Shangazi Akujibu

Wanataka nisomee ualimu nami nataka kuwa DJ; nishauri

August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Nilikosa alama za kujiunga na chuo kikuu. Familia yangu inanilazimisha nijiunge na chuo cha kiufundi nisome ualimu lakini mimi nataka kuwa DJ.

Naomba ushauri?

Ni jukumu la mzazi kukushauri ila ikiwa kipaji chako kiko kwenye muziki, tafuta njia ya kuonyesha kuwa unaweza kuwa DJ mwenye nidhamu na mafanikio.

Jaribu kupata mafunzo rasmi au hata kozi ili uridhishe familia na moyo wako.

Tunajuana mtandaoni na tayari ataka tuoane!

Nilikutana na mwanamume mtandaoni na tukapendana sana. Hatujawahi kukutana ana kwa ana. Sasa anataka tufunge ndoa. Ni sawa kumuamini?

Mapenzi ya mtandaoni yamejaa vizingiti. Kumjua mtu kwa ujumbe si sawa na kumjua ana kwa ana. Kabla ya kufikiria ndoa, jitahidi mkutane, ujue familia yake, marafiki zake, na maisha yake halisi.

Usikimbilie harusi kwa sababu ya emojis.

Kazi nje ya nchi au ndoa?

Ninapewa nafasi ya kuenda kufanya kazi nje ya nchi miaka mitano, lakini mchumba wangu hataki niende. Je, ndoto zangu ni muhimu kuliko ndoa?

Ndoto zako ni sehemu yako. Kama mchumba wako anakupenda kwa kweli, atakuvumilia na kukusubiri.

Usikubali kufunga ndoto zako kwa sababu ya hofu ya kumkosa mtu.

Ni sawa kuishi kwa mavyaa?

Hujambo shangazi. Nimeolewa lakini bado tunaishi na mama mkwe kwa sababu mume wangu hana uwezo wa kulipa kodi ya nyumba.

Je, ni aibu kuishi kwa wazazi baada ya ndoa?

Si aibu kuishi kwa mama mkwe ikiwa ni hali ya muda mfupi na kutokana na sababu halali kama ukosefu wa pesa.

Aibu huwa pale mume anakosa mipango ya kujitegemea na kutegemea mamake.