• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 7:50 AM
SHINA LA UHAI: Ndimu kutibu COVID-19 ni ‘Fake News’ – Ripoti

SHINA LA UHAI: Ndimu kutibu COVID-19 ni ‘Fake News’ – Ripoti

Na LEONARD ONYANGO

JE, umeona ujumbe ambao umekuwa ukisambazwa katika mitandao ya kijamii ukidai kuwa ndimu au vitamini C inasaidia kuua virusi vya homa ya corona?

Ikiwa umeuona ujumbe huo unaodaiwa kuandikwa na Laila Ahmadi, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanjan cha nchini China, basi tayari wewe ni mwathiriwa wa taarifa za kupotosha ambazo zimekuwa zikisambazwa kuhusiana na homa ya corona ambayo tayari imesababisha vifo vya watu zaidi ya 6,200 kote duniani.

Ujumbe huo ambao umekuwa ukisambazwa kwa kasi nchini Kenya na mataifa mengineyo kote ulimwenguni unadai kuwa ukinywa maji moto yaliyoongezwa ndimu utajikinga na homa ya corona.

Ili kujua kwamba ujumbe huo unapotosha, hakuna chuo kikuu nchini China kinachojulikana kama Zanjan. Mitandao inaonyesha kuwa Ahmadi anayedaiwa kuandika ujumbe huo ni muuguzi katika wadi ya kusaidia akina mama wajawazito kujifungua katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Zanjan nchini Iran.

Wataalamu wa afya pia wanasema kwamba hakuna ushahidi wa kisayansi wa kuonyesha kuwa maji moto na ndimu vinaua virusi vya corona.

Habari kuhusu maji moto na ndimu ni miongoni mwa maelfu ya taarifa za kupotosha ambazo zimekuwa zikisambazwa kuhusiana na kiini, tiba na kinga ya homa ya corona.

Habari nyinginezo ambazo zimekuwa zikisambazwa ni kwamba kunywa maji mara kwa mara kunasaidia kusukuma virusi vya corona tumboni ambapo vinauawa.

Japo wataalamu wanashauri watu kunywa maji mengi kutokana na faida zake kwa afya, wanasema kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisayansi kuthibitisha kuwa maji yana uwezo wa kusafisha virusi vya corona kooni.

Vita dhidi ya uenezaji wa habari za kupotosha kuhusiana na homa ya corona vinazidi kuchacha huku baadhi ya mitandao ya kijamii ikionekana kulemewa.

Google imepiga hatua kubwa katika kudhibiti uenezaji wa habari feki kuhusiana na homa ya corona lakini Facebook, Twitter, Whatsapp, Tik Tok na mitandao mingineyo inaonekana kulemewa.

Mtandao wa Google umepiga mrufuku maelfu ya programu za simu (apps) zinazodai kutoa taarifa kuhusu homa ya corona (Covid-19). Hiyo inamaanisha kuwa app za corona hazipatikani katika mtandao wa ‘Google Play’.

Homa ya corona ambayo ilianzia jijini Wuhan nchini China tayari imeambukiza zaidi ya watu 163,000 kote duniani na kati yao zaidi ya 6,100 wamefariki dunia. Watu 76,200, hata hivyo, wamepona.

Idadi hiyo inamaanisha kuwa uwezekano wa kupona baada ya kuambukizwa maradhi hayo ni asilimia 93.

Mtandao wa Google ambao pia humiliki YouTube umekuwa ukiondoa video zinazotoa taarifa za kupotosha kuhusiana na homa ya corona.

Mtandao wa Facebook umeanza kuondoa matangazo ya kupotosha yanayodai kutoa tiba au kinga ya kutibu homa ya corona.

Mtandao wa Facebook pia unawashauri watumiaji wake kutafuta taarifa za kweli kuhusiana na maradhi ya corona katika tovuti za mashirika yaliyoidhinishwa kama vile Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wizara ya Afya.

Mtandao wa Twitter umeshutumiwa kwa kuwa kitovu cha habari za kupotosha kuhusiana na homa ya corona.

Miongoni mwa taarifa za kupotosha ambazo zimekuwa zikisambazwa kupitia Twitter ni madai kwamba dawa za kuua viini vya corona mikononi (sanitiser) haina uwezo wa kuua virusi vya corona.

Lakini shirika la WHO linasisitiza kuwa dawa hiyo inasaidia pakubwa kuua viini vya corona.

WHO pia inahimiza watu kunawa kwa sabuni na maji kama njia mojawapo ya kuzuia virusi vya corona kusambaa kutoka kwenye mikono hadi kinywani, puani au machoni.

Mtandao wa WhatsApp ambao una watumiaji zaidi ya bilioni 2 kote duniani pia umeshutumiwa vikali kwa kushindwa kudhibiti taarifa feki kuhusu virusi vya corona.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ongezeko la mimba za mapema fumbo...

MAZINGIRA NA SAYANSI: Maji ya bahari hayaui virusi vya...

adminleo