• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
SHINA LA UHAI: Unene kupindukia shina la maradhi mengi duniani

SHINA LA UHAI: Unene kupindukia shina la maradhi mengi duniani

Na BENSON MATHEKA

MIONGONI mwa maradhi yanayohusishwa na mitindo ya maisha ni unene kupindukia.

Madaktari wanasema ugonjwa huu ndio shina la maradhi mengi yanayotokana na mitindo ya maisha ya watu yakiwemo Kisukari.

Kulingana na Dkt Swati Das wa hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi, unene wa mwili unasabababishia mtu matatizo ya kupumua, moyo, kisukari na msukumo wa damu.

“Unene wa mwili hutokana na mwili kuwa na mafuta mengi ambayo huwa yanazuia viungo vya mwili kufanya kazi vyema na kuathiri utendakazi wake,” aeleza Dkt Das.

Anasema unene wa mwili ni tatizo kubwa la kiafya kwa sababu unasababisha maradhi mengine ikiwa ni pamoja na baadhi ya saratani zinazoangamiza watu.

Wataalamu wanasema kwamba baadhi ya watu huwa na wakati mgumu kupunguza uzani kwa sababu ya jeni wanazorithi, mazingira, lishe na mazoezi wanayochagua kufanya au kushindwa kufanya kabisa.

“Hata hivyo, mtu akijitahidi na kupunguza unene kwa kilo chache, anaweza kuepuka hatari ya kupata maradhi yanayosababishwa na unene kupindukia,” aeleza Dkt Das.

Madaktari wanasema mtu hugunduliwa kuwa mnene kupindukia wakati kiwango cha nyama mwilini (BMI) kinazidi kilo 30 ikilinganisha na kimo chake.

BMI hupatikana kwa kugawa uzani wa mtu na kimo chake. Kipimo sahihi cha BMI ni kati ya 18-25.

Wataalamu wanasema BMI huwezesha mtu kukadiria kiwango cha mafuta katika mwili wake japo sio kipimo halisi cha mafuta mwilini.

Kulingana na Dkt Das, mtu anapaswa kumuona daktari akiwa na hofu kuhusu unene wake wa mwili ili apate ushauri wa jinsi ya kuupunguza.

“Hii ni kwa sababu kuna vichocheo tofauti vya unene kupindukia kama vile jeni, lishe na homoni za mwili. Hata hivyo muhimu ni mtu kuhakikisha anafanya mazoezi ili kupunguza kiwango cha mafuta na kalori mwilini,” aeleza Dkt Das.

Mbali na lishe, wataalamu wanasema baadhi ya pombe na vinywaji visivyolewesha vinavyotengenezwa kwa sukari kama vile soda na juisi, vinachangia hali hii.

Kuketi kwa muda mrefu

Aidha, watu wanaoketi kwa muda mrefu wakifanya kazi, pia wanakabiliwa na hatari ya kuwa na mili minene.

Kadhalika baadhi ya watu hupata mili minene kutokana na dawa wanazotumia kwa muda mrefu.

“Baadhi ya dawa zinaweza kufanya mtu kuwa na mwili mnene akikosa kufanya mazoezi na kupata lishe bora,” asema Dkt Patrick Njogu wa hospitali ya Bristol, mjini Machakos.

Wataalamu wanasema inaweza kuwa vigumu kwa mtu kupunguza unene wa mwili ikiwa watu anaoshinda nao hawapendi kufanya mazoezi na kutumia lishe bora.

Wanaongeza kuwa mtu anaweza kunenepa uzee unapobisha.

“Unene wa mwili haubagui wakubwa kwa wadogo. Hata hivyo, mtu anapozeeka, homoni za mwili huleta mabadiliko mwilini. Katika uzeeni, watu huwa hawafanyi kazi na mazoezi kwa wingi jambo linalowaweka katika hatari ya kuwa na mili minene,” asema Dkt Njogu.

Wataalamu wanashauri akina mama kufanya mazoezi baada ya kujifungua kwa sababu huwa katika hatari ya kuongeza uzani kupindukia.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa Kisukari haubagui na huua...

TEKNOHAMA: Google si daktari, wasema watafiti

adminleo