Makala

Sherehe kambi ya Ruto, viongozi wa majenzii wakilimana

Na LABAAN SHABAAN September 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MTETEZI wa haki za kibinadamu Mercy Tarus amemshambulia mwanaharakati mwenzake Morara Kebaso katika msururu wa shutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Tuhumu kali ziliibuka kati ya viongozi hawa wa vijana wa kizazi cha jenzii ambao katika kipindi kirefu cha siku ya Jumatano walirushiana cheche.

Aliyewasha moto huu ni Bi Tarus ambaye alimtuhumu Bw Kebaso kuwa mjanja na hakuwa na nia njema kuhusu suala la maendeleo ya vijana wa Gen Z.

Tarus alisema ameshiriki mikutano na kikundi kinachoongozwa na Kebaso awali.

Kulingana naye, Kebaso haelewi kabisa mustakabali wa vuguvugu la Gen Z.

Kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, Tarus amesema Kebaso hana mipango yake maalum akimtuhumu kwa kuiba mawazo ya mavuguvugu mengine.

Katika msururu wa kampeni za kuhamasisha umma, Bw Kebaso amekuwa akitumia kaulimbiu ya Kenya ni Home (Kenya ni Nyumbani), tukio ambalo limemchemsha Bi Tarus.

“Wanajitokeza na kuongea kwa ujasiri lakini kwenye mikutano hawawezi kujibu maswali mepesi kama vile chanzo chao cha mapato na kadhalika,” aliandika Tarus.

“Wanazunguka kusaka mawazo kwa jina la kukutana na wanamapinduzi wenzao na ghafla wanazichukua na kuyatekeleza ili yaonekane ni yao.  Huwezi kuendelea kuja kwangu kuomba ushauri na kumbe unajifanya umejitolea kushiriki uanaharakati na baadaye unatumia jina la mpango wangu (Kenya ni Home).”

Bi Tarus ameashiria kuwa Bw Kebasa amefadhiliwa na watu wenye nia mbaya kuvuruga vuguvugu la jenzii.

Anasema kuwa ‘Wakili huyu wa Jenzii’ ameanza kutelekeza masuala muhimu yanayoendana na matakwa ya vijana.

“Shughuli zake zimehama kutoka kwa uhamasisho wa kijamii na kuwa mikutano ya kisiasa. Anatumia vuguvugu la vijana kujinufaisha na haonekani tofauti na wanasiasa wanaopingwa na vijana,” aliendelea.

Bi Tarus alifafanua kuwa hana tatizo na wito wa Kebaso wa uwajibikaji na utawala bora. Hata hivyo, anamtaka kutoingiza jina lake kwenye kampeni zake.

“Ninajua mambo haya zaidi yako na ndiyo sababu unakuja kwangu. Nimekuwa nikikuambia unahitaji mpango wa kufanikisha mambo,” alisema Tarus.

“Katika mipango yako isiyoeleweka usitaje jina langu na kutumia kaulimbiu yangu. Kuwa mbunifu. Unatumia mifumo ambayo imewekwa bila kuunda mfumo wako ili tulaumiwe pamoja?”

Kebaso alipata umaarufu kupitia video anazorekodi na kurusha mitandaoni akikashifu utepetevu katika serikali ya Rais William Ruto.

Kujibu shutuma za Bi Tarus, Bw Morara alisema hakuna anayeweza kumiliki vuguvugu na badala yake wanaweza kuwa katika kundi hilo.

“Naomba kila mmoja achapishe nembo ya Kenya ni Home na kuangika kutani. Turekodi video za ‘Vampira Diaries Videos’ kuonyesha kilichoibwa vijijini na mijini kupitia ufisadi na miradi iliyokufa. Lengo ni kuchangamsha watu wafanye wanachoweza kufanya,” aliandika Morara kwenye akaunti yake ya mtandao wa X.