SHANGAZI AKUJIBU: Naogopa kumpoteza mwana wa mpenzi wangu tukioana
Na SHANGAZI
HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 32 na nimependana na mwanamke aliye na mtoto wa miaka mitatu kutokana na uhusiano wa awali. Nimekuwa nikimtembelea nyumbani kwake na tunapendana sana na mtoto wake huyo hadi nahisi kama ni wangu kumzaa. Hofu yangu ni kuwa nikimuoa hatimaye mtoto atatuacha na kurudi kwa baba yake mzazi. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Kulingana na maelezo yako, huna sababu ya kuwa na wasiwasi. Sababu ni kuwa mtoto huyo bado ni mdogo hajaanza kufikiria kuhusu asili yake. Pili unasema kuwa umeweza kujenga uhusiano wa karibu kati yako naye. Inawezekana kwa mtoto kumpenda baba yake wa kambo kuliko baba mzazi. Mara nyingi hali hiyo hutegemea na jinsi baba wa kambo anavyomchukulia mtoto huyo. Ukimpenda kama wako kumzaa, yeye pia atakupenda na mtakuwa na uhusiano thabiti na wa kudumu. Kwa sababu hiyo, huna cha kuogopa bora tu udumishe uhusiano wenu huo.
Ni mwaka wa tatu na amebana chungu cha asali, nifanyeje?
Kwako shangazi. Huu ni mwaka wa tatu nikiwa katika uhusiano na mwanamke tunayependana sana. Kusema kweli mpenzi wangu amekuwa akinionyesha mahaba kwa kila namna isipokuwa tu amekataa kabisa na asali nami natamani sana kuonja. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Uhusiano wa kudumu huongozwa na mapenzi wala si tamaa. Iwapo kweli unampenda mwenzako kwa dhati, sielewi ni kwa nini umeingiwa na tamaa ya kulamba asali. Je, yako ni mapenzi ama ni tamaa? Mtu anayempenda mwingine anaweza kusubiri hadi mwenzake atakapokuwa tayari kwa jambo hilo. Akishuku kuwa unafuata asali tu huenda akauacha.
Tabia ya mke wangu yanitia wasiwasi, nahisi kuna jambo
Kwako shangazi. Nimeoa na ninafanya kazi mbali na nyumbani. Nimeanza kumshuku mke wangu kwa sababu mara nyingi nikimpigia simu huwa hashiki na hatimaye nikimpata na kumuuliza ni kwa nini hunipa sababu ambazo mimi siziamini. Nishauri.
Kupitia SMS
Iwapo hujawahi kumshuku mke wako, huna sababu ya kumshuku bila sababu ya maana. Mwanamke akiwa nyumbani huwa na kazi nyingi na ni rahisi simu kupigwa akose kuisikia. Iwapo unashuku kuna mambo yasiyofaa yanayofanya akose kushika simu zako, anza kumtembelea nyumbani ghafla bila kumwambia. Kama ana mambo yake, siku moja utamfumania.
Mpenzi hapokei simu na hajibu SMS zangu au amepata mpya?
Kwako shangazi. Mpenzi wangu wa miaka mitatu ametoweka ghafla katika maisha yangu. Wiki moja sasa imepita hajanipigia simu wala kunitumia SMS. Mimi mwenyewe nimempigia simu na kumtumia SMS mara nyingi lakini hajibu. Inawezekana kuwa amepata mwingine?
Kupitia SMS
Hizo ni dalili za kutosha kwamba mpenzi wako amekuacha lakini hataki kukwambia ukweli huo. Inawezekana amepata mwingine ama ameamua tu kwamba hataki tena uhusiano kati yenu. Itakuwa bora ukubali kuwa uhusiano wenu umekwisha ndipo uweze kumtoa katika mawazo na kuendelea na maisha yako.
Jamaa ataka tuvunje uhusiano kwa kuwa nimepata kazi mbali
Mambo shangazi? Nimehamishwa kikazi nikapelekwa mbali na mpenzi wangu. Jambo hilo limemuathiri vibaya mwenzangu hadi anapendekeza kwamba tuvunje uhusiano wetu. Hofu yake kuu ni kuwa nitapata mwanamume mwingine ninakoenda. Nimemhakikishia kuwa nitaendelea kuwa mwaminifu kwake lakini haniamini. Nifanye nini?
Kupitia SMS
Huo ni wivu wa kimapenzi na ishara kuwa mpenzi wako anakupenda kwa dhati. Ukweli ni kuwa anashuku tu kuwa utapata mwingine wala hana hakika. Isitoshe, anajua unampenda kwa dhati na umemhakikishia uaminifu wako kwake. Pendekezo lake hilo ni namna ya kupima hisia zako kwa hivyo usikubali. Ninaamini kuwa muda si mrefu atazoea hali hiyo na mawazo hayo kumuondoka.