Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Penzi langu lote liko kwake, lakini ni mchoyo sana

March 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 26 na kuna mwanamume ambaye ninampenda kwa moyo wangu wote. Tatizo pekee ni kuwa anapuuza mahitaji yangu ya kifedha ingawa ninaamini ana uwezo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa wapenzi wanafaa kusaidiana, ukimpenda hufai kuweka maanani jinsi ambavyo utafaidi kifedha kutoka kwake. Huenda mwenzako hajui shida yako hiyo kama hujamwambia. Labda ukimwambia atajitolea kukusaidia kama ana uwezo na iwapo kweli anakupenda.

 

Twapendana hata kama ameoa nami pia nimeolewa

Kwako shangazi. Kuna mwanamume anayenipenda nami pia nampenda ingawa bado hatujaanza uhusiano. Tatizo ni kuwa ana mke na mimi pia nimeolewa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hata kama mnapendana, mnajua kuwa mkianza uhusiano utakuwa haramu. Na kama hujui, mpango wa kando kwa watu walio katika ndoa huwa ndio mwanzo wa mwisho wa ndoa zao. Umeolewa, kwa hivyo acha tamaa na utulie katika ndoa yako.

 

Niliwachanganya wawili na walipojua wakanihepa wote

Vipi shangazi? Nilikuwa nimependana na wasichana wawili kwa wakati mmoja. Kwa bahati mbaya, walijuana na wakatoweka maishani mwangu ghafla hata kwa simu siwapati. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Haikuwa bahati mbaya kwa wasichana hao kujuana bali bahati nzuri ili iwe funzo kwa matapeli wa kimapenzi kama wewe. Suala la mapenzi ni zito na ni makosa kwa mtu yeyote kuchezea hisia za wengine. Mimi sina la kukwambia kwani mwiba wa kujidunga hauambiwi pole. Endelea kujuta kutokana na kitendo chako.

 

Wapi huyo anayesaka?

Hujambo shangazi? Hivi majuzi nilisoma kwenye safu hii kuhusu mwanamke ambaye anatafuta mume. Tafadhali naomba kuwasiliana naye kwa simu ili tujuane nione kama atanifaa.

Kupitia SMS

Samahani, kuna watu wengi wanaotuma jumbe zao hapa wakitafuta wachumba na huwa siweki nambari zao za simu. Hata hivyo, ni matumaini yangu kwamba msichana aliyetuma ujumbe huo atasoma huu wako kisha atafute namna ya kuwasiliana nawe. Kila la heri.

 

Nashindwa kumtoa mawazoni mwangu

Nilikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na kijana fulani lakini nikamuacha alipoanza kunionyesha dharau kwa kutongoza wasichana wengine mbele yangu. Ni miaka miwili sasa tangu nimuache na nimeshindwa kabisa kumsahau kwa sababu ninampenda kwa dhati. Je, nimtafute turudiane?

Kupitia SMS

Ninahisi kuwa kijana huyo alitosheka na penzi lako na kwamba hatua yake ya kuwatongoza wasichana wengine ukiwepo ilinuiwa kukuchukiza ili umuache na hatimaye uliingia katika mtego wake. Sielewi ni kwa nini unataka kujilazimisha kwake licha ya kukutendea hayo. Huenda hata akakutendea mabaya zaidi. Hata kama unampenda, itabidi ukubali kwamba huna nafasi katika moyo wake na utafute mapenzi kwingine.

Hataki kuja kwangu

Vipi shangazi? Kuna msichana ambaye nimekuwa nikimtongoza kwa muda mrefu na hatimaye amenikubali. Amekuwa akiniahidi kuwa atanitembelea nyumbani kwangu lakini hajafanya hivyo. Nashindwa kumuelewa. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama uhusiano wenu bado ni mchanga, huenda msichana huyo anahisi vigumu kukutembelea kwa sababu hajakujua vyema na anahofia usalama wake mikononi mwa mtu mgeni. Ushauri wangu ni kwamba umpe muda mjuane vizuri na kuzoeana, na ninaamini hatimaye atatimiza ahadi yake kwako. Mapenzi ya dhati yanahitaji subira.

 

Ameniambia hataki mapenzi mbali tuwe marafiki tu

Shikamoo shangazi? Nina msichana ambaye tumekuwa marafiki wakubwa kutokana na mazoea ya muda mrefu. Tumekuwa tukiandamana katika sehemu mbalimbali, zikiwemo maskani za starehe na ananichukua kama mpenzi wake. Hatimaye ameteka moyo wangu kimapenzi lakini nilipomwambia juzi alikataa na kuniambia anataka urafiki tu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Urafiki wa muda mrefu kati yako na msichana huyo umekupelekea kudhani kuwa anakupenda na ndiyo maana unashangaa kwamba amekataa ombi lako. Kama hutaki kuharibu urafiki wenu, ni muhimu umwamini, uelewe na kuheshimu msimamo wake.