Demu amekuwa akikutana na Ex eti ni kahawa tu ilhali tunapanga harusi!

NINA mpenzi na tumeanza mipango ya harusi. Kinachonishangaza ni kwamba amekuwa akikutana na mpenzi wake wa zamani na nikimuuliza anasema waliachana lakini bado ni marafiki. Ananichezea?
Si hali ya kawaida kwa wapenzi kuachana kisha kuendelea kuonana eti ni marafiki. Mara nyingi huwa wamekosana na hali hiyo huleta uadui kati yao. Nahisi kuna kitu kinaendelea kati yao. Mwambie mpenzi wako avunje uhusiano huo kwanza.
Mume hataki kuja kwetu kuomba msamaha ilhali ni yeye alikosea
Ni miezi miwili sasa tangu niache mume wangu na kurudi kwetu baada ya kunikosea. Amekuwa akinishawishi nirudi lakini wazazi wanasema ni lazima aje nyumbani wazungumze. Amekataa wito huo. Nifanye nini?
Wazazi wako wanataka kusuluhisha tofauti kati yenu na kuzuia hali hiyo kutokea siku za baadaye. Ni ujeuri kwa mume wako kukataa wito huo na ni ishara kwamba hana haja nawe wala ndoa yenu.
Kuna uvumi mtaani kwamba mwanamke fulani amekuwa akimtembelea
Nampenda sana mpenzi wangu lakini nahisi yeye ananihadaa. Rafiki yangu ni jirani yake mtaani na ameniambia kuna mwanamke amekuwa akimtembelea. Ninaamini hiyo ndiyo sababu hajawahi kunionyesha kwake. Nifanyeje?
Kama mpenzi wako amekukataza kumtembelea basi una sababu ya kumshuku. Mwambie rafiki yako achunguze hadi siku ambayo atamuona mwanamke huyo kisha akufahamishe uende uthibitishe.
Bado ndo tunajuana na tayari ameanza kuniomba pesa
Kuna mwanamke ambaye amenasa moyo wangu na kuna matumaini kwamba tunaweza kuwa wapenzi. Lakini ameanza kuniomba pesa. Ningependa kumsaidia ila nahisi ni mapema.
Hizo si dalili nzuri kutoka kwa mtu ambaye mmejuana kwa muda mfupi tu, hata bado hajawa mpenzi wako. Ukianza kumpa pesa, hutaweza kujua iwapo anakupenda kwa dhati ama nia yake ni pesa. Itabidi umpime ili ujue nia yake.