Sifa zinazomfanya Uhuru kusalia kipenzi cha wengi Mlima Kenya
NA WANDERI KAMAU
MIONGONI mwa jamii ya Agikuyu, mtu hakuchaguliwa vivi hivi tu kuwa kiongozi wa jamii.
Kulingana na wazee, kulikuwa na vigezo kadhaa ambavyo vilikuwa vikizingatiwa kabla ya mtu kukwezwa kuwa kiongozi au msemaji wa jamii hiyo.
Nguzo hizo zilikuwa tatu; kwanza, lazima mtu huyo awe tajiri, maarufu na shujaa.
Mjadala huo umezuka kufuatia juhudi zinazoendelea katika ukanda wa Mlima Kenya kuhusu ni nani anayefaa kuwa kiongozi wa kisiasa na msemaji rasmi wa ukanda huo.
Kwa baadhi ya watu, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ndiye anayefaa zaidi, wakisema ana sifa tatu kuu ambazo mtu alihitajika awe nazo ili kutawazwa kuwa kiongozi wa jamii ya Agikuyu.
Kulingana na Mzee Njui Wanjui, Bw Kenyatta ni mtu tajiri, ikizingatiwa kuwa anatoka kwenye familia chache nchini zinazokisiwa kudhibiti uchumi wa taifa hili.
“Babake Uhuru, Mzee Jomo Kenyatta, aliweka msingi mzuri wa kiuchumi, kibiashara na kimapato kwa familia yake. Alifahamu kuwa kama kiongozi, watu humwangalia kiongozi wao kusuluhisha changamoto zinazowakumba wanapojipata kwenye mgogoro wa kimaisha. Hivyo, si vizuri kiongozi kuwa katika hali ambapo hawezi kuwasaidia watu wake wanapokumbwa na changamoto,” akasema Mzee Njui.
Anasema kuwa hilo ndilo limemfanya Bw Kenyatta kuwa katika hali nzuri kupigania au kuendelea kushikilia nafasi ya msemaji mkuu wa eneo la Mlima Kenya, kwani “hata juhudi za kuwarai watu kumuunga mkono zinahitaji fedha”.
“Ni wazi kuwa mkono mtupu haulambwi. Miongoni mwa Wakikuyu, lilikuwa jukumu la mfalme kuwachinjia na kuwashibisha wageni wake. Hilo ndilo lililompa ukubalifu na hekima miongoni mwao. Si mara moja tumemwona Bw Kenyatta akifanya hivyo, kwa mfano kupitia vikao tofauti vya Chama cha Jubilee,” akasema.
Mwanahistoria Wilson Nderitu, pia anasema Bw Kenyatta amedhihirisha sifa yake kama shujaa.
Anasema kuwa ushujaa wake ulidhihirika alipokuwa na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), jijini The Hague, Uholanzi.
“Hizo zilikuwa nyakati ngumu sana kwa Bw Kenyatta kama Rais wa Kenya na kiongozi wa kisiasa wa jamii hii. Ikiwa hangekuwa mtu mwenye ushujaa, basi hangewania urais mnamo 2013 kutokana na shtuma alizokuwa akipata kutoka kwa mataifa ya Magharibi, kama vile Amerika na Uingereza. Hata hivyo, aliamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho bila kuogopa lolote,” akasema mwanahistoria huyo.
Wadadisi wanasema kuwa Bw Kenyatta pia ni mtu mwenye sifa; anayejulikana kote kote, kutokana na msingi wa kisiasa uliowekwa na Mzee Kenyatta.
Ikizingatiwa bado ana uwezo huo licha ya kustaafu kama Rais, wadadisi wanasema ni rahisi sana kwake kuendelea kushikilia nafasi hiyo.