Shangazi Akujibu

Ameninyima asali, anasema hataki kuharibu usichana wake

August 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Shikamoo shangazi. Nina miaka 26. Nimependana na msichana fulani kwa mwaka mmoja. Nina hamu ya kuonja asali lakini amekataa akisema hataki kuharibu usichana wake. Nifanye nini?

Kama kweli unampenda msichana huyo, muelewe na uheshimu kauli yake la sivyo utamkosa. Hatima ya mapenzi ya dhati ni ndoa. Ukisubiri hadi wakati huo atakuwa mke wako na utakuwa na uhuru wa kufurahia asali bila vikwazo.

Niliugua hakuja hossy, huyu anipenda kweli?

Mwaka uliopita niliugua na nikalazwa hospitalini kwa miezi kadhaa. Mpenzi wangu hakunitembelea hata siku moja. Ameanza kunipigia simu tu baada ya kujua nimepona. Ananipenda kweli?

Mpenzi wako alikosea kwa kutoweka wakati ambao ulimhitaji zaidi. Hata hivyo, ni wazi kuwa hujamtoa kabisa katika maisha yako. Hakuna kosa lisiloweza kusamehewa. Kama amekuhakikishia bado anakupenda, msamehe mwendelee na uhusiano wenu.

Nampenda ilhali yeye naye hanipendi hata!

Nina mke na nampenda sana. Lakini nimechunguza na kugundua kwamba yeye hanipendi. Sitaki kuendelea kuishi katika ndoa isiyo na mapenzi. Nishauri.

Sijui ni mambo gani umeona ili kuamua kuwa mke wako hakupendi. Ninaamini ulimuoa kutokana na kuridhika na mapenzi yake. Kama kweli hakupendi, maisha yenu yatakuwa magumu. Shauriana naye mtafute suluhisho.

Nimegundua kumbe ana mke mwingine ushago

Nimeolewa na tuna watoto wawili. Nimegundua mume wangu ana mke mwingine mashambani. Ameungama na kuomba msamaha huku akitaka niwe mkewe wa pili. Tafadhali nishauri.

Maisha ya ndoa ni ushirika muhimu na mtu anahitajika kumchunguza na kumfahamu vyema mwenzake kabla ya kuchukua hatua hiyo. Ungefanya hivyo ungeepuka hali hiyo. Sasa itabidi ukubali kuwa mke wa pili ama umuache.