• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
SHANGAZI AKUJIBU: Ninampenda lakini nahisi ananidharau na kuniona fukara

SHANGAZI AKUJIBU: Ninampenda lakini nahisi ananidharau na kuniona fukara

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye ninampenda kwa dhati na nia yangu hasa ni kumuoa. Hata hivyo, kuna jambo fulani ambalo linanitia hofu kuhusu hatima ya uhusiano wetu. Mpenzi wangu ana kazi nzuri na yenye mshahara mkubwa. Mimi nimeajiriwa kuuza katika duka na mshahara wangu ni mdogo. Kwa muda ambao tumekuwa pamoja, nimegundua kuwa mpenzi wangu ananichukulia kuwa mtu duni kutokana na kazi yangu na mapato yangu madogo. Ninampenda sana lakini pia siwezi kuishi na mke asiyeniheshimu. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume aliumbwa kuwa kichwa nyumbani kwake na anastahili heshima hata kama ni maskini bora tu anajitahidi ipasavyo kukimu familia yake. Anapokosewa heshima, ndoa hiyo haiwezi kuwa na amani. Itabidi uchague kati ya mapenzi uliyo nayo kwake na heshima ambayo unastahili kutoka kwake akiwa mke wako.

 

Wazazi wa mume hawajanikubali

Shangazi pokea salamu zangu. Nimeolewa na mwanamume aliyekuwa ameoa mwanamke mwingine lakini wakaachana. Mimi pia nilikuwa nimeolewa na nikaachana na mume wangu nikiwa na watoto wawili. Mume wangu anawapenda watoto hao kama wake mwenyewe. Tatizo ni kuwa wazazi wake hawajanikubali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa mume wako ni mtu mzima na mwenye akili timamu kwa hivyo wazazi wake hawafai kuingilia maisha yake ya ndoa. Ni haki yake kuchagua mwanamke anayemtaka kuwa mke wake. Pili, kama mnaishi kwa amani na mume wako, msimamo wa wazazi wake kukuhusu haufai kukuhangaisha moyoni. Mtoto wao alikupenda mwenyewe wala hukumlazimisha.

 

Nahofia ataniwacha akimaliza masomo ambayo nimeyalipia

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi tunayependana kwa dhati. Nimekuwa nikimsaidia kugharamia masomo yake kwa sababu anatoka familia maskini na pia ninaamini hatimaye atakuwa mke wangu. Lakini marafiki zangu wananishauri niache kutumia pesa zangu kwake kwa sababu huenda akaniacha akimaliza masomo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Usiwaruhusu marafiki zako waingilie uhusiano wenu. Huyo ni mchumba wako na umeamua kumsaidia kwa sababu unaamini atakuwa mke wako. Hata akibadili nia baadaye, utakuwa umemsaidia na hiyo itakuwa baraka kwako. Isitoshe, unatumia pesa zako kwa hivyo hawana sababu ya kuingilia mpango huo.

 

Anipendaye alikuwa na mke wakatengana sasa ataka kunioa, je, anaweza kurejea?

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tunayependana na tumekubaliana kwamba atanioa. Hata hivyo nimesikia alikuwa na mke na wakaachana. Sasa naogopa huenda mke wake akarudi na kunipata kwake. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Badala ya kutegemea habari za kuambiwa, ni muhimu umuulize mpenzi wako. Kama kweli alikuwa na mke, thibitisha kutoka kwake na ikiwezekana kutoka kwa jamaa na marafiki zake kwamba wameachana kabisa na hakuna matumaini kwao kurudiana.

 

Aliolewa ila nahisi mahaba niliyompa yatamrejesha kwangu

Shangazi naomba ushauri wako. Kuna mwanamke tuliyekuwa wapenzi lakini akaniacha akaolewa na mwanamume mwingine. Tulipokuwa wapenzi nilimuonyesha mahaba ya hali ya juu na ninaamini hakuna mwanamume mwingine anayeweza kumpa mapenzi kama hayo. Bado sijakata tamaa na nimekuwa nikimtupia chambo kwa matumaini kuwa siku moja nitamnasa arudi kwangu. Nipe ushauri wako.

Kupitia SMS

Hata kama ulikuwa ukimpa penzi tamu kama asali, ni muhimu ujue kuwa huyo sasa ni mke wa mwenyewe na unafaa kuheshimu ndoa yao. Isitoshe, sielewi ni kwa nini alikuacha akaolewa na mwanamume mwingine kama kweli alithamini na kufurahia penzi lako. Nahisi kuwa unapoteza wakati wako kumtupia chambo samaki aliyenaswa kitambo kisha akageuzwa kitoweo. Shauri yako.

You can share this post!

MAPISHI: Jinsi ya kupika mboga mchanganyiko

BONGO LA BIASHARA: Kibanda kandokando ya Barabara Kuu...

adminleo