Sheria: Hauwezi kukubaliana na mume au mkeo kutalikiana kienyeji hapa Kenya
Katika miaka ya hivi karibuni, Kenya imekuwa na mazungumzo yanayoongezeka kuhusu mageuzi ya sheria za talaka ili kuruhusu talaka kwa makubaliano ya pande zote mbili ilivyo katika mataifa mengine kuboresha sheria za kifamilia.
Hata hivyo, mnamo Aprili 24, 2025, Mahakama Kuu ya Kenya jijini Nairobi ilitoa uamuzi katika Kesi ya Katiba E075 ya 2022, ikisisitiza kwamba talaka kwa makubaliano bado haijatambuliwa kisheria nchini Kenya, na hivyo kuimarisha mfumo wa sasa wa talaka unaotegemea kosa.
Katika kesi ya Coppler Attorneys & Consultancy dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Bunge la Kitaifa, mlalamishi alipinga sehemu ya X ya Sheria ya Ndoa, 2014, akidai kwamba inalazimisha wanandoa wanaotaka kuachana kupitia mchakato wa kisheria unaohusisha kulaumiana. Walisema kuwa mfumo huu unasababisha uhasama, unaharibu malezi ya watoto, na kuathiri heshima ya familia.
Mlalamishi aliomba Mahakama iamue kwambaSehemu ya X ya Sheria ya Ndoa ni kinyume cha Katiba, kwamba wanandoa waruhusiwe kuvunja ndoa kwa makubaliano ya pande zote, na kwamba Bunge ilazimishwe kurekebisha sheria hiyo.
Lakini Mahakama Kuu ilitupilia mbali ombi hilo, na kutoa maamuzi muhimu kadhaa ikiwemo kusisitiza kuwa ndoa ni taasisi ya kijamii inayopaswa kulindwa. Mahakama ilisisitiza kuwa ndoa si makubaliano ya kibinafsi pekee bali ni msingi wa jamii ya Kenya unaolindwa chini ya Kifungu cha 45 cha Katiba.
Sheria inalenga kuzuia ndoa kuvunjika kirahisi kwa kuhakikisha kuwa kabla ya talaka, kuna nafasi ya ushauri, upatanisho na usuluhishi. Talaka kwa makubaliano ingeondoa nafasi hiyo ya jamii kulinda ndoa kama taasisi muhimu ya kijamii. Kulingana na mahakama, mfumo wa talaka kwa kosa bado unatumika
Sheria ya Ndoa, 2014 inaruhusu talaka kwa misingi ya uzinzi, ukatili, kuachwa, au kuvunjika kabisa kwa ndoa. Hata hivyo, lazima ushahidi wa hali hizo utolewe na makubaliano pekee hayatoshi.
Mahakama ilisema kuwa makubaliano ya pande mbili pekee si sababu halali ya kuvunja ndoa. Kutokuwepo kwa kipengele hicho katika sheria hakukiuki Katiba bali kunalinda thamani ya kijamii iliyowekwa kwenye ndoa.
Mahakama ilikumbusha kuwa haiwezi kulazimisha Bunge kutunga sheria kwa namna fulani, kwani jukumu la kutunga sheria liko chini ya Kifungu cha 94(1) cha Katiba.
Mahakama ilisema kuwa ingawa mtu ana haki ya kuondoka kwenye ndoa, maslahi ya kulinda taasisi ya familia yanapewa kipaumbele zaidi ya matakwa binafsi ya kupata “njia rahisi” ya kuachana.
Uamuzi huu ulitolewa wakati ambapo Mswada wa Sheria ya Ndoa (Marekebisho), 2023 ulikuwa umependekeza kuruhusu wanandoa kuachana kwa makubaliano bila kulazimika kuthibitisha kosa.
Kwa mujibu wa mswada huo wanandoa wangeweza kuwasilisha ombi la pamoja la kuvunja ndoa na mahakama ingetoa amri ya talaka ikiwa makubaliano ya mali na malezi ya watoto yamefikiwa.
Hata hivyo, mjadala wa mswada huo uliahirishwa, na mfumo wa sasa wa talaka kwa msingi wa kosa unaendelea kutumika.