Afya na JamiiMakala

Sheria za Tanzania zinavyochangia kutoweka kwa ndovu wa Kenya

Na PAULINE ONGAJI September 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 5

KATIKA kipindi cha miaka mitatu tu huenda Kenya ikapoteza ndovu wake maalum wenye pembe kubwa zaidi, al-maarufu Super Tuskers.

Janga hili limechangiwa na ongezeko la visa vya uwindaji ndovu kwa pembe zao, kwenye mpaka wa Kaskazini mwa nchi ya Tanzania, na mbuga ya wanyama ya Amboseli hapa nchini.

Takwimu za wahifadhi ndovu zinaonyesha kwamba katika kipindi cha miezi minane iliyopita, ndovu watano wanaojumuisha idadi ya ndovu wanaopatikana kwenye mpaka wa mbuga ya wanyama ya Amboseli na Kilimanjaro Magharibi, wamepigwa risasi na kuuawa na wawindaji, wanapovuka mpaka kutoka Kenya kuelekea nchini Tanzania.

Kulingana na watafiti na wahifadhi ndovu, mwisho wa mwaka wa 2023, ndovu wawili wakomavu wa kiume kutoka Kenya, kila mmoja akiwa na pembe ya zaidi ya kilo 45, waliuawa nchini Tanzania—hatua ambayo inakiuka marufuku ya miaka 30- dhidi ya uwindaji ndovu.

Hii ilifuatiwa na upigwaji risasi wa ndovu wa tatu wa Kenya mwezi Februari 2024.

Mbali na sheria za Tanzania zinazoruhurusu uwindaji ndovu, ongezeko la visa vya kuuawa kwa wanyama hawa limehusishwa na hatua ya nchi hii kutoa vibali vipya vya kuwawinda ndovu katika maeneo ya kaskani mwa nchi hiyo, yanayopakana na mbuga ya wanyama ya Amboseli, nchini Kenya.

Nchini Kenya, uwindaji ndovu umepigwa marufuku tokea mwaka wa 1973. Chini ya Sheria ya Wanyamapori ya Kenya ya 2013 (WCMA 2013), kujihusisha na uwindaji ndovu unachukuliwa kuwa hatia ambayo inaadhibiwa na faini isiyopungua Sh20 milioni, kifungo cha maisha au vyote, hasa kwa vifaru weusi na weupe, vile vile ndovu.

Kwa upande mwingine, sheria  ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya 2019 ya Tanzania, imepiga marufuku uwindaji wa ndovu walio na pembe chini ya kilo 20 zenye urefu wa chini ya sentimeta 160.

Mbali na kuwacha mwanya kwa wawindaji kuua baadhi ya wanyama hawa, kwa upande mwingine pia, sheria ya Tanzania inawaruhusu wawindaji ndovu kuwaua wanyama hawa, kupitia vibali vinavyotolewa na Halmashauri ya Wanyamapori ya Tanzania (TAWA) kwa kampuni za kuwinda wanyama.

Kwa kawaida, msimu wa uwindaji huwa kati ya Julai 1 na Desemba 31, ambapo orodha hutolewa ya wanyama wanaokubaliwa kuwindwa, na ndovu ni mojawapo ya spishi zinazolengwa.

Mojawapo ya kampuni ambazo zimekuwa zikihushwa na shughuli hii ni Kilombero North Safaris, inayomilikiwa na mfanyabiashara, Bw Akram Aziz.

Japo usimamizi na uhifadhi wa ndovu nchini Tanzania unatambuliwa kama jukumu la utawala wa serikali ya nchi hiyo,  ndovu wamekuwa wakiishi mpakani kati ya Kenya na Tanzania, na hivyo usalama wa wanyama hawa, kwa miaka, umekuwa ukiambatana na makubaliano baina ya nchi hizi mbili.

Makubaliano haya yalifikiwa mwaka wa 1994 baada ya kisa kilichostaajabisha ulimwengu ambapo wawindaji nchini Tanzania waliwaua ndovu wanne (RBG, Sleepy, Saibulu, and Oloitipitip), karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania. Kutokana na kisa hicho, mwaka wa 1995, marufuku dhidi ya uwindaji ndovu yalifikiwa baina ya nchi hizi mbili.

Hata hivyo, makubaliano hayo yalivunjiliwa mbali mwaka wa 2022 kampuni ya Kilombero North Safaris, iliposhinda ridhaa ya Ngasurai, na uwindaji wa ndovu ukaanza mwaka wa 2023.

Tuliwasiliana na Bw Aziz, mumliki wa kampuni ya Kilombero Safaris kupitia barua pepe, ili kutaka kupata maoni yake kuhusu jinsi shughuli za kampuni yake zinavyoendelea kuathiri idadi ya ndovu nchini Kenya.

Lakini kulingana na Bw Aziz, uwindaji unaotekelezwa na kampuni yake ni wa manufaa kwa idadi ya ndovu. Aidha, anapinga vikali kwamba ndovu wanaowindwa nchini Tanzania ni sawa na wale wanaotoka Kenya.

“Hakuna utafiti wa kisayansi unaothibitisha madai kwamba ndovu wanaowindwa Tanzania ni sawa na wale waliotoka Kenya,”alisema.

Lakini kulingana na sayansi, mambo ni tofauti. Dkt Paula Kahumbu, mtafiti wa ndovu na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la uhifadhi wa ndovu la WildlifeDirect, asema, kuna ushahidi kwamba ndovu wanaopatikana eneo la Magharibi wa Kilimanjaro Tanzania ni wale wanaopatikana katika mbuga ya wanyama wa Amboseli.

“Tunajua hivi kwa sababu hawa ni ndovu ambao wametafitiwa sana ulimwenguni – miaka – 51 years.  Wanatambulika kutokana na sifa zao za kipekee na wao hupigwa picha sana, kumaanisha kwamba wanaweza kutambuliwa kwa urahisi na wataalam,”aeleza.

Kulingana na Cynthia Moss, mtafiti katika shirika la Amboseli Trust for Elephants, mfano mzuri ni Gilgil, ndovu maarufu wa kiume aliyewindwa na kupigwa risasi katika upande wa Tanzania wa eneo hili.

Mwezi Machi mwaka huu, Bi Moss pamoja na mtafiti mwenzake Bi Norah Njiraini, walimtambua ndovu Gilgil baada ya kupokea picha kutoka kwa mzoga wa ndovu wa kiume aliyeuawa katika eneo la Enduimet, nchini Tanzania, kabla ya kuchomwa. Walimtambua ndovu huyu baada ya kulinganisha picha hii na ya awali ya mzoga tofauti.

Aidha, kulingana na watafiti, ngozi ya ndovu ni sawa na alama ya kidole, kwani kwa kawaida ina mikunjo, violezo vya mishipa ya damu, mafumba, na uvimbe, sifa zinazoweza kutofautisha  kila ndovu.

Utafiti mwingine wa wanasayansi katika shirika la Amboseli Trust for Elephants (ATE) unaonyesha kwamba kila ndovu anatambulika kibinafsi na ana nambari au jina maalum, pamoja na picha zinazohifadhiwa.

Pia, kuna kanzidata ya kina inayojumuisha kila ndovu aliyetambuliwa katika kipindi cha miongo mitano, na huhusisha taarifa kama vile kuzaliwa, vifo na nambari za zaidi ya ndovu 4,000.

“Sasa wanajaribu kuficha ushahidi kwa kuwachoma na tunachopata ni makaburi na jivu, ambapo inakuwa ngumu kwetu kuwatambua ndovu husika,”aeleza Dkt Kahumbu.

Idadi kubwa ya ndovu katika mbuga ya wanyamapori ya Amboseli  ni wale wanaopatikana kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania.

Kulingana na utafiti wa mashirika ya uhifadhi wa ndovu ya Elephant Voices, Big Life Foundation na Amboseli Trust for Elephants, mfumo ikolojia huu, unajumuisha mbuga ya wanyama ya Amboseli na zingine zinazozingira hifadhi zingine nchini Kenya, eneo linaosimamiwa na hifadhi ya wanyamapori  ya Enduimet nchini Tanzania.

Kwa sasa kuna familia 65 za ndovu zinazojumuisha takriban  ndovu 2,000 kwenye mfumo huu. Familia 17 ambazo zinajumuisha ndovu 365, huvuka na kuingia nchini Tanzania kila wakati.

Idadi ya ndovu katika mbuga ya Amboseli inajumuisha baadhi ya ndovu wa kiume wenye pembe kubwa zaidi barani Afrika, sifa inayotokana na muundo jeni maalum.

Pembe wake wa kipekee hata wamefanyiwa maonyesho katika taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na makavazi ya Uingereza.
Lakini sasa kulingana na wahifadhi, ni ndovu kumi pekee walio na pembe zenye uzito wa tariban kilo 45 waliosalia nchini Kenya, na wengi wao wanapatikana kwenye mbuga ya wanyama ya Amboseli.

Kwa mujibu wa wanasayansi, huchukua takriban miaka 35 kwa ndovu wa kiume kutimu umri wa kuweza kuzalisha kila mwaka.
Ndama wengi wanaozaliwa huwa kupitia hawa ndovu wakomavu wa kiume wanaosakwa na wawindaji,” aeleza Dkt Joyce Poole, Mkurugenzi wa kisayansi katika shirika la ElephantVoices.

Kwa sasa wanasayansi wanahofia kwamba pindi wawindaji hawa watakapowaangamiza na kuwamaliza hawa ndovu wakubwa, sasa wataelekeza macho yao kwa wale wachanga.

“Ndovu wanaolengwa ni a kiume ambao wako katika umri wa kuzalisha, ambao wanahitajika kuendeleza kizazi,”aeleza Dkt Kahumbu.

Tulipowasiliana na huduma ya uhifadhi wanyapori (KWS), tulifahamishwa kwamba hawawezi angazia masuala ya sera yanayohusiana na taifa jirani kutokana na makubaliano ambayo huongoza mahusiano ya nchi mbili. Tulishauriwa kutafuta mwongozo zaidi kutoka wa Wizara ya Utalii na Wanyamapori.

Tulipowasilianana Bi Silvia Museiya, Katibu wa Kudumu katika Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Utalii na Wanyamapori, alisema ni kweli kwamba wizara hiyo imepokea malalamishi kuhusu ndovu wa Kenya na kwamba “wizara inakusanya takwimu kuhakikisha kwamba tunatoa taarifa sahihi hivi karibuni,”aliongeza.

Aidha, tuliwasiliana na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori ya Tanzania kupitia barua pepe ili kupata maoni yao kuhusu uhuisiano baina ya kutoweka kwa ndovu wa Kenya, na sheria za uwindaji wanyama hawa nchini Tanzania, lakini hatukupata majibu.

Kulingana na wahifadhi ndovu hapa nchini, Tanzania ina uwezo wa kusaidia juhudi za uhifadhi wa wanyama hawa nchini Kenya kwa kusitisha utoaji vibali vya kuwaua wanyama hawa.

Ndiposa mnamo Agosti 12, 2024,  katika siku ya maadhimisho ya Siku ya Ndovu duniani, wahifadhi ndovu hapa nchini Kenya waliwasilisha maombi  kwa Rais William Ruto na mwenzake kutoka Tanzania, Bi Samia Suluhu, kushirikiana ili kuwalinda ndovu.

[email protected]