SIHA NA LISHE: Faida ya kula mapera
Na MARGARET MAINA
MAPERA ni matunda baadhi ya watu husema yana ugumu wakiyala.
Hata hivyo, yakishaiva huwa laini. Muhimu ni kwamba huwa yana nyama na mbegu mbegu nyingi.
Matunda haya yana faida kubwa sana kwa afya ya mwili wa mwanadamu jinsi ifuatavyo: –
Yana vitamini C
Mapera yana ukwasi mkubwa wa Vitamini C ambayo ni muhimu sana katika mwili wa mwanadamu.
Ni kinga nzuri ya kisukari
Ulaji mbaya wa watu wengi unawaweka katika hatari ya kuugua kisukari.
Mapera yatakupunguzia hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari.
Hii ni kwa sababu mapera yana utajiri mkubwa sana wa nyuzinyuzi (fibre), ambayo ni muhimu sana katika kupunguza kiasi cha sukari kwenye damu.
Kuimarisha uwezo wa kuona
Mapera yana utajiri mkubwa sana wa vitamini A au Retinol ambayo ni muhimu sana katika kusaidia kuona vizuri. Hivyo basi kama ilivyo kwa karoti, mapera yanasaidia katika kuongeza na kuimarisha uwezo wa mtu kuona.
Kurekebisha kiwango cha shinikizo la damu
Madini ya Potassiumu yaliyomo ndani ya mapera yanasaidia katika kurekebisha shinikizo la damu (Blood Pressure).
Yana madini ya shaba
Mapera yana madini ya shaba (Trace element copper ) ambayo ni mazuri sana katika ufanyaji kazi wa thyroid.
Tezi za thyroid zisipofanya kazi vizuri zinaweza kusababisha matatizo mengi ya kiafya kwa mwanadamu.
Yana madini ya manganese
Mapera yana utajiri mkubwa wa madini ya manganese ambayo yanausaidia mwili katika kunyonya ama kupata virutubisho muhimu kutoka kwenye vyakula tunavyo kula.
Mapera ni muhimu katika afya ya akili ya mwanadamu
Vitamini B3, Vitamini B6 ambazo zinapatikana ndani ya tunda la mpera ni muhimu katika kuimarisha afya ya akili ya mwanadamu. Mapera yatasaidia kuufanya ubongo wako utulie.
Ni muhimu sana katika ngozi ya mwanadamu
Vitamini C, viondoa sumu na karotini ambazo zinapatikana ndani ya tunda la mpera ni muhimu sana katika kuimarisha afya ya ngozi.