Tangu nimuonjeshe asali hisia zangu kwake zimeisha kabisa
Kwako shangazi. Mpenzi wangu amekuwa akitaka kuonja asali lakini nilitaka tungoje hadi tujuane vizuri. Juzi alinishawishi hadi nikakubali. Tangu siku hiyo hisia zangu kwake zimetoweka. Nifanye nini?
Ni wazi kwamba huna mapenzi ya dhati kwa mwanamume huyo. Unasema ulikubali ombi lake kutokana na ushawishi wake, si kwa hiari yako. Sasa umejua humpendi, tafuta namna ya kumaliza uhusiano huo.
Mchumba ninayetaka kuoa amehamia mbali kikazi
Kwako shangazi. Mpenzi wangu amehamishwa kikazi. Imekuwa vigumu kwetu kuonana ilhali sijazoea. Tumeanza mipango ya ndoa na nahofia maisha yatakuwa magumu hata zaidi tukioana. Naomba ushauri wako.
Mpenzi wako hawezi kuacha kazi kwa ajili ya mapenzi yenu. Jambo la kufanya kwa sasa ni kuvumilia tu bora kila mmoja anamwamini mwenzake. Lakini ni muhimu mfanye mipango ya kuishi pamoja baada ya ndoa.
Dada jirani ameuteka moyo wangu ila nachukia ulevi wake
Kwako shangazi. Mwanamke jirani yangu ameteka moyo wangu kimapenzi. Kuna kila dalili kuwa yeye pia ananipenda. Lakini nimegundua anapenda pombe na sidhani naweza kuishi na mke mlevi. Waonaje?
Uamuzi ni wako. Kama huwezi kuishi na mke anayekunywa pombe, huyo hatakufaa, labda akubali kuacha. Mnaweza kupendana kisha ujaribu kumshawishi aache. Mtu anaweza kufanya chochote kwa ajili ya mapenzi.
Mpenzi wangu amekataa kunioa eti sababu nina mtoto
Kwako shangazi. Mpenzi ameniambia hawezi kunioa eti kwa sababu nina mtoto. Tumekuwa pamoja kwa miaka mitatu na nilimwambia siku ya kwanza tulipokutana na akaniambia hiyo si hoja. Nifanye nini?
Mwanamume huyo ilitaka tu kukutumia na ametimiza nia yake. Siku hizi wanaume wengi hawapendi kuoa wanawake walio na watoto. Hatua yake hiyo isikuvunje moyo. Weka matumaini kuwa hatimaye utapata mume.