Shangazi Akujibu

Mimi ni mkonda sana, hata mabinti hawanitamani

Na PAULINE ONGAJI January 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Shangazi,

TANGU utotoni nimekuwa mvulana mwembamba mwenye kifua kidogo. Ninahisi hiyo ni mojawapo ya sababu ambazo zimenifanya kutokuwa kivutio cha mabinti. Sasa nataka kifua kipana, nifanyeje?

Kwanza kabisa unaweza kupanua kifua kupitia mazoezi. Lakini pia kumbuka kuwa huenda haya ni maumbile yako na itakuwa muhimu na vyema zaidi kujikubali jinsi ulivyo.

Huyu kaka ni muongo ajabu, iko shida!

Kwa miezi kadhaa sasa nimekuwa katika uhusiano na kalameni fulani. Ni mtanashati na amejaliwa kila sifa za kutamanisha na ninampenda sana. Lakini jamaa ni muongo sana na nimeshindwa kabisa kumuamini. Nifanyeje?

Ikiwa una ushahidi wa kutosha kwamba ni muongo na juhudi zako za kujaribu kuzungumza naye ajirekebishe hazijafua dafu, una kila haki ya kumuacha.

Nimemzimia kinoma ila demu hana haja nami

Nimekuwa nikimtamani binti mmoja ambaye tunaenda kanisa moja. Hata hivyo, licha ya jitihada zangu za kunasa jicho lake ili nipate fursa ya kumfungulia moyo ni kama hanitaki kabisa. Nitamnasaje?

Penzi halilazimishwi. Usipoteze muda kwa mtu asiyekuwa na haja nawe.

Naelekea kugonga 50 na bado ni kapera

Mimi ni mwanamume anayekaribia miaka 50. Nimekuwa katika mahusiano kadhaa ambayo hayajafanikiwa. Sasa nahofia kwamba huenda nisipate mke. Nipe ujanja Shangazi!

Suala la uhusiano na ndoa sio la kuharakishwa. Kila mtu ana wakati wake. Kuwa na subira na wakati ufaao utakapotimia utakutana na anayekufaa.