Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Wazazi wametisha kunilaani nikiolewa na wasiyemtaka

October 7th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 32 na nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani hata tumezaa mtoto pamoja. Tunapendana sana na ameahidi kunioa. Lakini wazazi wangu wamepinga uhusiano huo na wanatishia kunilaani nikiamua kuolewa na mwanamume huyo. Ninawaheshimu sana lakini pia nahisi kuwa wanaingilia haki na uhuru wangu wa kuishi na mwanamume chaguo la moyo wangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kulingana na umri wako, wewe ni mtu mzima na una haki na uhuru wa kujiamulia mambo muhimu kuhusu maisha yako. Mapenzi na ndoa ni mambo muhimu ambayo mtu anafaa kujiamulia yeye mwenyewe bila kuingiliwa na watu wengine. Ni vyema kuwaheshimu wazazi wako lakini tishio lao kwamba watakulaani kwa kuchagua mwanamume wa maisha yako halina msingi. Hiyo itakuwa laana haramu na haiwezi kukuathiri. Endelea na mipango yako, hatimaye watakubali uamuzi wako.

 

Tuliachana nikiwa na wana 4, sasa adai nirudi ilhali ameoa na mie nimepata mume

Shangazi nimekuja kwako unipe ushauri. Nilikuwa nimeolewa lakini tukaachana na mume wangu miaka mitano iliyopita. Nilitoka kwake na watoto wetu wanne na nimepata mume mwingine hivi majuzi. Sasa mume wangu wa awali ametuma mtu kuniambia nirudi kwake ilhali ninajua alioa mwanamke mwingine miaka mitatu iliyopita na tayari wamezaa watoto wawili. Nishauri.

Kupitia SMS

Miaka mitano ya utengano wa mume na mkewe ni muda mrefu sana. Hiyo ndiyo sababu kila mmoja wenu aliamua kuendelea na maisha yake baada ya kuona kuwa hapakuwa na dalili za kurudiana. Hata hivyo, hakuna lisilowezekana ulimwenguni. Iwapo kila mmoja wenu yuko tayari kutoka katika ndoa yake ya sasa ili mrudiane, hiyo ni juu yenu na itakuwa sawa tu bora kuna maelewano.

 

Tabia yake ilinifanya nimtoroke, sasa adai hali shwari turudiane

Kwako shangazi. Ni miezi miwili tangu nilipomuacha mwanamke mpenzi wangu kutokana na tabia yake. Sasa ameanza kunitafuta akisema ameacha tabia hiyo. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea tabia iliyokufanya umuache na jinsi unavyompenda. Kama amekuambia mwenyewe kuwa ameacha tabia hiyo, mpe nafasi uone kama anavyosema ni kweli.

 

Nilimpa mimba kwa nia ya kumuoa akaendea mwingine, sasa ananitaka!

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 36. Nilikuwa na mpenzi niliyempenda kwa dhati na hata nilimpa mimba kwa sababu nilikuwa tayari kumuoa. Ajabu ni kwamba aliniacha akaolewa na mwanamume mwingine. Miaka mitatu baadaye, wameachana na amekuja kwangu akitaka turudiane. Bado sijapata mwingine. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Wakati mwingine sisi binadamu hufanya maamuzi tukidhani ni ya busara kisha kujuta baadaye. Ni lazima kuna jambo au mambo mazuri yaliyomvuta mpenzi wako kwa huyo mwanamume mwingine hadi akakuacha na kuolewa naye. Inawezekana kuna mengi mabaya kumhusu mwanamume huyo ambayo amegundua na ndiyo maana amemuacha na kurudi kwako. Iwapo bado unampenda, msamehe na kumpa nafasi nyingine katika moyo wako. Bila shaka amejifunza na ameamua kutulia kwako.

 

Nimetafuta wa kunifaa sijapata, sasa shangazi, vipi tukirushana roho?

Shangazi pokea salamu zangu za dhati na mapenzi tele kwako. Pongezi kwa kazi yako nzuri katika ukumbi huu. Kusema kweli, nimevutiwa sana na ujuzi wako kuhusu masuala ya mapenzi na ndoa. Tafadhali nisamehe ukihisi nimekukosea. Nimetafuta kwa muda mrefu mwanamke wa kurusha roho naye lakini kufikia sasa sijapata. Waonaje ukawa ndio wewe? Tafadhali nijibu.

Kupitia SMS

Nashukuru kwa pongezi zako nyingi kuhusu kazi yangu. Hata hivyo, kama ulipanga kuzitumia kama chambo, basi umeambulia patupu. Kando na mimi, sidhani kuna mwanamke mwenye akili zake timamu anayeweza kuingia katika mtego kama huo. Pili, mimi nishapata wangu ambaye ananitosha na sina nafasi ya mwingine. Endelea kutafuta.