• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
SHINA LA UHAI: Corona pigo kwa afya ya uzazi

SHINA LA UHAI: Corona pigo kwa afya ya uzazi

Na PAULINE ONGAJI

WIKI tatu hazijakamilika tangu Mati Nyamai, 45, kumzika marehemu mkewe, Lydia Nduku Mati, 41, lakini bado hajapata muda wa kuombeleza.

Bw Nyamai, ambaye ni mkandarasi kutoka kijiji cha Kiimani, kaunti ndogo ya Mbui-nzau, Kaunti ya Makueni, anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwalea wanawe sita, vilevile kuwasaidia kukubali uhalisia wa kifo cha ghafla cha mama yao.

Marehemu Lydia alifariki Machi 31 baada ya kuvuja damu alipokuwa akijifungua mtoto wao wa saba, ambaye pia alifariki.

“Mke wangu alitarajiwa kujifungua mnamo Machi 31 kulingana na ratiba ya kliniki. Hata hivyo mnamo Machi 30 mwendo wa saa tano usiku alianza kukumbwa na maumivu tuliyoamini kuwa uchungu wa uzazi. Lakini kutokana na sababu kuwa tayari yalikuwa masaa ya marufuku ya kutotoka nje, hatungeweza kwenda hospitalini. Pia, hakukuwa na mbinu ya usafiri kuelekea katika kituo cha matibabu, kilicho umbali wa kilomita tatu kutoka nyumbani,” anaeleza.

Ili kukabiliana na maumivu, anasema, marehemu mkewe alimshauri ampeleke kwa mkunga maarufu kijijini ili atumie utaalamu wake kupunguza uchungu, huku akisubiri kwenda hospitalini keshoye.

“Tulilazimika kukatiza vichakani na giza hadi nyumbani kwake ambapo mkunga huyo alifaulu kumpunguzia maumivu. Mambo yalirejelea hali ya kawaida lakini mwendo wa saa tisa alfajiri Machi 31 tukiwa nyumbani, alianza kuvuja damu kutoka ukeni,” anakumbuka.

Kulingana na Bw Nyamai, haya yaliendelea hadi mwendo wa saa kumi na moja asubuhi (mwisho wa masaa ya kafyu) ambapo walifaulu kumpata mwendesha bodaboda aliyempeleka marehemu Lydia katika hospitali ya kaunti ndogo ya Kibwezi.

“Aliwekwa kitandani kwa saa moja ambapo baadaye walimpeleka katika thieta. Baada ya muda, daktari alirejea na kutuambia kwamba mtoto alizaliwa akiwa amefariki baada ya kusakamwa na damu akiwa tumboni,” aeleza.

Kwa upande mwingine, daktari alisema kwamba marehemu Lydia alikuwa katika hali mbaya kwani alikuwa amepoteza kiwango kikubwa cha damu, na hivyo alihitaji kuongezewa.

“Lakini tena akasema kwamba hospitali hiyo haikuwa na damu na hivyo ilibidi watafute. Mwendo wa saa nane adhuhuri walituarifu kwamba tayari walikuwa wamepata damu kutoka eneo la Voi na kwamba ambulansi ilikuwa njiani kwenda kuleta bidhaa hiyo,” aeleza.

Hata hivyo, mwendo wa saa kumi jioni; hata kabla ya ambulansi kufika hospitalini, Bw Nyamai anasema walipokea taarifa za huzuni kutoka kwa daktari kwamba mkewe alikuwa ameaga dunia.

“Daktari alituandikia idhini ya kuturuhusu kurejesha mwili wake nyumbani na siku iliyofuatia – chini ya masaa 24 baada ya kifo chake, tukamzika, pasipo ibada yoyote ya wafu wala upigwaji picha, kuambatana na utamaduni wetu,” aongeza.

Anasema kwamba bado hajaamini kwamba mkewe hayupo tena, lakini anasisitiza kwamba hana muda wa kuwazia hayo hasa wakati huu wa janga la maradhi ya Covid-19.

Kwa sasa anasema mawazo yake yote ameyaelekezea wanawe kwani ndiye mama na baba. “Japo sijarejea kazini, nitakapohitajika kufanya hivyo, nitalazimika kukaa masaa mengi kazini na bado najiuliza maswali kuhusu jinsi nitakavyoweza kufanya hivyo na kuwatunza wanangu pia,” aeleza.

Bw Nyamai anaamini kwamba mambo yangekuwa tofauti endapo mkewe angefikishwa hospitalini pindi alipoanza kukumbwa na uchungu wa uzazi licha ya marufuku ya kutotoka nje, au endapo angepokea damu pindi alipofika hospitalini. “Naamini kwamba hangefariki,” asisitiza.

Japo kuna data chache kuhusiana na athari za maradhi ya COVID-19 kwa wanawake wajawazito, wataalamu wanahofia kwamba hatua ya marufuku ya kutotoka nje, iliyochukuliwa na mataifa mbalimbali ili kupunguza usambazaji wa maradhi haya, yaweza sababisha ongezeko la vifo vya wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

Wanatabiri haya kuambatana na matukio ya yaliyoshuhudiwa wakati wa mkurupuko wa maradhi ya Ebola katika baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi kati ya mwaka wa 2014 na 2016.

Mwaka wa 2015, UNFPA ilitabiri kwamba mkurupuko huo ungesababisha vifo 120,000 vya wanawake wajawazito na watoto wakati wa kujifungua.

Juma lililopita, Dkt Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, alitaja afya ya uzazi kuwa mojawapo ya huduma ambazo zitaathirika pakubwa kutokana na Covid-19.

Dkt Jemimah Kariuki, mtaalamu wa masuala ya uzazi na mwanajinalokojia anasema kwamba itakuwa vigumu kuzuia ongezeko la idadi ya vifo vya wanawake na watoto wakati wa uzazi, ikiwa hakuna atakayeingilia kati na kuhakikisha kwamba wanawake wajawazito wanapokea huduma wanazohitaji.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba wanawake wajawazito hawataenda hospitalini au kufika wakiwa wamechelewa wakihofia kuambukizwa maradhi haya katika vituo vya kiafya. Hii inamaanisha kwamba kutakuwa na ongezeko la idadi ya akina mama watakaojifungua wakiwa nyumbani, suala litakalowaweka katika hatari zaidi,” aongeza.

Sio hayo tu, Dkt Kariuki anasema kwamba mara nyingi wakati wa mkurupuko, rasilimali nyingi huondolewa kutoka huduma za uzazi na kuelekezewa sehemu zingine zinazodhaniwa kuwa za dharura.

“Tayari hospitali ya Kaunti ya Mbagathi imetengewa matibabu dhidi ya maradhi haya. Hali hii ni sawa katika baadhi ya sehemu za hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta. Naelewa umuhimu wa hatua ya serikali, lakini hospitali hizi hushughulikia idadi kubwa ya wanawake wajawazito, suala ambalo bila shaka litaathiri kutolewa kwa huduma hizi,” aeleza.

Kwa sasa Dkt Kariuki asema zahanati, kliniki na vituo vingine vya kiafya vinapaswa kushughulikia visa vya kawaida vya kujifungua, huku wajawazito wanaohitaji huduma za dharura pekee wakiruhusiwa kwenda katika hospitali za viwango vya juu. Hii itazuia msongamano katika hospitali hizi hasa wakati huu wa janga la corona,” aeleza.

Dkt Kariuki ambaye mnamo Aprili 7, 2020, alianzisha kampeni za kusaidia wanawake wajawazito kufikia huduma za uzazi wakati huu anachelea kwamba kuna uwezekano wa akina mama kumiminika hospitalini licha ya kutokumbwa na dharura.

“Nimesikia visa kuhusu wanawake waliojawa na hofu wanaoenda hospitalini usiku licha ya kutokumbwa na uchungu wa uzazi wala hali ya dharura yoyote. Wengi wanakwamilia hospitalini baada ya kuambiwa warejee nyumbani,” aongeza.

Kulingana na Dkt Kariuki, ili kujiepusha na hali ya aina hii, wanawake wajawazito wanaweza tumia huduma za kuwasiliana kwa majukwaa ya kieletroniki (telemedicine), kuzungumza na madaktari wao kuhusu masuala madogo madogo ya kiafya, na hivyo kuzuia mtagusano usiohitajika.

Pia, anasisitiza haja ya kuwaelimisha kuhusu wanachopaswa kufanya wanapohisi namna fulani, vile vile dalili za kukumbwa na hali ya dharura ili waweze kufika hospitalini kwa wakati ufaao kabla ya masaa ya kafyu.

Ili kuzuia balaa kama iliyoshuhudiwa katika mataifa ya Magharibi mwa Afrika wakati wa mkurupuko wa Ebola, Dkt Kariuki anapendekeza kuajiriwa sio tu kwa madaktari zaidi, bali pia wahudumu wengine wa kiafya.

“Utambuzi mmoja wa virusi vya corona hospitalini unalazimu wahudumu wa kiafya waliomshughulikia mhusika kuwekwa kwenye karantini ya lazima, suala linaloathiri hata zaidi idadi ya wahudumu wa kiafya. Kutokana na sababu hii, madaktari na wahudumu zaidi wa kiafya wanapaswa kuajiriwa hata katika viwango vya kaunti, pindi wanapokamilisha masomo,” aongeza.

You can share this post!

TAHARIRI: Tusilegeze kamba dhidi ya corona

Fifa yapendekeza timu ziruhusiwe kubadilisha wachezaji...

adminleo