SIHA NA ULIMBWENDE: Matumizi mbalimbali ya mshubiri
Na MARGARET MAINA
Huzuia na kuondoa michirizi ya tumbo itokanayo na ujauzito
ANZA kwa kupaka majimaji ya Aloe vera yaani mshubiri juu ya tumbo lako na ufanye kama unamasaji taratibu juu ya tumbo mara mbili kwa siku katika kipindi chote cha ujauzito na baada ya kujifungua kwa miezi michache mpaka michirizi ipotee.
Hutumika kutibu matatizo ya tumbo
Ukiinywa juisi ya mshubiri, hutibu vidonda vya tumbo na kiungulia. Pia husafisha mfumo wote wa mmeng’enyo wa chakula. Chukua jeli ya Aloe vera kiasi cha nusu kikombe changanya na maji nusu kikombe halafu kunywa mara mbili kwa siku.
Huimarisha kucha dhaifu
Paka majimaji ya Aloe vera juu ya kucha zako sehemu zote juu na chini kila siku na kisha uzitazame baada ya siku kadhaa uone zitakavyokuwa zimerudisha ule uzuri na ugumu wake wa mwanzo au zamani.
Huondoa vipodozi
Kwa usalama kabisa huondoa makeup kwenye jicho na ni nzuri kwa ngozi laini inayozunguka jicho lako.
Husafisha ngozi na kuondoa alama zitokanazo na kuungulika juani
Chunusi na kuungua kwa ngozi kutokana na jua vyote hivi vinatibika kirahisi kwa kutumia mshubiri. Paka mara mbili kwa siku katika ngozi mpaka uone umepona kabisa.
Huondoa makunyanzi na mikunjo ya ngozi
Ngozi hupenda sana Vitamini C na E ambazo zote zinapatikana katika Aloe vera na kusaidia kuiacha katika hali ya unyevuunyevu. Ikiwa utachanganya jeli ya Aloe vera na mafuta ya asili ya nazi, utapata krimu nzuri ya kuongezea mafuta muhimu na unyevunyevu katika ngozi.
Jeli ya Aloe vera hupenyeza katika ngozi kwa haraka na sifa yake ya kulainisha ngozi husaidia ngozi kubaki na unyevunyevu.
Hukabiliana na mafua
Jeli ya Aloe vera huongeza kinga ya mwili. Ina Vitamini A, B, C, na E. Mmea huu una orodha ndefu ya madini muhimu kwa mwili.
Huongeza nguvu mwilini
Matumizi mengine ya kitabibu ya mshubiri ni kuongeza usawa wa nguvu mwilini. Hii ni kutokana na uwepo wa vitamini B14.
Huondoa mba kichwani
Changanya jeli ya asili ya Aloe vera na shampoo yako. Dakika chache kabla ya kwenda kulala, paka vizuri mchanganyiko huo kwenye nywele zako na uache zikauke kidogo. Safisha nywele zako asubuhi.
Hutibu chunusi
Aloe vera huondoa chunusi kwa kuziondoa seli zilizokufa katika ngozi na hivyo kuvifungua vinyweleo katika ngozi na kuondoa mafuta yaliyoganda katika hivyo vishimo.
Paka jeli ya aloe vera katika eneo lililoathirika na chunusi. Pia makovu yaliyoachwa kutokana na chunusi yanaweza kuondolewa kwa kupaka jeli ya Aloe vera pekee.