• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:46 PM
SIHA NA LISHE: Namna ya kuondoa asidi inayosababisha kiungulia kwenye maharagwe na tumbo kujaa gesi

SIHA NA LISHE: Namna ya kuondoa asidi inayosababisha kiungulia kwenye maharagwe na tumbo kujaa gesi

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MAHARAGWE yasipoandaliwa vizuri yanaweza yakakusababishia kiungulia kwa muda mrefu na wakati mwingine tumbo hujaa gesi na kukunyima raha.

Maharagwe ni chanzo kizuri cha protini B na nyuzinyuzi. Asidi aina ya Phytic ipatikanayo kwenye maharagwe ikutanapo na madini ya mwili kama zinc, copper, calcium, magnesium na madini chuma husababisha tatizo la kiungulia na tumbo kujaa gesi kwa baadhi ya watu.

Tatizo hili huwasumbua zaidi wale wasiokula nyama na vyakula vitokanavyo na wanyama kwani vyakula vyao hua na asidi nyingi ya phytic.

Ingawa huwezi ukatoa asidi yote ya phytic kwenye maharagwe, unaweza kuipunguza kwa kiasi kikubwa kwa kuloweka maharagwe kwenye maji.

Wengi mnaloweka maharagwe kwenye maji ili kuyalainisha na kufanya yaive haraka wakati wa kupika, lakini msichojua ni kwamba kuloweka huko hupunguza asidi ya hyptic kwenye maharagwe ambayo ni chanzo cha kiungulia kwa wengi.

Asidi hiyo pia hutonesha vidonda vya tumbo na kuleta maumivu makali kwa wale wenye tatizo la vidonda vya tumbo.

Watu wengi wamezoea kuloweka maharagwe usiku na kuyapika siku inayofatia. Ingawa kuloweka huku kumezoeleka kwa wengi, tafiti zinaonyesha kwamba njia hii ya ulowekaji wa maharagwe ni hatari sana kwa afya kwani hutoa nafasi, mazingira mwafaka na muda mrefu kwa vijidudu viletavyo magonjwa vipatikanavyo kwenye maharagwe kuzaliana na kukua.

Ingawa maharagwe hupikwa kwa muda mrefu na kwa moto mkali bado haitoshi kuua vijidudu vya aina yote. Bakteria watengenezao sumu mara nyingi hubakia hai na huweza kuwa chanzo cha magonjwa kwa mlaji wa maharagwe hayo.

Ukiamua kutumia njia hii, basi loweka maharagwe na uyaweke ndani ya jokofu ili kupunguza uwezekano wa vijidudu hao kuzaliana kwenye maharagwe.

Kuloweka maharagwe kwa muda mfupi ni njia nzuri na bora zaidi ya kupunguza asidi ya phytic kwani huipunguza kwa kiwango kikubwa na kwa haraka zaidi kuliko njia ya kuyaloweka kwa muda mrefu.

Njia hii fupi kwa upande mwingine haitoi nafasi ya vijidudu viletavyo magonjwa kuzaliana kwenye maharagwe; na huokoa muda kwani huchukua muda mfupi.

Ulowekaji huu huchukua kati ya saa moja hadi saa nne na si zaidi. Ni juu ya mpishi kuchagua aloweke kwa muda wa saa ngapi.

Hata hivyo, ni vyema kujua kwamba ukiloweka kwa muda wa saa nne utatoa kiasi kikubwa cha phytic kuliko ukiloweka kwa muda wa saa moja.

  • pima kiasi cha maharagwe unachotaka kuandaa/kupika
  • chambua maharagwe ili kuondoa mabovu, mawe na uchafu mwingine wowote
  • osha maharagwe
  • kwa kutumia kikombe ulichopimia maharagwe, pima maji mara mbili ya kipimo cha maharagwe na uweke kando
  • katika sufuria, weka maharagwe na kisha ongeza maji uliyopima
  • bandika sufuria yenye maharagwe mekoni yachemke kwa dakika mbili tu (hesabu dakika mbili kuanzia pale yanapoanza kutokota na sio dakika mbili kuanzia ulipoyabandika mekoni.
  • epua baada ya dakika hizo kuisha
  • acha kwa kati ya saa moja hadi muda wa saa nne (kutegemea muda ulio nao)
  • chuja maji yote kwenye maharagwe.
  • maji yaliyochujwa kwenye maharage huwa yamebeba phytic
  • weka maharagwe kwenye sufuria, ongeza maji, bandika mekoni kisha chemsha hadi maharagwe yaive.
  • baada ya kuivisha maharagwe, unaweza kuyapika au kuyaunga kwa namna upendayo.

You can share this post!

Jinsi ya kuhifadhi mboga na matunda katika jokofu

WAJIR: Kutoaminiana baina ya vikosi vya usalama na wakazi...

adminleo