Makala

SIHA NA LISHE: Zabibu na umuhimu wake mwilini

December 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MARGARET MAINA

[email protected]

ZABIBU ni matunda matamu na yana faida nyingi kiafya kwa mwili.

Kuna zabibu za rangi ya kijani, nyekundu na nyeusi.

Unaweza kula zabibu kama matunda, zabibu zilizokaushwa au kama juisi ya zabibu. Zabibu hutumika sana kutengeneza mvinyo (wine) sehemu mbalimbali duniani.

Faida za zabibu kiafya hujumuisha kusaidia kuondoa kukosa choo yaani mmeng’enyo wa chakula kwenda vizuri, kupunguza uchovu na kadhalika.

Virutubisho vilivyo ndani ya Zabibu ni Nishati, Wanga, Sukari, Kambakamba, Mafuta, Protini, Vitamini B1, B2, B3, B5, B6, B9,C, E na K, Madini, Kalsiamu, Chuma, Magnesium, Manganese, Sodiamu, Potasiamu, na Fosforasi.

Faida za zabibu kiafya

Zinatumika kutibu pumu.

Zabibu zinasaidia kuongeza unyevunyevu kwenye njia ya hewa na hivyo kupunguza utokeaji wa pumu.

Huimarisha mifupa

Madini ya shaba, chuma na manganizi yanapatikana kwa wingi kwenye zabibu, na madini haya ni sehemu ya kujenga mifupa imara na yenye afya. Kula zabibu mara kwa mara inasaidia kupunguza kutokea kwa mifupa kulainika kutokana na umri kuwa mkubwa. Pamoja na kuimarisha mifupa, madini haya husaidia mwili kufanya kazi vizuri.

Hulinda dhidi ya magonjwa ya moyo

Zabibu huongeza nitric oxide kwenye damu ambayo huzuia damu kuganda, husaidia kuzuia mafuta kulundikana kwenye mishipa ya damu na ina kampaundi za flavonoids ambazo husaidia kutoa sumu mwilini. Haya yote husaidia kupunguza hatari ya magonjwa moyo na shinikizo la damu.

Kusafisha figo

Zabibu zina viondoa sumu ambazo husaidia kuondoa sumu kutoka kwenye figo. Pia hupunguza tindikali ya uric kwa kuongeza kiasi cha mkojo unaotengenezwa na figo.

Kupunguza lehemu

Zabibu zina uwezo wa kupunguza lehemu kwenye damu. Zina kampaundi ambazo zinadhaniwa kupunguza mafuta ya lehemu kwenye damu. Pia aina ya kampaundi iliyo kwenye ngozi ya zabibu ziitwazo saponins hupunguza unywonyaji wa lehemu kutoka kwenye utumbo.