• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
SHINA LA UHAI: Tatizo la maumbile lifanyalo matiti kuwa makubwa kupindukia

SHINA LA UHAI: Tatizo la maumbile lifanyalo matiti kuwa makubwa kupindukia

Na PAULINE ONGAJI

AKIWA katika shule ya msingi, Elizabeth Mbole, 30, alikejeliwa na wenzake kwamba matiti yake makubwa yanatokana na mazoea ya kupapaswa na wanaume.

Ni matamshi yaliyomchoma mtima na hata kumfanya kujihisi kutopendeza ila pia ni wakati huu Bi Mbole alianza kugundua kuwa maumbile yake yana kasoro.

“Matiti yangu yalianza kulegea, na tofauti na wenzangu, katika umri wa miaka 15 nilikuwa nimeanza kuvaa sidiria,” asema.

Hangeweza kushiriki katika shughuli zingine shuleni kama vile michezo kwani kifua chake kikubwa kilikuwa kimeanza kuwa kizito na kumpa maumivu pia.

“Ni hali ambayo ilinitia wasiwasi na nikamfungulia roho nyanya ambaye nilikuwa na ukaribu naye. Lakini kila nilipomtajia, alinituliza kwa kuniambia kuwa litaisha baada ya kuzaa na kunyonyesha,” aeleza.

Wazazi wake hawakuwa na majibu hata baada ya kuwashinikiza hasa ikizingatiwa kuwa hakuna jamaa yeyote mwingine alikuwa na tatizo kama lake.

“Mamangu alikuwa akiniambia kwamba ni jambo la kawaida, na kwamba halina suluhu,” anasema.

Kwa hivyo kwa miaka alivulimia kejeli na bezo asijue la kufanya.

“Hata nilikuwa nimebandikwa jina ‘Madam Matiti’ huku baadhi ya wanaume wakinitania kwamba waliyafurahia,” aeleza.

Hatimaye alimzaa bintiye huku akiwa na uhakika kuwa ushauri wa nyanya ungetimia ila mambo hayakubadilika. Badala yake yalizidi kuwa makubwa na mazito zaidi na nyanya akamsisitizia azae tena na kunyonyesha ili kuyapunguza, ushauri ambao wakati huu aliupuuza.

“Lakini muda ulivyozidi kusonga, mambo yalizidi kuwa mabaya kwani nilianza kuhisi maumviu makali na hata kushindwa kufanya mambo ya kawaida kama vile kupanda ngazi. Katika taaluma yangu kama karani wa masuala ya kisheria, nilikuwa nasafiri sana kikazi ambapo katika juhudi hizi, nililazimika kubeba vipini kwani mikanda ya sidiria ingekatika wakati wowote,” aongeza.

Hali hii ilimnyima starehe kazini na hata kuzima ule motisha wa kufanya kazi. Mara nyingi alitaka kukaa tu nyumbani.

Hii ni kwa sababu pia watu aliokuwa akiwasilisha habari kwao, walikuwa wakikodolea macho kifua chake badala ya kumsikiliza. Hali ambayo alihisi ilimvunjia heshima na kushusha imani yake.

“Hii iliathiri motisha wangu wa kufanya kazi. Nilitamani tu kukaa nyumbani. Hata nilipofua sidiria zangu, nilikuwa nikizianika ndani ya nyumba kwa kuhofia majirani watanisuta,” asema.

Isitoshe, aliacha kutangamana na watu na hata kuunda urafiki na utendakazi wake pia ulianza kuzorota.

Mwishowe alichoka na maisha ya kujitenga na upweke na akaamua kutafuta suluhu kwa kwenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi zaidi. Katika pilkapilka hizi, Oktoba 2017 alikumbana na habari ambazo baadaye zilikuja kumfaa pakubwa.

“Binti fulani alikuwa amechapisha katika kikundi kimoja cha kupunguza uzani kwamba alikabliwa na wakati mgumu kupunguza ukubwa wa matiti yake. Nilifuatilia hadithi hii ambapo mmojawapo wa wanachama alimpendekezea afanye utafiti kuhusu tatizo linalofahamika kama Gigantomastia,” aeleza.

Hii ilimpa ari ya kufanya utafiti zaidi na kutafuta usaidizi ambao kwa bahati nzuri aliupata kutoka kwa Wakfu wa Gigantomastia ( Gigantomastia Foundation) uliogharimia matibabu yake. Na Julai mwaka jana, Bi Mbole alifanyiwa upasuaji wa kupunguza matiti kwa jina Breast Reduction Mammoplasty.

Ruth Makena, mwanzilishi wa wakfu huu ambao umekuwa ukiwapa matumaini ya kurejelea maisha yao ya kawaida wanaokumbwa na hali hii anasema kwamba, hili ni janga ambalo limepuuzwa.

“Changamoto kuu ni fedha. Wanawake wengi wanazidi kuugua kisiri hasa kutokana na sababu kwamba wengi hawawezi kumudu gharama ya upasuaji,” asema Bi Makena ambaye pia aliwahi kukumbwa na hali hii.

Kulingana na Dkt Martin Ajujo, daktari wa upasuaji wa kurekebisha hitilafu mwilini katika Chuo Kikuu cha Nairobi, Breast Hyperplasia au Gigantomastia kama inavyofahamika, ni tatizo adimu linalosababisha matiti kukua zaidi ya kawaida.

“Tatizo hili laweza kutokea bila sababu, katika umri wa kubalehe, wakati wa ujauzito au kutokana na matumizi ya aina fulani ya dawa. Hata baada ya upasuaji, huenda likajitokeza tena,” asema.

Chanzo

Kulingana naye, haijulikani nini hasa husababisha hali hii lakini kuna mambo kadha wa kadha ambayo yaweza kuchangia.

Aidha, Dkt Ajujo anasema kwamba jeni pia zaweza kusababisha hali hii.

“Kwa kawaida wanawake wa Kiafrika wameumbwa na matiti makubwa wakilinganishwa na wale wa asili zingine, suala linalofafanua kwa nini tatizo hili huwakumba wanawake weusi zaidi.”

Pia, anasema kwamba unene kupindukia unamweka mtu katika hatari ya kukumbwa na hali hii, lakini haimaanishi kwamba ukipunguza uzani, basi utakabiliana na tatizo leneyewe.

Hapa nchini Kenya hakuna takwimu rasmi kuhusu tatizo hili. Hata hivyo tafiti kadha za kimataifa zinaonyesha kwamba, endapo ni kutokana na ujauzito, humkumba mwanamke mmoja kati ya 100,000 duniani kote.

“Ishara ni pamoja na matiti kulegea ambapo hii huandamana na ishara zingine kama vile maumivu ya shingo, mgongo, kubadilika kwa rangi ya ngozi chini ya matiti, maumivu ya uti wa mgongo na matatizo ya kupumua,” asema.

Mbali na matatizo ya kimwili, Dkt Ajujo anasema kwamba hali hii yaweza kumsababishia mgonjwa mfadhaiko kutokana na kukejeliwa.

Tiba

Lakini kuna matumaini kwa wagonjwa, huku mbinu mwafaka na thabiti zaidi ya matibabu ikiwa ni upasuaji wa kupunguza ukubwa wa matiti. “Upasuaji huu unahusisha kuondolewa kwa mafuta, tishu na ngozi kutoka sehemu hii, na mwishowe kuziunda ili kuchukua umbo la kawaida,” aeleza.

Dkt Ajujo, anakadiria kwamba kila mwaka kati ya upasuaji 300 na 400 wa kupunguza ukubwa wa matiti hufanywa nchini.

Kwa kawaida anasema kwamba shughuli hii huchukua kadri ya masaa mawili unusu.

“Hapa nchini, upasuaji huu waweza kugharimu kati ya Sh500,000 na Sh800,000 miongoni mwa wanawake,” adokeza.

Huathiri wanaume pia

Anasema kwamba sio tu wanawake wanaokumbwa na hali hii. “Kuna wanaume ambao hutaabika kisiri kutokana na tatizo hili. Miongoni mwa wanaume, tatizo hili huitwa gynecomastia, kumaanisha kuvimba kwa tishu za matiti. “Wanaume wanawakilisha kati ya 30% na 40% ya wagonjwa wanaosaka huduma za upasuaji kupunguza ukubwa wa matiti,” asema, huku akiongeza kwamba kwa wanaume, upasuaji hugharimu kati ya Sh300,000 na Sh400,000.

Dkt Ajujo anasema kwamba gynecomastia husababishwa na kutokuwa na usawa kati ya homoni za estrogen

na testosterone. “Mara nyingi wavulana huanza kushuhudia tatizo hili katika umri wa kubalehe, huku wanaume wakianza kuathirika kutokana na mabadiliko ya viwango vya homoni. Aidha, tatizo hili laweza kutokana na chakula, matumizi ya pombe na jeni,” asema.

Japo mgonjwa ana uwezekano wa kuendelea kuishi maisha ya kawaida baada ya upasuaji, Dkt Ajujo anasema kwamba changamoto kuu ni kwamba utaratibu huu ni ghali mno, suala linalozima wengi kufuatilia matibabu.

“Ni vigumu kupata bima ya afya kwa matibabu haya sababu kampuni nyingi za bima huchukulia utaratibu huu kuwa wa kimapambo(plastic surgery),” asema Dkt Ajujo.

Hasa kwa wanawake, anasisitiza kwamba upasuaji huu ni wa kimatibabu kwani endapo mgonjwa hatatibiwa, basi huenda akakumbwa na matatizo zaidi ya kiafya katika siku za usoni.

“Kuna hatari ya kukumbwa na majeraha ya uti wa mgongo, mabega na hata vidonda ambavyo huenda vikabadilika na kuwa kansa.”

Sio hayo tu, anasema kwamba kwa baadhi ya wanawake, huenda tatizo hili likapunguza uzalishaji maziwa kwa sababu tishu za matiti hufinya vifuko vya kuhifadhi maziwa.

Kwa upande wa wanaume pia, anasema kwamba endapo tatizo hili halitakabiliwa, huenda likasababisha matatizo ya kiafya kama vile kansa hasa iwapo ni upande mmoja ulioathirika.

  • Tags

You can share this post!

Kivumbi Gulf African Bank ikivaana na ECO Bank

Inspekta Mwala alimuua jamaa wetu, hafai kuachiliwa kwa...

adminleo