Makala

SHINA LA AFYA: Mapafu yasiyo na dosari hupunguza makali ya Covid-19

May 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na LEONARD ONYANGO

MITANDAONI kuna ushauri tele kuhusu jinsi ya kuepuka kuambukizwa virusi vya corona.

Miongoni mwa ushauri uliojazana mitandaoni unatoka kwa wanasiasa wasiokuwa na taaluma ya matibabu pamoja na makundi ya watafiti.

Kwa mfano, Rais wa Amerika Donald Trump alishangaza ulimwengu Aprili alipopendekeza kuwa dawa ya kuua viini (disinfectant) inaweza kuua virusi vya corona mwilini.

Rais wa Tanzania John Magufuli naye ameshikilia kwamba maombi ndiyo yanaweza kumaliza corona.

Baadhi ya watafiti wamekuwa wakidai kuwa vitamin D ambayo hupatikana kwa kuota jua, inaweza kupunguza makali ya virusi hivi.

Kadhalika, kumekuwa na madai kuwa kunywa maji moto yaliyo na ndimu pamoja na kitunguu saumu kunasaidia kuangamiza virusi hivi kooni.

Wiki iliyopita, kikosi cha watafiti wakiongozwa na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Cardiff cha nchini Uingereza, walidai kuwa dawa ya kusafishia mdomo (mouthwash) inaweza kumaliza Covid-19. Kulingana na watafiti hao, dawa hiyo ina kemikali inayoweza kuharibu virusi.

Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya watu dhidi ya kutumia ‘mouthwash’ kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya corona.

Aidha wataalamu wanaonya watu dhidi kuamini kila ushauri wanaokumbana nao mtandaoni. Wanasema kuwa njia pekee ya kuaminika ya kupunguza makali ni kuepuka mitindo ya maisha inayohatarisha mfumo wa upumuaji.

Corona ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa kupumua. Hiyo inamaanisha kuwa ikiwa mfumo wa kupumua una dosari, ni rahisi kulemewa.

Virusi vya corona vinapoingia mwilini kupitia pua, mdomo au macho, hukwenda moja kwa moja hadi kwenye mapafu.

Mapafu ndiyo huhusika katika kuweka hewa ya oksijeni kwenye damu. Kisha damu husambaza oksijeni kwenye sehemu zote za mwili.

Virusi hivi vinapofika mapafuni, mapafu huanza kukabiliana navyo. Makabiliano hayo husababisha yashindwe kutia hewa ya oksijeni kwenye damu na kuondoa gesi chafu ya kabondayoksaidi.

Damu inapokosa oksijeni ya kutosha, husababisha mwathiriwa kuwa na matatizo ya kupumua. Ugumu wa kupumua ni miongoni mwa dalili kuu za virusi vya corona bali na mwili kuwa na joto jingi. Dalili nyingine ni kikohozi kikavu, maumivu ya kichwa na mwili na mara nyingine kukosa hamu ya chakula.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa mtu aliye na matatizo ya mapafu au mfumo wa upumuaji kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi anapopatwa na virusi vya corona.

Hata hivyo wanasema kuwa inawezekana kwa watu kuboresha afya ya mfumo wa kupumua ili kuepuka kulemewa endapo watapatwa na maambukizi.

Dkt Robert Eitches ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kinga ya mwili katika hospitali ya Cedars-Sinai, Los Angeles nchini Amerika, alinukuliwa na mtandao wa CNN akisema kuwa kuna baadhi ya mambo unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano wa kuwa mgonjwa mahututi endapo utaambukizwa virusi vya corona kama vile;

Kuepuka kuvuta sigara au bangi

Moja ya hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa upumuaji ni kuepuka vitu vinavyodhuru mapafu kama vile uvutaji wa sigara, bangi, na kadhalika.

“Moshi wa sigara una chembe ndogo ambazo hukwama kwenye mapafu. Chembechembe hizo huharibu mapafu na kuyakosesha uwezo wa kukabiliana na virusi au bakteria wanaosababisha maradhi,” anasema Dkt Eitches.

Kuna hofu kuwa huenda idadi ya watu wanaovuta bangi ili ‘kupunguza’ msongo wa mawazo wakati huu wa janga la corona imeongezeka.

Lakini madaktari wanaonya kuwa kuvuta hata kiasi kidogo cha sigara au bangi kunaweka mtumiaji katika hatari kubwa ya kuwa mgonjwa mahututi iwapo ataambukizwa corona.

“Unapovuta bangi kunakuwa na mwasho kwenye mapafu. Mwasho huo unapokutana na virusi vya corona husababisha afya ya mwathiriwa kudorora,” anasema Dkt Jefferson Mboya, Nairobi.

Kulingana na takwimu za WHO zilizotolewa miezi minne iliyopita, idadi ya Wakenya wa umri wa miaka 15 na zaidi wanaovuta sigara ni milioni 5.9.

Hata hivyo, WHO inasema kuwa idadi ya wavutaji wa sigara nchini imepungua kwa asilimia 16 ikilinganishwa na miaka 20 iliyopita.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa idadi ya wanawake wanaovuta sigara imepungua maradufu kutoka asilimia 4.1 mnamo 2000 hadi asilimia 2.2 mwaka huu.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa Wakenya 30,000 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayohusiana na uvutaji wa sigara.

Serikali inahofia kuwa idadi hiyo huenda ikaongezeka kufuatia mkurupuko wa corona.

Kufanya mazoezi

Mazoezi yanaboresha afya ya mapafu, kulingana na wataalamu wa masuala ya afya.

Shirika la WHO linakadiria kuwa mtu mmoja kati ya wanne hafanyi mazoezi kote duniani.

WHO inasema kuwa kutofanya mazoezi ni miongoni mwa visababishi vya vifo kote duniani.

Asilimia 80 ya vijana wa kati ya umri wa miaka 5 na 17 hawafanyi mazoezi hata kidogo, kwa mujibu wa WHO.

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa (UN) linashauri kuwa vijana wa kati ya umri wa miaka 5 na 17 wanastahili kufanya mazoezi ya viungo kwa angalau dakika 60 kwa wiki.

Shughuli nyingine zinazohitaji nguvu kama vile kulima, kubeba mizigo pia zinasaidia kuboresha afya ya viungo.

Watu wa umri wa kati ya miaka 18 na 65 wanafaa kufanya mazoezi ya viungo kwa angalau dakika 150 kwa wiki.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa mazoezi yanawezesha mtu kupumua kwa kasi hivyo kufungua mishipa ya kupitisha hewa kwenye mapafu. Wanaofanya mazoezi ya viungo si rahisi kwao kuishiwa na pumzi wanapopatwa na virusi vya corona.

Kamasi

Kamasi husaidia pakubwa katika kuboresha afya ya mfumo wa upumuaji kwani husaidia kunasa viini, bakteria na virusi.

Lakini wataalamu wanasema kuwa kamasi zinapokuwa nyingi kupita kiasi na kugandana, hugeuka kuwa makazi ya virusi na kuzuia hewa ya oksijeni kufikia mapafu. Mwathiriwa anapopatwa na virusi vya corona hushindwa kupumua hivyo kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Dkt Mboya anasema kuwa walio katika hatari kubwa ya kushindwa kupumua kutokana na msongamano wa kamasi katika mfumo wa upumuaji ni waathiriwa wa maradhi ya pumu(asthma).

Anashauri watu kula vyakula vinavyofanya kamasi kuwa nyepesi kama vile pilipili.

“Waathiriwa wa pumu hutoa kamasi nyingi hivyo wanafaa kutumia dawa zao za kupumua (inhaler) ili kupunguza kiasi cha kamasi,” anasema.