu. Nikiwa nyumbani huwa ni kelele tu, sina amani. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Kutokana na maelezo yako, inaonekana mke wako alikubali ndoa hiyo, si kutokana na mapenzi, labda alitaka tu umsaidie kulea watoto wake. Na hata kama anakupenda ni makosa makubwa kuwabagua watoto wako kwa sababu hiyo ni damu yako. Mbali na kuwadhulumu watoto wako, umri wako umesonga na kelele zake zinaweza kuathiri vibaya afya yako. Kama unaweza, achana naye na utafute maisha yenye amani pamoja na watoto wako.
Amejaa mahaba na huutuliza moyo wangu, sijui nimuoe mke wa pili?
Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 38, nimeoa na tumejaliwa watoto wawili. Nimekuwa na mpango wa kando kwa miaka minne sasa. Nililazimika kufanya hivyo kwa sababu mke wangu huwa hana shughuli nami chumbani na kila mara huwa analalamika eti amechoka na hana hisia za shughuli hiyo. Kwa upande mwingine, yule wa pembeni hunipa raha na kunifikisha kileleni. Licha ya uhusiano wetu, anamheshimu mke wangu na huniambia nisiwahi kumuacha wala kumtesa. Je, nimuoe mke wa pili?
Kupitia SMS
Ingawa unamlaumu mke wako kwa kushindwa kukutimizia wajibu wake wa chumbani, hujamwambia hatua ambayo umechukua kutokana na udhaifu wake huo. Kabla hujaingilia uhusiano nje ya ndoa, ungeshauriana naye kuhusu jambo hilo, labda angetafuta namna ya kujirekebisha. Kama umeamua kuwa uliye naye ndiye anayekufaa, ni muhimu mke wako ajue kuhusu mipango yako ili naye aweze kufanya uamuzi wake.
Nimechanganyikiwa kwa kuambukizwa HIV na mpenzi, sasa sijui nitafanya nini
Shikamoo shangazi! Nimejipata taabani kutokana na mapenzi. Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja. Mwezi uliopita nilimtembelea mpenzi wangu nyumbani kwake na nikapata dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi. Nilipomuuliza alinidanganya kuwa ni za rafiki yake. Niliamua kwenda kupimwa na nikapatikana na virusi. Nilirudi kwake nikamwambia ndipo akakiri kuwa anaugua. Nimechanganyikiwa sana, sijui nitafanya nini?
Kupitia SMS
Kuna usemi kuwa maji yakimwagika hayazoleki. Licha ya masaibu yaliyokupata, nitakulaumu wewe kwa kushiriki mapenzi bila kutumia kinga ilhali unajua tunaishi enzi za Ukimwi na magonjwa mengine ya zinaa. Kama wewe na mpenzi wako hamkutaka kutumia kinga, mngepimwa kwanza kujua hali yenu ili kuepuka janga ambalo limekupata. Itabidi uende hospitalini kwa ushauri kuhusu hali yako kisha uwekwe katika mpango wa kutumia dawa. Kwa njia hiyo, utaweza kuishi maisha ya kawaida.
Nikizungumzia ndoa yeye hunipeleka kwa rafiki yake na si kwao, je, ananificha jambo?
Kwako shangazi. Nina mpenzi lakini kuna jambo fulani ambalo sielewi kumhusu. Kila tukipanga tuonane huwa ananipeleka nyumbani kwa rafiki yake. Nimekuwa nikitaka kujua kwao lakini amekuwa akinipa vijisababu. Inawezekana kuna kitu ananificha?
Kupitia SMS
Ni wazi kuwa mpenzi wako hataki ujue kwao kwa sababu anayoijua mwenyewe. Mojawapo ya sababu hizo na ambayo inaweza kuathiri uhusiano wenu ni kwamba huenda ameoa na bila shaka anajua ukienda kwao utajua. Ni muhimu uzungumze naye akuelezee ana mpango gani na pia ufanye juhudi zako mwenyewe ujue kwao ili upate ukweli wa jambo hilo.