WASONGA: Shule sharti ziheshimu imani za kidini za wanafunzi
Na CHARLES WASONGA
KIPENGEE 2 (4) cha Katiba ya sasa kinasema kuwa sheria yoyote ambayo ikinakinzana nayo kwa njia yoyote ile ni haramu na haitatambuliwa.
Nacho kipengee 32 (1) kinalinda uhuru wa kuabudu kwa kusema kinaposema: “Kila mtu ana haki ya dhamira, dini, fikra, imani na maoni.”
Ni haki hizi ambazo zimekiukwa wakati wasimamizi wa shule mbili walipoadhibu wanafunzi kutokana na misimamo yao ya kidini.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Kabianga katika Kaunti ya Kericho aliwatuma nyumbani wanafunzi 17 wa kidato cha nne kwa kukataa kufanya mtihani majaribio na badala yake wakaamua kushiriki ibada kwa muhibu wa imani yao.
Na katika Kaunti ya Busia usimamizi wa Shule ya Upili ya St Joseph’s Ganjala mwaka jana ulikuwa umekataa kuwasajili wasichana wa kidato cha kwanza kwa sababu walikataa kunyoa nywele.
Wasichana hao ambao ni waumini wa kanisa la Hour Assembly Ministries, walisema ni kinyume cha imani yao kwa waumini wa kike kunyolewa.
Lakini Mwalimu Mkuu Patrick Simiyu alishikilia kwamba kwa mujibu wa sheria za shule hiyo kuhusu mavazi wanafunzi hawaruhusiwi kuwa na nywele ndefu.
Inakubalika kwamba Sheria ya Elimu ya Msingi ya 2015 inatambua kanuni za shule ambazo hutoa mwongozo kuhusu mienendo hitajika kwa wanafunzi. Kanuni hizo pia hutoa mwongozo kuhusu mavazi ya wanafunzi wakiwa shuleni.
Kilichojiri katika kisa cha Shule ya Upili ya St Joseph Ganjala ni mgongano kati ya sheria ya elimu ya msingi, kanuni za shule na Katiba ya Kenya inayolinda uhuru wa kuabudu na haki ya watoto kupata elimu.
Katika hali kama hii, mwalimu mkuu wa shule hiyo atapatikana na makosa endapo wazazi wa wasichana hao watatu watawasilisha kesi kortini.
Itakumbukwa Januari mwaka jana, tukio kama hili lilitokea katika Shule ya Upili ya Olympic Nairobi, mwanafunzi wa kike wa kidato cha kwanza alipofukuzwa kwa kukataa kunyoa nywele za rasta.
Hii ni licha ya kwamba alipokuwa akisajiliwa shuleni humo, wazazi wake waliwasilisha stakabadhi zilizoonyesha kuwa msichana huyo ni mwanachama wa Muungano wa Rastafarian Nchini (RSK).
Suala hilo lilipofikishwa mahakamani, Jaji Enock Chacha Mwita wa Mahakama Kuu aliamuru kwamba mwanafunzi huyo aruhusiwe kusoma lakini “ahakikishe kuwa rasta zake ni safi na zimefunikwa kila wakati.”
Kwa hivyo, wasimamizi wa shule wanapaswa kuheshimu kanuni za dini na imani za wanafunzi wao kwa sababu zinalindwa na Katiba. Wasitumie sheria za shule kuadhibu wanafunzi kwa misingi ya imani yao.