Shangazi Akujibu

Shangazi, nataka dume la ushago hawa wa mjini hatuwezani

Na PAULINE ONGAJI February 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NIKO na miaka 30. Natamani kuolewa ila sitaki wanaume wa mjini kwani tabia zao ni za kutisha. Nisaidie kusaka mume kutoka mashambani.

Itakuwa makosa kwako kutumia kigezo hicho kumtafuta mume. Usikimbilie uhusiano, ukikutana na mtu unayempenda chukua muda wako kumjua vyema awe wa mjini au mashambani. 

Anatisha kufichulia mpenzi wangu kwamba tulikula uroda, japo nilikuwa mlevi

Nimekuwa katika uchumba na mpenzi wangu kwa miaka minne na tunapanga kufunga ndoa karibuni. Hata hivyo, wiki kadhaa zilizopita nilisafiri kwa ziara ya kazi. Usiku mmoja baada ya kuburudika kwa mvinyo tulishiriki ngono na jamaa tunayefanya kazi naye. Sasa ananilazimisha tuwe na uhusiano la sivyo amwambie mchumba wangu.

Hiyo ndiyo hatari ya kula uroda pembeni ilhali uko katika ndoa au uchumba. Suluhisho ni kumweleza ukweli mpenzi wako na kumwomba msamaha.

Mke amebania mshahara wake hataki kununua chochote nyumbani ilhali pesa zimeniishia

Nimeoana na mke wangu kwa miaka 10 na nimekuwa nikikidhi mahitaji yote ya familia. Katika siku za hivi majuzi tumekumbwa na matatizo ya kifedha kutokana na pandashuka kazini mwangu. Licha ya mke kufanya kazi hataki kuchangia gharama za matumizi nyumbani, kiasi kwamba siku hizi anaficha mshahara wake.

Ndoa na uhusiano haipaswi kuwa na siri hata katika masuala ya kifedha. Zungumza na mkeo kwa upole kuhusu wasiwasi wako. Nina uhakika kwamba ikiwa anaheshimu uhusiano wenu na anakupenda atakusikia.

Ana tabia ya kuniaibisha mbele ya marafiki na jamaa zetu

Mume wangu ana mazoea ya kuniaibisha kwa jamaa na marafiki zetu hususan kuhusu mapishi na miereka ya chumbani. Nimwambie vipi kwamba ananikosea?

Mwambie waziwazi mkiwa peke yenu jinsi tabia yake inakukera na usisitize kuwepo mipaka.