SHINA LA UHAI: Aina za Fistula
Na PAULINE ONGAJI
NASURI ya uzazi ni uwazi usio wa kawaida unaounganisha sehemu ya uke na viungo vingine kama vile kibofu cha mkojo, utumbo mpana au rektamu.
Mara nyingi madaktari hufafanua hali hii kama shimo/tundu katika uke linaloruhusu kinyesi au mkojo kupitia ukeni.
Hali hii hasa hutokana na uchungu wa uzazi kwa muda mrefu (prolonged labour) na licha ya uterasi kuendelea kubana kama kawaida, mtoto hushindwa kutoka kutokana na kukwama kwenye fupanyonga.
Hali hii huwakumba hasa akina mama kutokana na uchungu wa uzazi kati ya siku sita na saba, pasipo usaidizi wa mhudumu wa afya aliyehitimu.
Uchungu huu husababisha mbano unaosukuma kichwa cha mtoto dhidi ya fupanyonga. Tishu nyepesi kati ya kichwa cha mtoto na fupanyonga hubanwa na kukosa kupata damu ya kutosha.
Ukosefu huu wa damu ya kutosha, hufanya tishu hizi nyepesi kuangamia na kusababisha mashimo kati ya kibofu na uke au rektamu na uke wa mama.
Hali hii ndio husababisha mgonjwa wa nasuri kushindwa kudhibiti mkojo au kinyesi.
Nasuri huwakumba hasa wanawake kutoka mataifa maskini ambapo wengi wao hujifungua pasipo usaidizi wa kimatibabu. Kuna aina mbalimbali ya nasuri ya uzazi ikiwa ni pamoja na:
• Nasuri ya kibofu (Vesicovaginal fistula): Pia inafahamika kama nasuri ya kibofu. Uwazi huu hujitokeza baina ya uke na kibofu. Kulingana na madaktari aina hii ya nasuri imekithiri sana.
• Ureterovaginal fistula. Aina hii hutokea iwapo kuna uwazi usio wa kawaida baina ya uke na mifereji inayobeba mkojo kutoka kwa figo hadi kwenye kibofu.
• Urethrovaginal fistula. Aina hii ambayo pia inafahamika kama Urethral Fistula, ni uwazi unaotokea baina ya uke na mrija unaobeba mkojo kutoka mwilini mwako.
• Rectovaginal fistula. Katika aina hii ya nasuri, uwazi uko baina ya uke na sehemu ya chini ya rektamu.
• Colovaginal fistula. Aina hii ya nasuri husababishwa na uwazi baina ya uke na utumbo mpana.
• Enterovaginal fistula. Aina hii ya nasuri ni uwazi baina ya uke na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.