Makala

Si kila kipindi cha watoto kwenye runinga ni kizuri

Na BENSON MATHEKA July 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Wazazi wana mitazamo tofauti kuhusu watoto wao wadogo na utazamaji wa runinga. Huku baadhi ya wazazi wakikosa kuruhusu kabisa watoto wao kutazama runinga wakiwa na umri mdogo, wengine huwaruhusu watoto wao kutazama vipindi maalum mradi tu vinafunza maadili au vina thamani ya kielimu.

Hii si makala ya kuamua iwapo mtoto wako anapaswa kutazama runinga au la – huo ni uamuzi wa kibinafsi unaotegemea familia husika.

Kwa wazazi wanaoruhusu watoto wao kutazama runinga, makala hii inalenga kuwasaidia kuhakikisha wanapata manufaa ya kweli kutokana na kile watoto wao wanachotazama.

Vipindi vya watoto vinavyolenga elimu mara nyingi huishia kufaidi mtoto kuhusu maisha – kama vile kuwa na nidhamu, kuishi kwa amani na familia, au kuwatendea mema marafiki. Hii ndio sababu vipindi hivi huvutia sana wazazi wengi.

Hata hivyo, watoto wanaweza kushushuhudia migogoro au tabia hasi miongoni mwa wahusika.

Ili mtoto aelewe somo kuu la hadithi ya runinga, anahitaji kuwa na uwezo wa kufikiri kwa undani – kuunganisha mwanzo, kati na mwisho wa simulizi, kuelewa sababu ya changamoto na matokeo yake, na kwa nini tabia njema ni chaguo bora.

Tatizo ni kuwa uwezo huu wa kufikiri bado huwa unaendelea kukua kwa watoto. Hii inamaanisha kuwa, licha ya kujifunza maadili mazuri, kuna uwezekano pia wanaiga baadhi ya tabia hasi wanazoona kabla ya kupata ujumbe chanya.

Katika utafiti uliochapishwa hivi karibuni kwenye Journal of Applied Developmental Psychology,watafiti waligundua kuwa vipindi vya kielimu kwa watoto vinaweza kwa bahati mbaya kufundisha baadhi ya tabia mbaya pia.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Iowa State na Chuo Kikuu cha Buffalo, New York, waliwachunguza watoto wa chekechea darasani na kwenye uwanja wa michezo katika vituo tofauti vya kulelea watoto. Walikusanya pia taarifa kutoka kwa walimu na wazazi.

Waligundua kuwa watoto waliotazama vipindi vya kielimu walionyesha tabia za “unyanyasaji wa uhusiano” kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na wale wasiovitazama. Huu si unyanyasaji wa kimwili, bali ni ule wa kihisia kama vile kusema: Wewe si rafiki yangu tena au “Hutakaribishwa kwenye sherehe yangu ya kuzaliwa.”

Ingawa lengo la vipindi hivi ni kufundisha watoto jinsi ya kutatua migogoro ya uhusiano, si watoto wote wanaweza kutofautisha kati ya somo linalofundishwa na tabia wanayopaswa kuiga.

Kabla hujapiga marufuku kabisa vipindi vya watoto, kuna hatua kadhaa za kuchukua

Weka muda wa kutazama

Hakikisha mtoto anapata muda wa kucheza, kutangamana na marafiki au familia, na kushiriki mazoezi.  Shughuli hizi mara nyingi hufundisha mambo muhimu zaidi ya yale yanayoonyeshwa kwenye runinga.

Chagua kwa makini

Angalia kwa makini maudhui ya vipindi anavyotazama mtoto wako. Si kila kipindi cha watoto kinafaa.

Tazama mamoja na mtoto

Kuwa sehemu ya utazamaji. Zungumza naye kuhusu anachoona.Mweleze ni kwa nini tabia hasi katika kipindi haikuwa sahihi na jinsi ilivyomwathiri mhusika mwingine. Vilevile, muonyeshe matokeo mazuri ya tabia njema.