Shangazi Akujibu

NIPE USHAURI: Kalamu ya mpenzi wangu ni fupi na haiandiki vizuri, nimechoka

May 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Vipi shangazi. Kalamu ya mpenzi wangu haiandiki ipasavyo. Ni fupi na haijanolewa. Kamwe kabisa hanitoshelezi. Japo wazazi wake wananibembeleza niendelee kukaa naye, napanga kumwacha. Nipe ushauri.

Urefu au ufupi wa kalamu sio hoja. Kumbuka kuna wale walio na kalamu ndefu ila hawajui kuitumia ipasavyo. Hata hivyo, kuna haja mtafute ushauri kutoka kwa mtaalamu. Hata hivyo, ikiwa unahisi huridhiki, unaweza kufanya maamuzi yanayowiana na furaha na ustawi wako wa muda mrefu.

Anataka kunioa lakini ana watoto 2 tayari, nifanyeje?

Vipi shangazi. Kuna huyu mwanaume ninayempenda lakini ana watoto wawili kutoka uhusiano wake wa zamani. Anasisitiza kuwa nitakuwa mama wa watoto wake lakini sina hakika kama nipo tayari kwa jukumu hilo. Naomba ushauri.

Kuoa au kuolewa na mtu aliye na watoto ni uamuzi mkubwa unaofaa kuangaziwa kwa umakinifu. Zungumza naye kuhusu matarajio na majukumu ya pamoja. Ikiwa huna uhakika, chukua muda kufikiria kabla ya kufanya uamuzi.

Mume wangu hayuko tayari kwa ndoa yenye watoto

Shikamoo shangazi. Nimekuwa kwenye ndoa kwa miaka mitano lakini mume wangu hataki tuanze familia. Kila nikimwongelesha anadai bado hatuko tayari. Ninataka kuwa mama lakini sijui nitafanye nini. Nisaidie.

Kuanzisha familia ni uamuzi wa pamoja. Na ikiwa mmoja wenu hayuko tayari, basi itakuwa vigumu sana ndoa hiyo kustawi. Ikishindikana, mtafute ushauri kutoka kwa mtaalamu wa masuala ya ndoa.

Tofauti yetu ya dini imekuwa kizuizi kikuu kwetu kuoana

Kwako shangazi. Kuna huyu mwanadada tunapendana sana lakini dini zetu zinatofautiana. Familia yangu haikubali kabisa tufunge ndoa. Nimejaribu kuwaeleza lakini wameshikilia msimamo wao. Nifanye nini?

Masuala ya dini yanahitaji mawasiliano ya kina. Zungumza na familia yako kwa heshima na uwahakikishie kwamba uamuzi wako ni wa upendo na ya kuheshimu imani za kila mtu.