Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke wa mtu asema ananitaka, yuko tayari kufanya chochote kunipata

July 19th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 25 na nina mpenzi tunayependana sana. Hata hivyo, kuna mwanamke jirani yangu mtaani anayeniambia halali kwa kuniwaza ingawa ni mke wa mtu. Nimemwambia nina mpenzi lakini hataki kusikia na ameapa kuwa ni lazima atanipata. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Unajua vizuri kuwa mwanamke huyo hawezi kukulazimisha kuwa na uhusiano naye hata kama anakupenda kama nini. Kama hataki kuelewa kuwa una mpenzi na huna nafasi ya mtu mwingine katika moyo wako, muache aendelee kuhangaika, mwishowe atachoka atulie kwa mume wake.

 

Nataka mpenzi lakini bado niko kwa wazazi

Shikamoo shangazi! Nilimaliza shule ya upili mwaka mmoja uliopita na ninasuburi kujiunga na chuo kikuu. Natamani sana kuwa na mpenzi lakini tatizo ni kuwa ninaishi katika nyumba ndogo na wazazi wangu na pia ninalala chumba kimoja na kaka yangu mdogo hivi kwamba hata nikipata mpenzi siwezi kumualika kwetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hiyo ni hali inayowakumba vijana wengi hasa wanaoishi mijini ambako kodi ya nyumba ni ghali kwa hivyo wanaishi katika nyumba ndogo pamoja na watu wa familia zao. Sidhani ni lazima umualike mpenzi wako kwenu kwa wakati huu kwani bado unasoma na huna mpango wa kuoa. Mnaweza kuendelea kukutana mahali kwingine hadi wakati utakapopata kazi na kuanza kuishi kwako.

 

Aliyenipa penzi miaka mitatu ameoa mwingine

Shangazi pokea salamu zangu za dhati. Kijana aliyenipa mahaba kwa miaka mitatu tukiwa wapenzi aliamua kuoa mwanamke mwingine. Hatua yake hiyo ilinikasirisha kwa siku chache lakini hisia zangu kwake zimerudi tena zikiwa nzito ajabu. Nimemwelezea na ananiahidi eti niwe na subira atanioa. Nimechanganyikiwa.

Kupitia SMS

Nashangaa kwamba umefungwa macho na mapenzi ya kijana huyo kiasi cha kukaidi ukweli ulio wazi. Bila shaka amejua udhaifu wako na ndiyo maana anaendelea kukuhadaa ukiangalia tu. Kama alikuacha akaoa mwanamke mwingine, unatarajia kwamba atamuacha kisha akuoe? Utangoja! Ningekuwa wewe ningemzika katika kaburi la sahau nijitafutie maisha kwingine.

 

Tunapanga ndoa na nimesikia anachovya buyu la mke wa mtu!

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 26 na kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu sasa. Ameahidi kunioa na nimeshangaa kusikia kutoka kwa watu wanaomjua kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mke wa mwenyewe. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama habari hizo ni za kweli, basi huyo ni mwanamume hatari kuwa naye. Chunguza kwa makini na ukithibitisha umuepuke kabisa kwani itakuwa wazi kwamba hakupendi kwa dhati bali anachezea maisha yako tu.

 

Yeye ni mtu twafanya mambo mengi pamoja ila amekatalia asali

Vipi shangazi? Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na tunasoma pamoja na mwanamke mpenzi wangu. Tunapendana sana na tufanya mambo mengi pamoja. Ajabu ni kwamba amekataa kabisa tushiriki burudani akidai eti wakati haujafika. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kila jambo lina wakati wake na mpenzi wako anajua hivyo ingawa wewe unaonekana kutoelewa. Mapenzi ya dhati yana subira kwa hivyo huna budi kukubaliana naye iwapo unampenda.

 

Naambiwa ana mke aliyemtupa ushagoo

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanaume tunayefanya kazi pamoja na amekuwa akiahidi kuwa atanioa. Lakini mwanamume rafiki yake amenidokezea kuwa ameoa na mkewe anaishi mashambani. Nimemuuliza akakana na nimeamua kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Si jambo la busara kutegemea habari za watu kufanya uamuzi kama huo kwa sababu wanaweza kukuhadaa. Sijui ni kwa nini unaonekana kuwa na hakika kwamba mpenzi wako ana mwingine ilhali umeambiwa tu. Nakushauri uchunguze mwenyewe hadi umfumanie ndipo uchukue hatua hiyo.