Shangazi, wanaume wa watu kwa ploti ni mafisi tu, nihame?
Nilihamia ploti fulani miezi kadhaa iliyopita. Napenda mahali hapa lakini waume wa watu wananimezea mate. Nifanyeje?
Hiyo ni balaa! Umekiri hao ni waume wa watu, hivyo uwezekano ni mkubwa kwamba wanachotaka ni burudani tu. Unahatarisha maisha, usalama na afya yako kwa kutaka kujihusisha na mabwana wa wengine. Hama haraka upesi kutoka kwa hiyo ploti.
Ex bado hajapata mtu nawazia kumfaa kimahaba ili akate kiu
Miaka michache iliyopita nilipendana na kaka fulani tukajaliwa mtoto. Lakini uhusiano haukudumu na tukaachana. Mimi sasa nishaolewa lakini yeye bado hajafanikiwa. Nimeguswa moyo ili nimsaidie kukata kiu ya mapenzi. Kuna ubaya?
Sana! Wewe ni mke wa mtu na ukijaribu kufanya hivyo utavunja ndoa yako. Cha muhimu ni umpe nafasi ahusike katika maisha ya mwanawe, pasipo kuingiza uroda kati yenu kwani unahatarisha ndoa yako.
Sponsa anataka nimzalishe msichana pekee
Kwa miezi kadhaa nimekuwa katika uhusiano na mke wa mtu na hafichi. Mumewe amemzalisha watoto wa kiume pekee na sasa anataka nimtungishe mimba ya mtoto msichana.
Huyo ni mke wa mtu unacheza na moto. Una uhakika upi kuwa utamzalisha mtoto wa kike? Hakuna mtu aliye na uwezo wa kuamua jinsia ya mtoto atakayejaliwa.
Nimesikia familia ya demu wangu wanamtafutia mume aliye na pesa!
Nimeishi na binti fulani kwa miaka miwili sasa na bado hatuna mtoto. Aidha, bado hatujarasimisha uhusiano wetu lakini tunapanga kufanya hivyo karibuni. Majuzi niligundua wakwe zangu watarajiwa wanamtafutia mume aliye na pesa.
Una ushahidi upi? Zungumza na demu wako na ikiwa anakupenda hawezi kuruhusu jambo kama hilo kufanyika. Endeni mkawaone wazazi mkiwa pamoja na muwaeleze mipango yenu ya kufunga ndoa rasmi.