Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa kando hukasirika nikimpigia simu mke wangu

April 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

SHANGAZI pokea salamu zangu. Nina mke lakini pia nina mpenzi wa pembeni. Tatizo ni kwamba mpenzi wangu huyo huona vibaya kila nikimpigia simu mke wangu tukiwa pamoja. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi katika ukumbi huu kwamba watu wanaoanzisha uhusiano na wengine waliooa au kuolewa huwa hawana nia njema kwa ndoa zao, na wakipata nafasi watazivuruga na kuzivunjilia mbali. Hali kwamba mpenzi wako hukasirika ukimpigia simu mke wako ni ishara kamili kuwa anamchukia, na akipata nafasi nzuri atawatenganisha ili abaki yeye. Mpenzi wa pembeni ni wa nini ilhali umeoa?

 

Mke aniaibisha kwa wazazi wake

Habari shangazi? Nina mke niliyemuoa miaka miwili iliyopita na tuna mtoto mmoja. Siku za hivi majuzi mwenzangu amebadilika sana kwani hanisikii na ameanza kufuata ushauri wa wazazi wake na pia anaomba pesa kutoka kwao akisema mimi ni maskini. Ukweli ni kuwa ninampa kila kitu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inaonekana masaibu yanayokumba ndoa yenu yamechochewa na wazazi wa mke wako. Ushauri wao kwake na pesa wanazompa zimemfanya afure kichwa na ndiyo maana ameanza kukudunisha na kukuita maskini. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ameamua kutoka katika ndoa hiyo na huenda dharau anayokuonyesha ni mbinu ya kukuchokoza ili mkosane apate kisingizio cha kukuacha. Jitayarishe kwa hilo.

 

Tunahusiana kiukoo

Shikamoo shangazi! Nilikutana na msichana fulani miezi miwili iliyopita nikampenda na nilipomdokezea nia yangu akakubali. Hata hivyo, katika ile hali ya kujuana nimegundua kuwa tuna uhusiano wa kiukoo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uhusiano wa kiukoo ni tofauti na uhusiano wa damu. Mnaweza kuwa watu wa ukoo mmoja lakini msiwe na uhusiano wa damu. Kama uhusiano wenu ni wa kiukoo tu si wa damu, mnaweza kuendelea na uhusiano wenu. Kabla hamjaenda mbali katika uhusiano wenu, ni muhimu muulize wazazi au jamaa zenu ili mjue iwapo mna uhusiano wa damu.

 

Ninaumia moyoni kwa kuachwa ghafla

Kwako shangazi. Msichana ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu aliniita nyumbani kwake majuzi na kuniambia kuwa hanitaki tena. Uamuzi wake huo wa ghafla umenishtua sana na kuniachia maumivu moyoni. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaelewa kuwa inauma sana mtu kuachwa ghafla na mpenzi wake tena bila sababu. Hata hivyo, fahamu kuwa uhusiano unategemea hiari ya mtu na akiamua kuwa hataki kuendelea nao ana haki ya kujiondoa. Kubali uamuzi wake na uendelee na maisha yako.

 

Nisaidie na mistari ya kutuliza mpenzi wangu

Shikamoo shangazi! Tafadhali nakuomba unifanyie hisani. Naomba tu unitumie maneno matamu ya kimapenzi ili nimtumie wangu mpenzi afurahi. Ninaamini akiyapata atalala unono na kunipenda hata zaidi.

Kupitia SMS

Samahani mwenzangu lakini hilo mimi sitaweza. Sababu ni kuwa, huyo ni mpenzi wako na ni wewe mwenyewe unayefaa kutafuta hayo maneno matamu ya kumwambia ili kuchochea mahaba yenu. Kwako kuniomba nikutafutie maneno hayo ni uzembe tu, hutaki kuwa mbunifu.

 

Nimeolewa lakini hatujafahamisha wazazi wetu

Mambo shangazi? Nimeolewa kwa mwezi mmoja sasa na wazazi wa mume wangu bado hawajaenda kwetu. Wamekuwa wakiahidi kufanya hivyo lakini kila wakipanga wanapangua. Sitaki kuendelea kuishi na mwanamume ambaye wazazi wangu hawamjui. Nifanye nini?

Msimamo wako huo ni mwema na ndio unafaa. Bila shaka wazazi wa mume wako wanahitaji zawadi au sehemu ya mahari kuwapelekea wazazi wako, na labda wamekawia kwa sababu hawajakuwa tayari. Hata hivyo usilegeze kamba. Shirikiana na mume wako kuwasukuma hadi watimize mpango huo ndipo uweze kutulia ukijua umeolewa kihalali.