Shinikizo za maisha zilimwacha akining’inia padogo ila amegeuka msaada kwa wanaoumia kimya kimya
HUKU suala la afya ya akili likiendelea kupenya katika jamii ambayo miaka ya awali halikuchukuliwa kwa uzito, kijana Belden Magare ameibuka kuwa nembo ya ushindi licha ya giza nzito la mahangaiko.
Kama wanaume wengi nchini Kenya na kwingineko, alipambana na vita vya matatizo ya afya ya akili kimya kimya. Alizongwa na matatizo mengi ya kifamilia yaliyogeuka kuwa kesi kortini, na kuzidisha msononeko.
Ukosefu wa kazi nao ukaongeza mafadhaiko na kukata tamaa. Shinikizo kutoka kwa kanisa lake za kumtaka kuishi kulingana na matamanio ya jamii na dini zikamfanya ahisi kutengwa. Alihisi hakuna aliyeelewa mateso ya kisaikolojia aliyokuwa akipitia.
“Katika kipindi hicho cha giza, nilielewa wazi unyanyapaa unaozunguka afya ya akili, haswa kwa wanaume. Nilihitaji usaidizi wa afya ya akili ila hakuna aliyekuwa upande wangu na nikalazimika kupambana peke yangu,” anasimulia Belden.
Kutia chumvi kwenye kidonda, uhusiano wake, ambao ulikuwa chanzo cha faraja, ulivunjika wakati mchumba wake alipopata ujauzito wa mwanaume mwingine.
Usaliti huu ukamwingiza zaidi katika hali ya kukata tamaa na kumwacha akining’inia padogo.
“Afya yangu ya akili ilizorota hadi kufikia hatua ya kufikiria kujiua. Nilihisi mpweke, kwani nilitengwa na jamii ambayo mara nyingi hutarajia wanaume kubaki imara licha ya changamoto wanazopitia. Hata hivyo, katika nyakati hizo za giza, nilipata chembe ya matumaini; niliingiwa na hamu ya kuhakikisha kwamba hakuna mwanaume mwingine yeyote ambaye atateseka kimya kimya kama mimi,” anaeleza Belden.
Alipata nafasi ya kuunda jukwaa ambapo wanaume wanaweza kutafuta msaada wa afya ya akili bila kuhofia kuhukumiwa. Hapo ndipo msingi wa Seed for Hope ulizaliwa.
Tangu kuzinduliwa kwake Oktoba 2024, shughuli za shirika la Seed for Hope tayari zimeshika kasi na zaidi ya wanachama 25 wanafanya kazi pamoja kuleta mabadiliko. Misheni mbili kuu za shirika hili ni kutetea ufahamu wa afya ya akili miongoni mwa wanaume na kusaidia wanafunzi mahiri wasiojiweza ili waweze kuendeleza elimu yao.
“Kama sehemu ya dhamira yetu ya kuondoa unyanyapaa kuhusu afya ya akili miongoni mwa wanaume, shirika la Seed for Hope liliandaa mazungumzo ya Afya ya Akili na wanaume Desemba 8, 2024,” aliarifu Glantwill Ruvinzu, mkurugenzi wa elimu katika shirika la Seed for Hope Foundation.
Grantwil anasema kuwa shirika hilo linatafuta kikamilifu ushirikiano na kampuni, mashirika yasiyo ya serikali na watu binafsi wanaopenda afya ya akili na elimu.
“Ushirikiano ni ufunguo wa kupanua ufikiaji wetu na kuleta tofauti kubwa. Wale walio tayari kuunga mkono au kujiunga na programu zetu wanaweza kuwasiliana nasi. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kupanda mbegu za matumaini na kukuza jamii yenye afya bora,” anaeleza Ruvinzu.
Kulingana na Belden, Seed for Hope Foundation inakua kwa kasi, ila anakiri kuwa wanahitaji usaidizi wa kujitolea, mshirika au hata wakili akisema kuwa mchango wa mtu yeyote utakuwa muhimu mno.
“Pamoja, tunaweza kuunda ulimwengu ambapo afya ya akili inapewa kipaumbele. Hakuna mtu anayepaswa kuteseka kimya kimya. Tuzime unyanyapaa. Afya ya akili ya wanaume ni muhimu,” anamalizia.