SIHA NA LISHE: Faida za maji ya madafu
Na MISHI GONGO
MAJI ya madafu ni maarufu sana miongoni mwa wenyeji katika eneo la Pwani ya Kenya.
Dafu (ngeli ya li-ya) ni nazi changa ambayo haijakomaa.
Pamoja na kutumika kama kinywaji kwa ajili ya kuondoa kiu, maji ya madafu yanaaminika kuwa na faida kede kede kwa mwili wa binadamu.
Ili kuimarisha kinga ya mwili na kupata manufaa mengine, wataalamu wa tiba na dawa asilia huagiza watu kutumia maji ya madafu kwa wingi.
Miongoni mwa faida zake ni kuzuia upungufu wa maji mwilini na kuimarisha ubongo na misuli.
Faida zingine ni kusaidia kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa kiharusi, kurekebisha kiwango cha sukari katika mwili na kusaidia kurekebisha ngozi na kuponya makovu.
Aidha husaidia kuua bakteria wa aina mbalimbali wakiwamo wale wanaosababisha maambukizi kwenye njia ya mkojo – UTI – kutokana na virutubisho vilivyoko ndani ya maji ya tunda hilo.
Pia linasemekana kusaidia kupunguza tatizo la msukumo mkubwa wa damu mwilini.
Wataalamu wa lishe wanashauri maji hayo yanywewe asubuhi kabla ya mtu kutumia chakula au kinywaji chochote.
Kwa watu wanene, huwasaidia kupunguza uzani uliopitiliza na kuwaongezea hamu ya kula kutokana na uasilia wake.