Makala

SIAYA: Matumaini tele kwa wakazi baada ya dhahabu kupatikana kijijini

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 3

Na VALENTINE OBARA

KWA miongo mingi, wakazi katika kijiji cha Onyata kilicho eneobunge la Rarieda katika Kaunti ya Siaya, wamekuwa wakiamshwa kwa sauti tamu za ndege alfajiri kuenda kushughulikia mashamba yao madogo.

Lakini hali hii imebadilika kwa miezi mitatu sasa kwani wanakijiji hao wamekuwa wakiamshwa kwa sauti za mashine za kusaga mawe na badala ya kuenda shambani, wengi wao huelekea moja kwa moja hadi katika eneo ambako uchimbaji wa dhahabu unaendelea.

Kwa siku nzima, makumi ya wanaume kwa wanawake hufanya shughuli tofauti kama vile uchimbaji wa mawe kutoka kwa mashimo yaliyochimbwa kwenye ardhi, usagaji wa mawe na usafishaji wakitumai kupata madini ya dhahabu ambayo wao huyaita ‘pesa’.

Wanakijiji walieleza Taifa Leo kwamba gramu moja ya madini hayo huuzwa kwa Sh3,000 au zaidi hasa kwa madalali.Bw Fredrick Were, mmoja wa wanakijiji, asema shimo ambamo dhahabu huchimbwa limekuwepo kijijini humo tangu miaka ya 1930 lakini halikuwa likitumiwa hadi katikati ya mwaka huu wakati Wakenya wanaofanya biashara ya kutafuta madini kutoka Kusini mwa Nyanza walipotua katika kijiji hicho kutafuta dhahabu.

“Walikuwa wanazurura tu wakitafuta mahali ambapo kuna madini ya dhahabu. Walipowasili hapa walikuta shimo lililochimbwa na Wazungu ambao waliondoka mwaka wa 1936. Walipogundua kwamba Wazungu walikuwa wameshughulika hapa, walianza kuondoa taka zilizokuwa zimeziba shimo hilo na baada ya miezi mitatu au minne hivi, walifikia mawe yaliyokuwa na dhahabu,” akasema.

Ingawa uchimbaji dhahabu si jambo geni katika eneo hili la Asembo, shughuli hii ilikuwa imesitishwa kwa miongo mingi isipokuwa katika sehemu chache ambapo watu binafsi hutafuta dhahabu kwenye maziwa madogo.

“Nimekuwa nikifanya kazi hii kwa miaka mingi lakini umepita muda mrefu tangu niwe katika eneo hili. Nimeifanya tangu mwaka wa 1972. Nilikuwa nikiifanya Nyanza Kusini, Kakamega na sasa niko Asembo. Kwa sasa biashara imenoga,” Bi Milka Akinyi akasema kwa furaha huku macho yake yakitazama tu chombo cha kuchuja mawe yaliyosagwa ambacho kimetengenezwa kwa mbao na vipande vya magunia.

Ni katika mchujo huu ambapo Bi Akinyi na wengine huondoa uchafu kwenye mawe yaliyosagwa yakageuka poda, na baadaye kutumia kemikali ya zebaki kutenganisha dhahabu na uchafu uliosalia.

“Mawe yaliyosagwa huletwa kwenye chombo hiki na mimi huchuja. Dhahabu hubaki kwenye kichungi kisha sisi hukamua gunia hadi mchanga wote ambao umechanganyika na dhahabu huondolewa, na kutia zebaki kututolea pesa yetu. Tunafahamu vyema pesa inavyokaa kwa kutazama tu kwa macho makavu,” akasema.Shughuli hizi zimebadilisha kwa kasi sura ya kijiji cha Onyata kwani sasa kinafanana na soko linalokua ilhali awali sehemu nyingi zilikuwa na vichaka.

Wafanyabiashara wamejenga vibanda ambapo kuna wauzaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mavazi na vyakula, mbali na huduma za kutoa na kupokea pesa kwa njia ya simu.Zaidi ya haya, shughuli hizi za uchimbaji wa dhahabu zimeanza pia kuvutia watalii hasa katika msimu huu wa sherehe za Krismasi ambapo wakazi wengi wa mijini huwa wameelekea mashambani.

Licha ya haya, kumekuwepo mivutano kati ya wanakijiji na watu wanaosemekana kutoka kaunti za nje.Tulipozuru eneo hilo, hatukufanikiwa kushuhudia jinsi mawe yanavyochimbwa kwani maafisa wa utawala waliamua kusitisha shughuli hiyo na kufunga kiingilio cha machimbo yaliyo chini ya ardhi baada ya mzozo kuibuka siku iliyotangulia kuhusu watu walio na haki ya kuingia shimoni.

Bw Were asema uchimbaji huu umevutia watu kutoka Tanzania na Kusini mwa Nyanza ambako uchimbaji aina hii hufanywa kwa kiwango kikubwa hasa katika Kaunti ya Migori na viungani mwake.

Afisa wa utawala aliyeomba asitajwe jina kwa kuhofia kuadhibiwa, alisema kuna makubaliano kati ya wanakijiji na wasimamizi wa uchimbaji huo ambao wanasemekana kuongozwa na mwekezaji aliye na sehemu nyingine za uchimbaji maeneo ya Magharibi na Nyanza.

Kwa sasa, mikutano huandaliwa mara kwa mara kwa nia ya kutuliza uhasama kati ya wadau huku maafisa wa utawala wakijitahidi kuhakikisha shughuli hizo zinaendelezwa kisheria na pia kuzuia mizozo ambayo inaweza kufanya baraka hii kugeuka kuwa karaha.