• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
SHANGAZI AKUJIBU: Mke ataka tulishane mahaba tu, anikataza kuenda kazini

SHANGAZI AKUJIBU: Mke ataka tulishane mahaba tu, anikataza kuenda kazini

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nimeoa kwa karibu mwaka mmoja sasa na tunapendana sana na mke wangu. Hata hivyo, nahisi kuwa mapenzi yake kwangu yamekiuka mipaka. Sababu ni kuwa yeye hana kazi na mara kwa mara amekuwa akinikataza kuenda kazini ili tushinde pamoja nyumbani tukilishana mahaba. Ninahofia kuwa nikiendelea hivyo nitapoteza kazi lakini pia sitaki mke wangu ahisi kana kwamba simpendi. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Hata kama ni mapenzi, hayo yake yamepita kiasi. Ni ajabu kuwa hatosheki kuwa nawe unapotoka kazini hadi usiku kucha na pia siku za wikendi. Ni muhimu umwelezee hofu yako na wakati huo huo kumhakikishia penzi lako. Ukweli ni kuwa leo ukifutwa kazi mtalala njaa kwani mapenzi hayaliwi. Hasa, siku atakayolala njaa mapenzi yake hayo yatayeyuka kama theluji ikichomwa na jua. Chunga kazi yako.

 

Katika miaka 5 ameonja asali mara moja tu, kunani?

Nimependana na mwanamume fulani na ameniahidi kuwa atanioa. Ameonja asali mara moja tu katika miaka mitano ambayo tumekuwa wapenzi. Nimekuwa nikitaka sana tuburudike tena lakini amekataa. Simuelewi kabisa kwani hiyo si hali ya kawaida kwa mwanamume. Unadhani ni kwa nini amekuwa hivyo?

Kupitia SMS

Ni kweli kuwa si hali ya kawaida kwa mwanamume kubembelezwa kuhusu jambo hilo na mara nyingi huwa ni kinyume chake. Sijui mwenzako amekuwa akikupa sababu gani ya kukataa ombi lako ilhali alikubali mara ya kwanza. Labda ameamua kujiondoa katika uhusiano huo na anatumia hiyo kama njia ya kukuambia. Itakuwa vyema umuulize ili ujue kiini cha msimamo wake huo.

 

Mume ananilaumu kushindwa kuzaa na atisha kuniacha pia

Hujambo shangazi? Tafadhali mwenzangu ninahitaji msaada wako. Nimeolewa kwa miaka miwili na bado sijapata mtoto. Sasa mume wangu ameanza kulalamika na kunilaumu kwa kushindwa kumzalia na anatishia kuniacha. Nampenda sana na sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Ni makosa kwa mume wako kuamua kuwa wewe ndiye ambaye umeshindwa kumzalia. Sababu ni kuwa wanaume pia hukosa uwezo wa kuzalisha na hali hiyo imethibitishwa kisayansi. Isitoshe, wawili wanapooana huapa kuishi pamoja kwa upendo katika uzima na magonjwa, utajiri na umaskini. Hata ikibainika kuwa huna uwezo wa kupata mtoto, mume wako hafai kutumia hali yako hiyo kuwa sababu ya kukuacha kama kweli anakupenda. Liwe liwalo, kama ameamua hivyo ni sawa. Lakini kabla hajachukua hatua hiyo, mshauri muende hospitalini kwanza ili mpimwe mjue palipo na shida. Huenda ni hali inayoweza kutatuliwa ili muweze kupata watoto.

 

Rafiki amtamani sana mpenzi wangu, anitia kiwewe kweli

Shikamoo shangazi! Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye tunapendana sana. Hata hivyo, mwanamke rafiki yangu anamtaka na ameniambia hivyo tena mara kadhaa. Mimi sina kinyongo naye kwa kuwa mpenzi wangu alitupata bado tukiwa marafiki lakini akanichagua mimi badala yake. Je, anaweza kunipokonya mpenzi?

Kupitia SMS

Nia ya mwanamke huyo inafanya urafiki wenu kuwa sawa na wa chui na kondoo. Ni jambo la kushangaza kuwa rafiki yako huyo anammezea mate mpenzi wako kiasi cha kukuambia wazi. Hiyo ina maana kuwa anaweza kutumia mbinu yoyote ile, hata dawa, ili kumpata mwanamume huyo. Inaonekana unamwamini sana mpenzi wako na ndiyo maana umeamua kupuuza matamshi ya rafiki yako ili kudumisha urafiki wenu. Ingawa hivyo, ni muhimu uwe mwangalifu sana kwa sababu umejua kuwa rafiki yako huyo pia ni adui wako.

  • Tags

You can share this post!

Tunisia yazamisha Ghana na kujikatia tiketi ya nane-bora

Wezi watumia misongamano kupora vipuri vya magari jijini

adminleo