SHINA LA UHAI: Hepatitisi: Watu wazima hatarini zaidi
Na LEONARD ONYANGO
HUKU ulimwengu ukiadhimisha siku ya Hepatitisi leo Jumanne, serikali imeelezea wasiwasi wake kuhusu damu ‘chafu’ inayokusanywa na Taasisi ya Kitaifa ya Kukusanya Damu (KNBTS) kutoka kwa vijana.
Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Rashid Aman, mwezi uliopita alifichua kuwa kiasi kikubwa cha damu inayotolewa na vijana imechafuliwa na virusi vinavyosababisha maradhi kama vile homa ya ini (hepatitisi A na B) HIV na kaswende.
Asilimia 80 ya damu inayotumiwa katika hospitali za humu nchini kuongezea wagonjwa wenye upungufu hutolewa kwa hiari na vijana wa kati ya umri wa miaka 16 na 25, kwa mujibu wa KNBTS.
Asilimia 60 ya damu hutolewa na wanafunzi wa shule za sekondari huku wenzao wa vyuoni wakichangia asilimia 20.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Nairobi kwa ushirikiano na KNBTS iliyochapishwa katika jarida la BioMed Research International mnamo Juni, mwaka huu, ilionyesha kuwa kiasi kikubwa cha damu inayotolewa na vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 25 imesheheni virusi vya Hepatitisi B (HBV).
Watafiti hao walipima sampuli 1000 katika Kaunti ya Kisumu na 34 kati yazo zilikuwa na virusi vya maradhi ya HBV.
Kulingana na ripoti hiyo, idadi kubwa ya vijana walio na chale (tattoo) mwilini wana virusi vinayosababisha ugonjwa wa HBV.
“Vifaa vinavyotumiwa kuchanja chale kwenye ngozi hueneza virusi vya HBV kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine,” inasema ripoti hiyo.
Mike Muigai ambaye hutoza wateja wake kati ya Sh150 na Sh300 kuchanja chale ndogo mtaani Kayole, jijini Nairobi anasema kuwa hajawahi kusikia lolote kuhusu ugonjwa wa Hepatitisi B na wala hajui jinsi unavyoenezwa.
Hiyo inaweza kumaanisha kuwa Bw Muigai hajakuwa akisafisha vifaa vyake vyema kabla ya kuvitumia hivyo kuweka wateja wake katika hatari ya kupatwa na hepatitisi.
Hepatitisi B ni ugonjwa wa kuambukizwa unaosababishwa na virusi vya HBV vinavyosababisha muasho kwenye ini. Aina nyingine za ni Hepatitisi A, Hepatitis C, Hepatitisi D na Hepatitisi E.
Virusi vya Hepatitisi A na E huingia mwilini kwa kula chakula au kunywa maji machafu yaliyo na virusi vya maradhi hayo.
Virusi vya Hepatitis A hupatikana kwenye kinyesi cha mwathiriwa. Watu wanaoishi katika mazingira machafu wako katika hatari ya kupatwa na virusi hivyo.
Hata hivyo, virusi hivi vinaweza kuzuiliwa kwa chanjo. Idadi kubwa ya waathiriwa wa Hepatitis A, hupona. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mnamo 2016 maradhi hayo yalisababisha vifo 7,134 kote duniani, sawa na asilimia 0.5 ya vifo vilivyotokana na aina nyinginezo za hepatitis.
Chanjo ya Hepatitisi E ipo lakini haipatikani katika mataifa mengi licha ya ugonjwa huo kuwa hatari. Kulingana na WHO, maradhi ya Hepatitisi E yalisababisha vifo 44,000 kote duniani mnamo 2015, ambavyo ni sawa na asilimia 3.3 ya vifo vilivyosababishwa na aina nyinginezo za hepatitisi. Aina hii ya hepatitisi imekolea zaidi katika mataifa ya bara Asia.
Hepatitisi B, C na D huenezwa kupitia damu kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine au kupitia ngono.
Virusi vya HBV pia vinaweza kuenezwa kutoka kwa mama hadi mtoto. Maambukizi ya virusi hivyo yanaweza kuzuiliwa kwa kudungwa chanjo. Hii ndiyo aina ya hepatitisi ambayo ni hatari zaidi. Hepatitisi B husababisha ini kuwa ngumu na pia kansa ya ini. WHO inakadiria kuwa Hepatitisi B ilisababisha vifo 887,000 kote duniani mnamo 2015. Nchini Kenya, maambukizi ya Hepatitisi B yanakadiriwa kuwa asilimia 8 kwa mwaka.
Hepatitisi C inaweza kuenezwa kupitia damu au kwa kutumia vifaa vichafu kama vile kujidunga sindano. Hepatitisi C haina chanjo, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). Aina hii ya hepatitisi huchangia kwa kiasi kikubwa kwa kansa ya ini. WHO inakadiria kuwa kuna jumla ya watu milioni 71 walio na maradhi ya Hepatitisi C kote duniani. Shirika hilo la afya linakadiria kuwa mnamo 2016 watu 399,000 walifariki kote duniani.
Hepatitisi D huathiri tu watu wanaougua hepatitisi B hivyo kufanya hali yao kudorora zaidi. Mara nyingi huambukizwa kutoka kwa mama hadi kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Mnamo 2016, vifo vilivyosababishwa na hepatitisi vilikuwa vingi kuliko vile vilivyotokana na Ukimwi, malaria na kifua kikuu ulimwenguni, kulingana na ripoti ya utafiti kuhusu magonjwa duniani.
Wataalamu wanaonya kuwa idadi ya watu walio na maradhi ya hepatitisi humu nchini inaongezeka kwa kasi ya kutisha.
Utafiti uliofanywa humu nchini na kuchapishwa katika jarida la BMC Infectious Diseases ulibaini kuwa watu wazima nchini Kenya hawapewi chanjo dhidi ya virusi vya hepatitisi, hali ambayo huenda ikawa hatari katika siku za usoni.
Utafiti huo uliofanywa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH), Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (Eldoret), Hospitali ya New Nyanza General (Kisumu) na Hospitali Kuu ya Pwani (Mombasa) ulibaini kuwa kila eneo humu nchini linakabiliwa na aina tofauti ya hepatitisi.
Watafiti hao kutoka Taasisi ya Kutafiti Tiba (Kemri), Chuo Kikuu cha Nairobi, Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) na Maabara ya Virusi ya Canada walipima jumla ya wagonjwa 389 katika hospitali hizo.
Walibaini kuwa Hepatitisi B ndiyo inaongoza kwa maambukizi humu nchini ikifuatiwa na Hepatitisi A.
Watafiti walipata kwamba asilimia 6.3 ya wagonjwa waliopima walikuwa na Hepatitisi A. Kisumu iliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waathiriwa wa Hepatitisi A kwa asilimia 9.2 ikifuatiwa na Nairobi (asilimia 6.3) na Mombasa (asilimia 5)
Kilichowashangaza watafiti hao ni kwamba asilimia 6.3 ya sampuli 382 zilizopimwa walikuwa watu wazima waliopatikana na virusi vya Hepatitisi A.
Hiyo inamaanisha kuwa watu wazima pia wanafaa kupewa chanjo ya kuwakinga dhidi ya Hepatitisi A. Waathiriwa wengi wa aina hii ya hepatitisi wanaishi katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu haswa mjini.
Asilimia 50.6 ya sampuli zilizopimwa zilipatikana na virusi vya HBV. Mji wa Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu, uliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waathiriwa wa Hepatitisi B kwa asilimia 92.9, ukifuatiwa na Mombasa (asilimia 81.8), Wagonjwa 128 kati ya 168 waliopatikana na Hepatitisi B walikuwa katika hali mbaya.
Watafiti hao walibaini kuwa idadi kubwa ya wanawake, haswa wajawazito, walikuwa na virusi vya Hepatitisi E kuliko wanaume.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa maradhi ya Hepatitis B yamekolea zaidi katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa Kenya kwa asilimia (13.9).
Kwa mfano, Katibu wa Kaunti ya Mandera Abdinur Maalim Hussein anasema kuwa asilimia 4.5 ya wahudumu wa afya waliopimwa hivi karibuni katika hospitali mbalimbali za eneo hilo walipatikana na virusi vya Hepatitisi B.
“Tafiti ambazo zimefanywa zinaonyesha kuwa uwepo wa idadi kubwa ya watu walio na virusi vya Hepatitisi B katika eneo la Kaskazini Mashariki unatokana na uendelezaji wa tamaduni hatari kama vile ukeketaji wa wanawake, kuoa wake wengi. Kadhalika, watu wazima hawapatiwi chanjo ya Hepatitisi B hivyo wanaendelea kuambukizana,” anasema Bw Hussein.
Idadi kubwa ya wagonjwa wa Hepatitisi C wanapatikana katika eneo la Pwani. Maambukizi ya Hepatitisi C katika maeneo ya Pwani yanakadiriwa kuwa asilima 35.
Profesa Elijah Songok, mtaalamu wa masuala ya virusi na Mtafiti Mkuu wa Kemri, jijini Nairobi anasema kuwa Hepatitisi C imekita mizizi katika eneo la Pwani kutokana na kuwepo kwa visa vingi vya matumizi ya dawa za kulevya kama vile kokeini.
“Watumiaji wa dawa za kulevya hutumia vifaa kama vile sindano kwa pamoja hivyo kuambukizana virusi vya Hepatitisi C,” anasema.
Prof Songok anasema kuwa kati ya asilimia 13 na 16 ya waathiriwa wa virusi vya hepatitisi pia wanaishi na virusi vya HIV.
“Hii inatokana na ukweli kwamba virusi vya Hepatitisi B, C na D huenezwa kupitia damu au ngono, sawa na virusi vya HIV,” anaelezea.
Chanjo
Kenya ilifanya chanjo ya Hepatitis B kuwa ya lazima miongoni mwa watoto mnamo 2002. Wengi wa watoto walio chini ya miaka 16 wamepewa chanjo hiyo.
Lakini Prof Songok anasema kuwa mpango huo wa serikali kuhusu chanjo ya lazima kwa watoto haujatathminiwa ili kubaini mafanikio yake.
Ili kuzuia maambukizi ya Hepatitis B na C miongoni mwa wagonjwa, Prof Songok anasema, damu imekuwa ikipimwa kwa kina kabla ya kuongezewa wagonjwa.
“Damu inayopatikana na hepatitisi inatupwa na watu waliotolewa hufahamishwa na kushauriwa kutafuta huduma za matibabu. Kwa hili, serikali ya Kenya imepiga hatua kubwa,” anaelezea.
Hata hivyo, Profesa Sangok anakosoa serikali kwa kukosa mpango wa kutoa chanjo kwa watu wazima.
Anasema chanjo iliyopo ni ghali mno na Wakenya wengi hawawezi kumudu.
“Kadhalika, serikali haijaweka juhudi za kutosha za kuzuia maambukizi ya hepatitisi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto. Akina mama wajawazito wanapoenda kliniki hawapimwi hepatitisi tofauti na HIV ambapo ni sharti wapimwe,” anasema.
Kulingana na Prof Songok, serikali haijaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa watoto wanaozaliwa na wazazi walio na hepatitisi wanapewa dawa mara tu baada ya kuzaliwa ili kuwakinga dhidi ya maradhi hayo.
Anasema kuwa dawa za kutibu Hepatitisi C ni ghali mno nchini Kenya ikilinganishwa na nchini Misri ambapo wanapata huduma hiyo kwa bei nafuu.
Wakenya wanashauriwa kwenda kupimwa ili kubaini ikiwa wana hepatitis.
Kipimo cha hepatitisi hugharimu kati ya Sh500 na Sh1, 500 na mtu anapopatikana na virusi vya maradhi hayo hufanyiwa vipimo zaidi kabla ya kuanza kutibiwa.
Matibabu ya ugonjwa wa Hepatitisi C yanagharimu Sh120,000 kwa kila mgonjwa. Kwa kawaida matibabu ya maradhi hayo huchukua muda wa miezi mitatu.
Prof Songok anasema kuwa serikali imelaza damu katika kuhamasisha Wakenya kuhusu maradhi ya hepatitis.
“Serikali imeweka juhudi nyingi sana katika kuhamasisha umma kuhusu HIV, malaria na ugonjwa wa kifua kikuu na kutelekeza hepatitisi. Itakuwa vigumu kwa Kenya kushinda hepatitisi bila kuelimisha na kuhamasisha umma,” anasema.