Makala

SHINA LA AFYA: ‘Kwa miongo 3, selimundu umekuwa mwiba kwangu’

November 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 5

Na LEONARD ONYANGO

IWAPO atafanikiwa kumpata mke anayemjali na kumpenda jinsi alivyo, Brian Omondi Oyugi anasema kuwa huo utakuwa mwanzo mpya kwake.

Anasema kuwa anahitaji upendo zaidi ili apate hamu ya kutaka kuendelea kuishi.

“Kila ninapopata mpenzi, huniacha baada ya kubaini kuwa ninaishi na ugonjwa usiopona. Umri unazidi kusonga na ninatamani kuanzisha familia yangu. Vijana ambao nimewazidi umri kijijini kwetu katika Kaunti ya Homa Bay, wameoa. Kila mara ninapoenda nyumbani huwa wanashangaa kwa nini sijaoa ilhali ni ‘mzee’. Wananidharau hata nikiwapa ushauri ufaao hawanisikilizi kwa sababu wananiona kama ‘mtoto’ kwao,” anasema Brian.

Kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, Brian amekuwa akiishi maisha ya upweke. Kwake, hospitali imegeuka kuwa nyumbani.

Brian, 33, anaugua ugonjwa wa homa ya mifupa au selimundu (sickle cell).

Anasema kuwa unyanyapaa ni miongoni mwa changamoto kubwa ambazo amekuwa akikumbana nazo maishani.

Ugonjwa wa selimundu unatokana na dosari ya seli nyekundu za damu. Seli nyekundu hushindwa kusafirisha oksijeni mwilini hivyo kumfanya mwathiriwa kuhisi maumivu makali yasiyo na kifani.

Kwa kawaida seli nyekundu ambazo husafirisha oksijeni kupitia mishipa ya damu huwa na umbo la mduara au herufi ‘O’. Lakini kwa mgonjwa wa selimundu, seli nyekundu huwa na umbo la mwezi mwandamo (crescent) au herufi ‘C’.

Hizo seli zenye umbo la mwezi mwandamo zinaweza kukwama kwenye mishipa na kuzuia damu kuzunguka na kuisababisha kukosa kufikia baadhi ya viungo vya mwili.

Damu inapokwama, mgonjwa huhisi maumivu makali, haswa tumboni, kifuani na vifundo (joints) vya mwili. Mara nyingi mgonjwa hupata afueni baada ya kutibiwa hospitalini.

Ugonjwa huo hauna tiba lakini kuna dawa za kusaidia kupunguza maumivu na kuzuia damu kuganda mara kwa mara mwilini.

Wazazi wa Brian waligundua alikuwa na ugonjwa wa selimundu alipokuwa na umri wa miaka miwili.

Ugonjwa huo umekuwa mwiba kwake; ulimchelewesha kukamilisha elimu ya msingi na sekondari na miaka mitatu iliyopita ulimfanya kuacha kazi aliyokuwa akiifanya ya kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa wa virusi vya HIV.

“Nilipofika katika Kidato cha Pili, wazazi wangu walilazimika kunitoa katika shule ya upili ya Athi River, Kaunti ya Machakos, ambapo nilikuwa nikiishi kwenye bweni baada ya kulemewa na ugonjwa huu. Nilipelekwa hospitalini ambapo nilitibiwa kwa muda mrefu; nilikosa masomo kwa mihula miwili,” anaelezea.

Alipopata nafuu alihamishiwa katika shule Kahawa Garrison, Nairobi iliyo karibu na anapoishi pamoja na wazazi wake na kurudia Kidato cha Pili.

“Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, nilisomea stashahada na kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Moi ambapo nilisomea kozi ya Huduma kwa Jamii na kuhitimu 2015,” anaelezea.

Baada ya kuhitimu shahada (digrii) alisomea kozi fupi ya kutoa ushauri nasaha kwa waathiriwa wa virusi vya HIV na baadaye akaajiriwa.

“Lakini nililazimika kuacha kazi hiyo baada ya kulemewa na ugonjwa. Bosi alikerwa na mazoea yangu ya kuugua mara kwa mara. Nilipewa idadi ya watu ambao nilifaa kuwashauri lakini ilikuwa vigumu kufikia idadi hiyo kutokana na makali ya ugonjwa,” anaelezea.

Anasema kuwa wagonjwa wa selimundu wanapopata kidonda, huchukua muda mrefu kabla ya kupona kwa sababu kingamwili zao ni dhaifu.

Aidha damu inapoganda mwilini huhisi maumivu yasiyo kuwa na kifani. Kwa wanaume, damu inapoganda maumivu huwa makali zaidi kwani uume husimama bila kukoma – hali inayofahamika kama ‘Priapism’.

Brian anasema kuwa hali ya damu kuganda mwilini hutokea kwake kila baada ya miezi miwili.

“Hali hiyo inapotokea huwa ninakimbizwa hospitalini kudungwa sindano na nisipopata nafuu ninalazwa,” anasema.

“Damu inapoganda wakati mwingine mwathiriwa anazua fujo kama kichaa na hivyo madaktari wanalazimika kumdunga sindano ya usingizi kumpoza,” anaongezea.

Mara nyingi, hali hii hujitokeza kwa kushtukiza lakini Brian anasema kuwa huwa anaweza kutabiri kabla ya hilo kutokea.

“Nimeishi na ugonjwa huu kwa muda mrefu na ninaweza kutabiri wakati ambapo unajitokeza. Lakini kwa watoto huwa vigumu wazazi wao kutabiri hivyo ni rahisi kufariki,” anasema.

Kila anakokwenda, Brian hubeba begi lake dogo mgongoni. Ndani ya begi hilo kuna maji na dawa za kupunguza maumivu.

Dawa zilizomo ndani ya begi hilo ni tembe za Hydroxyurea, folic acid, Tranadol, Tramadol na Panadol.

Anaposafiri kwenda nyumbani kwao kijijini au maeneo mengineyo yaliyo na maambukizi ya juu ya malaria, anaongezea tembe ya Paludrine.

Hydroxyurea hupunguza uwezekano wa damu kuganda mwilini. Mgonjwa humeza tembe nne kila siku. Kila tembe huuzwa kwa kati ya Sh50.

Kwa siku, mgonjwa hutumia Sh200 au Sh6,000 kwa mwezi.

Tembe za folic acid husaidia kuongeza seli nyekundu za damu au kwa ufupi kuongeza damu mwilini.

“Kwa siku ninameza tembe moja ya folic acid; kila tembe inauzwa Sh5,” anasema.

Tramadol na Panadol hutumika kupunguza maumivu damu inapoganda.

“Tembe za Paludrine hutusaidia kujikinga na malaria ambayo ni hatari kwa waathiriwa na ugonjwa wa selimundu. Mgonjwa wa selimundu anapopatwa na malaria ni rahisi kufariki kwani ana kingamwili dhaifu,” anasema.

Tembe hizo za kuwalinda waathiriwa, hata hivyo, ni nadra katika maeneo mengi ya nchi.

“Dawa hizo hupatikana kwa wingi jijini Nairobi na miji mingine mikuu kama vile Mombasa, Kisumu na Nakuru. Ni vigumu kuzipata vijijini,” anasema.

Anasema kuwa madaktari na wauguzi katika hospitali nyingi nchini hawana mafunzo kuhusu namna ya kuhudumia waathiriwa wa selimundu.

Brian pia hubadilishiwa seli nyekundu za damu (red cell exchange) kila baada ya miezi mitatu; matibabu ambayo hugharimu Sh200, 000.

Matibabu hayo ya kubadilisha seli nyekundu humwezesha kukaa kwa angalau miezi mitatu bila kupatwa na tatizo la damu kukwama mwilini. Hiyo inamaanisha kuwa anahitaji angalau Sh800, 000 kwa mwaka za matibabu ya aina hii ambayo hupatikana katika hospitali kuu za kibinafsi kama vile MP Shah, jijini Nairobi.

“Nimekuwa nikipata msaada wa fedha kutoka kwa familia, wasamaria wema, marafiki na kanisa. Ninaomba sana nipate ajira ambayo itaniwezesha kujilipia mwenyewe gharama ya matibabu; sitaki kuwa mzigo kwa watu,” anasema huku akionekana kulengwalengwa na machozi.

Anapendekeza kuwa watu wanaoishi na tatizo hili watambuliwe rasmi kama walemavu na wawe wakipewa msaada na serikali kugharimia matibabu yao ambayo ni ghali mno.

“Serikali inafaa kuwa na takwimu za idadi ya watu walio na tatizo la selimundu nchini na iwatambue kama walemavu kama ilivyo katika mataifa mengi ya Ulaya. Matibabu ya ghali mno na Wakenya wengi, haswa kutoka familia maskini hawawezi kumudu,” anasema.

Kulingana na Wizara ya Afya, watoto 6,000 huzaliwa na tatizo la selimundu kila mwaka nchini Kenya.

Lakini kati ya asilimia 50 na 80 ya watoto wanaozaliwa na tatizo hili hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Brian anasema kuwa wengi wa watoto hufariki kwa sababu wazazi hawana ufahamu wa kutosha kuhusiana na maradhi haya, hivyo hawachukui hatua za haraka kuwatafutia matibabu.

“Damu inapokwama mwilini, mgonjwa anahitaji matibabu ya dharura. Lakini mara nyingi mgonjwa mwenye tatizo hili anapoenda hospitalini, haswa hospitali za umma kama vile Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), anawekwa kungojea kwenye foleni. Kuna uwezekano mkubwa wa mgonjwa kufariki akiwa kwenye foleni,” anasema.

Brian anapendekeza kuwa kila hospitali iwe na chumba spesheli cha wagonjwa wa selimundu ili wapate matibabu ya dharura badala ya kuwekwa kungojea kwenye foleni kwa muda mrefu.

Waziri Msaidizi wa Afya (CAS) Dkt Rashid Aman anasema kuwa watu walio na tatizo la selimundu wako katika hatari kubwa ya kulemewa na virusi vya corona kwa sababu kingamwili zao ni dhaifu.

Kutokana na hofu ya kuambukizwa corona, Brian anasema kuwa amekuwa akijilinda kwa kukaa ndani ya nyumba tangu kisa cha kwanza kuripotiwa humu nchini miezi minane iliyopita.

“Ninatoka tu ndani ya nyumba kwenda hospitalini. Lakini mara nyingi daktari hunipa ushauri wa kimatibabu kwa njia ya simu. Sipendi maeneo yenye misongamano ya watu na ninafuata kikamilifu masharti yaliyowekwa na wizara ya Afya ili kujikinga na corona,” anasema.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watoto 240,000 huzaliwa na selimundu barani Afrika kila mwaka. Watoto 300,000 huzaliwa na tatizo hili kote duniani kila mwaka.

Asilimia tano ya watu duniani, hubeba chembe za selimundu ambazo huzipitisha kwa kizazi kingine, kwa mujibu wa WHO. Mtu anaweza kubeba chembe za ugonjwa huo bila kujua na kuzipitisha kwa mwanawe au mjukuu wake.

Brian anasema kuwa hajawahi kusikia mtu aliyekuwa na selimundu katika familia yake.

“Inawezekana mmoja wa mababu zangu kutoka upande wa mama au baba, alikuwa nao. Unajua zamani hakukuwa na vipimo hivyo si rahisi kujua,” anasema.

Vilevile anahimiza serikali kuhamasisha umma kuhusu namna ya kuishi na watu walio na tatizo hili.

“Tunakumbana na unyanyapaa tele. Baadhi ya marafiki au jamaa wanapojua kwamba nina selimundu wanaanza kunitenga. Unyanyapaa huo unatuongezea msongo wa mawazo. Sisi tunahitaji upendo na wala si kubaguliwa. Msongo wa mawazo, baridi kali na joto jingi kupindukia ni miongoni mwa mambo yanayosababisha damu kuganda ghafla mwilini,” anasema.

Aidha anasema kuwa upendo ambao baadhi ya waathiriwa wamekuwa wakipata, umewawezesha kutokata tamaa maishani.

“Watu tunaoishi na selimundu tuna kikundi cha WhatsApp ambapo nimekuwa nikisikia baadhi ya wenzetu wakisema kuwa upendo wanaopewa na familia zao unawapa nguvu ya kutamani kuendelea kuishi. Wengi wanasema kuwa wasingelikuwa na watoto na wake, wangelikuwa wamejitoa uhai ili kuondokea shida wanayokumbana nayo hapa duniani.

“Hata mimi nina imani kuwa siku moja Mungu atanipa mke na watoto watakaonipenda na kunipa nguvu ya kuendelea kupigana na ugonjwa huu kwa ujasiri,” anasema.