SHANGAZI AKUJIBU: Mwanamume nimpendaye amezingirwa na vidosho
Na SHANGAZI
SHANGAZI pokea salamu zangu. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nimempenda kwa moyo wangu wote na ningependa tuwe pamoja maisha yetu yote. Yeye ni mfanyabiashara na ameajiri wanawake wengi warembo katika biashara yake. Sasa hofu yangu kubwa ni kwamba anaweza kunaswa na mwingine aniache. Mimi pia ni mrembo lakini bado sijiamini. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Kosa kubwa wanalofanya watu wengi ni kutojiamini. Ni muhimu sana ujiamini katika mambo yote unayofanya maishani la sivyo utashindwa kutimiza malengo yako mengi. Kumbuka kuwa kabla ya mwanamume huyo kukudokezea penzi lake, alikuwa amekutana na wanawake wengi warembo lakini akaamua ni wewe anayetaka. Kama uhusiano wenu bado ni thabiti na hujaona dalili zozote mbaya, huna sababu ya kuwa na wasiwasi.
Nimetambua hakuna mrembo asiye na doa
Habari yako shangazi. Nina umri wa miaka 30 na bado sijaoa ingawa nimekuwa nikitafuta mchumba. Ukweli ni kwamba nimekutana na wanawake kadhaa lakini sijapata anayenifaa. Hasa, nimegundua kuwa hakuna mwanamke mrembo asiyekuwa na kasoro. Je, nitaishi bila mke? Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Ni haki yako kumpata mke mwenye sifa unazotaka ndipo uweze kufurahia ndoa yako. Shughuli hiyo ya kutafuta mwenzako wa maisha si rahisi na inahitaji subira. Pili, nakuonya tu kuwa kama unatafuta mwanamke asiye na kasoro hutampata kwani hakuna mtu asiye na kasoro hata wewe mwenyewe.
Alipewa udaku akaniacha ghafla
Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitano sasa lakini ameniacha ghafla. Sababu yake kuniacha ni rafiki yake mdaku ambaye alimhadaa eti nina mpenzi mwingine. Ukweli ni kuwa ninampenda kwa moyo wangu wote na kwa muda huo nimemjua yeye tu wala sina mwingine. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Ni ajabu kubwa kwamba mpenzi wako ameamua kujiondoa katika uhusiano wenu kutokana na udaku wa rafiki yake. Nguzo kubwa katika uhusiano wa kimapenzi na ndoa inafaa kuwa uaminifu kati ya wahusika. Kama mpenzi wako alichagua kumwamini rafiki yako kuliko wewe, basi hastahili kuwa mpenzi wako. Subiri uone kama atarudi kuomba msamaha na asipofanya hivyo, umsahau uendelee na maisha yako.
Aliramba asali kiporo ila asema aliteleza tu
Shikamoo shangazi! Nilikosana na mpenzi wangu nilipogundua kuwa alishiriki mahaba na mpenzi wake wa zamani. Amerudi kwangu kuomba msamaha akisema hakufanya hivyo kwa kupenda, eti aliteleza tu. Naomba ushauri wako shangazi kwa kuwa bado nampenda sana.
Kupitia SMS
Hakuna binadamu asiyekosea. Msamaha ni mojawapo ya nguzo muhimu katika uhusiano. Hali kwamba mpenzi wako amerudi kwako kuungama kwamba alikosa na ameomba msamaha ni thibitisho kwamba anakupenda. Tathmini moyoni iwapo unaweza kumpa nafasi nyingine kwani wewe pia unasema unampenda. Kuna usemi kuwa kutenda kosa si kosa, kosa ni kurudia.
Miaka imegonga 30 na sina hamu wala hisia kwa wanaume
Vipi shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 30. Sijaolewa wala sijawahi kuwa na mpenzi maishani mwangu. Sababu ni kwamba huwa sina hisia zozote kwa wanaume ingawa kuna wengi ambao wamekuwa wakiniomba mapenzi. Nina marafiki kadhaa wa kiume mahali ninakofanya kazi lakini mwanamume akinitajia kuhusu mapenzi huwa nakasirika sana. Sielewi shida yangu hasa ni nini. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Hisia za kimapenzi hutegemea maumbile ya mtu binafsi na mazingira ambayo amelelewa. Ukweli ni kuwa hisia hizo huja zenyewe, haziwezi kulazimishwa kwa hivyo hali yako hiyo isikutie hofu. Kuwa na subira na hatimaye zitakuja ili uhisi hamu ya kupenda na kupendwa pia.