Makala

Shule za mabweni taabani wanafunzi wakihamia za kutwa

Na STEPHEN ODUOR February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHULE za mabweni katika Kaunti ya Tana River zinakabiliwa na wakati mgumu baada ya idadi ya wanafunzi wanaojiunga au kusomea katika shule hizo kupungua pakubwa, na kuziacha zikikabiliana na mzigo mkubwa wa kifedha.

Shule ya upili ya Galole Model ambayo iliwahi kuwa shule bomba katika kaunti hiyo, inakaribia kufungwa kutokana na uhaba wa wanafunzi.

Shule hiyo iliyokuwa na wanafunzi 500, sasa ina wanafunzi 72, wazazi na walimu wakiuliza maswali kuhusiana na mustakabali wa shule hiyo.

Kwa sasa shule hiyo iliyokuwa mwanga kwa jamii, ilikuwa ikitoa hifadhi na mazingira mazuri kwa wanafunzi kutoka mjini na wale kutoka vijijini ikiwapa elimu ya hali ya juu.

Kwa mujibu wa naibu wa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi Farhiya Mutegi, kupungua kwa idadi ya wanafunzi kumechangiwa na matukio kadhaa yaliyofanyika ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Anahoji kuwa huenda kuondoka kwa wanafunzi hao kunatokana na kampeni inayoendeshwa na Mbunge wa eneobunge hilo.

“Mbunge, kwa hatua iliyoleta sifa na kukashifiwa kwa wakati mmoja, alipinga sana shule za mabweni , akiwataka wazazi kuwahamisha wanao kwa shule za kutwa,” akasema.

Kama sehemu ya kampeni hiyo, mbunge huyo aliahidi kulipa karo kikamilifu kwa familia ambazo zingewahamisha wanao kwa shule za kutwa, ahadi ambayo wazazi wengi hawangepuuza.

Kampeni hiyo ilipeperushwa sana katika redio zinazotamba humo kijijini, na kuchochea kuondoka huko.

“Ilikuwa kampeni iliyowavutia wazazi wengi. Walivutiwa sana na wazo zima la kuahidi masomo ya bure na kuwapa nafasi ya wanao kusomea karibu na nyumbani. Kile hawakufahamu ni kuwa kungekuwa na athari kwa shule kama zetu,” akasema Bi Mutegi.

Shule ya Kitaifa ya wavulana ya Hola, ambayo ilikuwa shule tajika ilipata kuwasajili wanafunzi 300 kutoka idadi yake ya kawaida 700.

Kilomita chache shule ya wasichana ya Mau Mau Memorial, ambayo ni shule tajika kaunti hiyo pia imepoteza zaidi ya wanafunzi 200 kwa shule za kutwa.

“Hali hii inatamausha sana. Tumesalia na idadi Ndogo sana ya wanafunzi na fedha zetu hazitoshi.Kupungua kwa wanafunzi na kuenda shule za kutwa kumetuacha katika hali tete, ambayo hatukuwa tumejipangia,” aksema mwalimu kutoka shule ya wavulana ya Hola ambaye hakutaka kutajwa.

Wazazi pia wamejipata katika njia panda kuhusiana na mabadiliko hayo. Wengine wakisema hatua ya mbunge imewasaidia kuokoa fedha walizokuwa wakilipa kwenye shule za mabweni, wengine wameelezea wasiwasi ya ubora wa masomo.

“Tumeahidiwa kuwa watoto wetu bado watapata elimu bora. Ila ninapata habari za kuwa shule hizo zimejaa wanafunzi kupita kiasi, na ubora wa elimu ni wa kutiliwa shaka. Inanipa wasiwasi,” akahoji mzazi ambaye alimhamisha mwanawe kutoka shule ya upili ya Galole Model.

Mashirika ya kijamii yametaka serikali kupitia wizara ya elimu kuingilia kati na kushughulikia Tatizo hilo la kifedha Pamoja na uongozi wa kaunti hiyo, wakieleza kutoingilia kati kutachangia shule kadhaa kufungwa.

Mwenyekiti wa shirika la Civil Society Network Bw John Dhadho ametaka wazazi, jamii na viongozi kuokoa shule hizo.

“Tunataka motto wa Tana River aendelee kupata elimu. Ila kunapaswa kuwa na uongozi ambao hautachochea kupunguza idadi ya wanafunzi, ila kuongeza idadi ya wanafunzi na kutimiza wajibu wa shule hizo. Tusipochukua hatua tutapoteza shule hizo kabisa,” akasema Bw Dhadho.