SIHA NA LISHE: Cha kufanya ili uwe na 'umbo dogo' na vilevile kupunguza uzani
Na MARGARET MAINA
WATU wengi wanatamani kuwa na umbo dogo.
Unachotakiwa kujua ni kwamba kikubwa unachotakiwa kuzingatia ni mazoezi na ulaji wako; kwa kuwa mwangalifu katika kiasi cha kalori unachoingiza mwilini kila siku.
Unatakiwa kuwa mwadilifu katika uchaguaji wako wa chakula; haimaanishi ukae hivyo ukiwa na njaa.
Kinachosisitizwa katika mpango huu ni kuwa waangalifu katika upangiliaji wa vyakula.
Aina hii ya mpangilio wa ulaji inafahamika zaidi kitaalamu kama ‘crash diet’.
Kula kiasi cha kalori 400- 500 kwa siku. Ingawa hivyo, unatakiwa kufanya mazoezi angalau kwa saa mbili kwa siku ili kupunguza mara mbili ya kiasi cha mafuta uliyokula katika siku hiyo.
Kunywa maji kwa wingi. Kwa kunywa kiasi kikubwa cha maji, itakusaidia kurahisisha umeng’enyaji wa chakula mwilini. Ni vyema mwili wako ukawa na maji ya kutosha ikiwa umeingia kwenye mpango huu wa ulaji Kula mboga za kijani: Zina Vitamini, protini na virutubisho vingine kwa wingi ambavyo ni muhimu kwa afya. Kama nilivyoainisha awali, utaratibu huu hauhamasishi kukaa na njaa, bali kula vyakula vilivyo bora kiafya.
Kula vyakula visivyokobolewa. Mara nyingi vyakula vya aina hii, huwa na virutubisho muhimu na vinavyohitajika katika ustawi wa mwili.
Punguza wanga katika mlo wako. Badala yake, unaweza kula protini na kuingiza vyakula kama mayai na samaki kwenye mlo wako.
Epuka kula vyakula vya mtaani. Vyakula kama chipsi, mihogo ya kukaanga – na jamii yake – vinachangia kwa kiasi kikubwa mtu kuongeza uzani wa mwili na pia kutia hitilafu katika umeng’enywaji wa chakula tumboni kwa kuufanya kuwa mgumu.
Kunywa supu za mbogamboga. Supu kama ya kabichi licha ya kujaza tumbo, husaidia katika kurahisisha mfumo wa umeng’enyaji chakula tumboni.
Kula saladi na matunda kwa wingi. Hii itasaidia kukuweka sawa kiafya.
Jizuie kula vyakula vyenye sukari nyingi na hata vile vya mtaani unavyohisi vinaweza kukwamisha mpango wako wa kupunguza uzani.
Lakini pamoja na yote haya, jipe mazoezi ya kutosha kama kukimbia au kuruka kamba. Je, unakumbuka ule mchezo wa ‘Public Van‘?