Makala

Siku 18 za masaibu ya mbunge wa Mosop kutokana na dawa zisizofanya kazi

Na FRIDAH OKACHI December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 4

MBUNGE wa Mosop Abraham Kirwa amesimulia masaibu ya kutisha ya kiafya ambayo nusura yamuue baada ya kudai kuwa alipewa dawa za moyo zisizo na ufanisi kwa siku 18 katika hospitali moja nchini, na hata kukataliwa kupewa huduma ya dharura licha ya kuonyesha dalili za wazi za mshtuko wa moyo.

Akizungumza baada ya kurejea nchini wiki mbili zilizopita baada ya kutafuta matibabu ya miezi kumi na tano nje ya nchi, mbunge huyo alisema kilichoanza kama siku ya kawaida Agosti 3, 2024, kiligeuka kuwa janga la kiafya lisilotarajiwa.

Bw Kirwa alikuwa amemwendea kumchukua mkewe kwenye uwanja wa ndege ili kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, kisha kuelekea kwenye kipindi chake cha kawaida cha redio cha Jumamosi. Hata hivyo, alianza kutoona vizuri na kupatwa na maumivu makali yaliyopelekea kukimbizwa hospitalini mara moja.

“Nilimwitisha mke wangu maji, lakini sikuweza hata kumwona aliposimama. Nilijua kuna tatizo,” alisimulia.

Alikimbizwa hospitalini, ambapo mkewe mwenye kuelewa taratibu za kitabibu za Marekani aliwasihi madaktari wampatie TPA (dawa ya kukabiliana na maradhi ya moyo yanayohusisha damu) inayotumika kote duniani ili kuzuia mshtuko wa moyo au kiharusi ikiwa mgonjwa atapewa ndani ya saa nne.

Kwa mujibu wake, daktari aliyekuwa zamu alikataa, hata baada ya daktari wa familia kusisitiza atibiwe. Badala yake, anasema waliambiwa waende nyumbani baada ya saa kadhaa.

“Tulikaa hadi saa nane mchana. Wakaniambia nirudi nyumbani saa nane. Mke wangu akawauliza, “Nitampeleka aje nyumbani na hajawahi kuugua hivi?” alihoji.

Mbunge huyo alisihi kufanyiwa kipimo cha damu. Matokeo ya vipimo yakionyesha kuwa na viwango vya juu hatari vya ‘enzymes’ zinazoashiria uharibifu wa moyo ndipo hospitali ikaidhinisha kumpelekwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Bw Kirwa alilazwa kwa siku 18, akipokea tiba na dawa alizodhani zinamsaidia. Badala yake, hali yake ilizidi kuwa mbaya.

“Daktari aliyekuwa akifuatilia uwezo wa moyo wangu aliona unazidi kushuka kutoka asilimia 25, 23, 18 hadi chini ya 15, kiwango cha kuhatarisha maisha. Moyo wangu ulikuwa unaelekea kukosa kufanya kazi tena. Mke wangu aliambiwa ukishuka chini ya 15, naweza kufa na kuomba idhini ya kusafirishwa nje ya nchi,” aliongeza Bw Kirwa.

Licha ya maombi yao, hospitali hiyo inadaiwa kukataa kuwasaidia kupata ruhusa ya matibabu nje ya nchi kwa muda ufaao.

Hatimaye waliandaa ndege ya dharura binafsi kuelekea Dubai japo wakakawia.

Kwa mshangao, Bw Kirwa anasema hospitali hiyo ilichelewesha kumruhusu kuondoka alfajiri, jambo lililokaribia kuvuruga safari ya uokoaji.

“Ingebidi niondoke kwa ndege ya dharura; lakini mpango wangu wa kuondoka ulicheleweshwa sana. Nilidhani naondoka alfajiri, ila nikaruhusiwa usiku wa manane.”

Alipowasili Dubai, madaktari waliamua kusitisha dawa zote alizokuwa amepewa Nairobi.

“Lakini nilipofika Dubai, dawa zile zile zikaanza kufanya kazi. Niliweza kutembea. Moyo wangu ukaanza kupanda kutoka asilimia 18, 20, 25 hadi 30,” alisimulia.

Alipohoji kwa nini dawa hizo zilifanya kazi Dubai lakini zikashindwa Nairobi, madaktari walimjibu kwa urahisi:

“Tunakuwekea dawa halisi,” alimjibu daktari wake wa Dubai.

Walimwonya kuwa dawa nyingi zinazoingia Kenya huenda ni bandia au duni, zikitengenezwa upya na kufungashwa upya kabla ya kuuzwa.

Bw Kirwa aliendelea kutafuta matibabu katika nchi ya Marekani, ambapo madaktari pia walitupa dawa alizokuwa amebeba kutoka nchini Kenya na kumpa zile zile kutoka Dubai. Hali yake ikaimarika na kurudi katika kiwango cha kawaida cha hadi 50% kupitia dawa sahihi na mazoezi ya moyo.

Mbunge huyo sasa anashangaa ni Wakenya wangapi waanaopoteza maisha kutokana na utambuzi mbaya, dawa bandia au uzembe.

“Nilikaribia kufa. Kama ningerejea nyumbani kama walivyotuambia mwanzoni, ningekufa njiani,” alisema Bw Kirwa.

Pia anashangaa mbona akanyimwa TPA, dawa ambayo ingeweza kuzuia mshtuko wa moyo papo hapo na kumwondolea miezi 15 ya mateso.

Kirwa anasema atawasilisha malalamiko rasmi kwa Bodi ya Dawa na Sumu.

“Lazima tuwawajibishe madaktari na wanafamasia. Rais amejitahidi, lakini watu ndani ya mfumo wanawaangusha Wakenya,” alionya.

Amesisitiza kuwa ana wasiwasi zaidi kwa Wakenya wa kawaida wasioweza kumudu matibabu Dubai au Marekani.

“Wangapi wamekufa kwa kuamini dawa ambazo si halisi? Inakuwaje kwa wale wasioweza kusafiri nje kama mimi?”

Rais wa Chama cha Wanafamasia Kenya, Dkt Wairimu Mbogo, amemtaka mbunge huyo kuwasilisha ripoti rasmi inayoeleza dawa alizopewa, akisema taarifa hiyo ni muhimu kwa uchunguzi wa kitaalamu. Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda umma, kwani ikiwa dawa hizo zina matatizo, huenda wagonjwa wengine wengi nchini pia wameathirika.

Chama cha Wanafamasia Kenya kimesema bado hakijapokea malalamiko yoyote rasmi na kimeeleza kuwa hospitali inayodaiwa ni taasisi yenye sifa nzuri.

“Hatuezi kuchunguza kisichoripotiwa. Ikiwa mheshimiwa anaamini alipokea dawa duni, lazima awasilishe malalamiko rasmi. Kenya ina mifumo na mifumo hiyo hufanya kazi tu watu wanapoitumia,” alisema Dkt Wairimu.

Katibu wa Huduma za Matibabu, katika Wizara ya Afya Dkt Ouma Oluga, amesema Kenya inaelekea kwenye mfumo wa kidijitali wa ufuatiliaji wa dawa, ambao utawezesha dawa kufuatiliwa kutoka zinapotengenezwa hadi kwa mgonjwa, hatua ambayo inalenga kuzuia matatizo ya baadaye.

“Wakati mwingine kunaweza kuwa na makosa ya utengenezaji, hata kutoka kwa kampuni halisi. Ndiyo maana ufuatiliaji wa dawa baada ya kuingia sokoni ni muhimu kuhakikisha kila dawa inayofika kwa Wakenya ni salama na yenye ufanisi.”

Dkt Oluga amesema uchunguzi ulianzishwa zaidi ya wiki mbili zilizopita baada ya mbunge huyo kutoa madai. Alisema tayari wamekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Dawa na Sumu pamoja na Maabara ya Kitaifa ya Kudhibiti Ubora wa Dawa, taasisi zilizo na mamlaka ya kufanya uchunguzi, na sampuli za dawa husika tayari zimekusanywa kwa uchunguzi.

“Ni kwamba inachukua siku 42 kubaini kama dawa ni bora au la, kwa sababu dawa moja ina molekuli nyingi na kila molekuli hupimwa pekee. Tunajaribu kupunguza siku hizo hadi 23 kwa kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa. Lakini kabla ya hapo, tayari tumechukua hatua.”

Hospitali imekanusha madai yaliyotolewa na Mbunge wa Mosop Bw Abraham Kirwa, ikisema dawa zote zinazotumika hospitalini hapo hupatikana tu kutoka kwa wasambazaji waliohitimu, kusajiliwa na kupitiwa kwa umakini.

Hospitali hiyo inasema kila dawa hupitia mchakato mkali wa uchunguzi kupitia Kamati ya Dawa na Tiba kabla ya kuidhinishwa kutumika.

Katika taarifa yake, hospitali imeeleza kujitolea kwake kuendeleza viwango vya juu vya usalama wa wagonjwa na ubora wa dawa, na imetuhakikishia umma kuwa taratibu zake zimeundwa kuwalinda wagonjwa wote.

[email protected]