• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Siku ambayo Gachagua aliandaa mkutano wa kisiasa nje ya hospitali 

Siku ambayo Gachagua aliandaa mkutano wa kisiasa nje ya hospitali 

NA MWANGI MUIRURI 

WENGI bado hawajatokwa na ‘picha’ waliyochora akilini mnamo Aprili 2, 2024 Naibu wa Rais Rigathi Gachagua alipoandaa mkutano wa kisiasa nje ya Hospitali ya Avenue Mjini Thika, Kaunti ya Kiambu wagonjwa wakiwa vitandani.

Bw Gachagua alishangiliwa kwa sauti za juu na wafuasi waliofika eneo hilo ambapo alisisitiza kuhusu azma yake kuangamiza mitandao ya pombe za mauti.

Bw Gachagua alikuwa amefika katika hospitali hiyo kumjulia hali Kamanda wa kituo cha polisi cha Juja Chifu Inspekta John Misoi ambaye alikuwa amelazwa katika kituo hicho cha afya baada ya kushambuliwa kwa mishale na genge la pombe haramu na mihadarati.

Shambulizi hilo dhidi ya Bw Misoi lilitekelezwa mnamo Machi 31, 2024 alipokuwa katika harakati za kuongoza kikosi chake kuvamia danguro lililoko Kijiji cha Gachororo eneobunge la Juja.

Baada ya Bw Gachagua kumaliza ziara hiyo ya ndani ya hospitali, alitoka nje na akahutubia wananchi akitumia kipaza sauti huku akiwa juu ya gari lake nje ya kituo hicho kilichokuwa na wagonjwa waliolazwa.

Naibu Rais alitambulisha umma wanasiasa alioandamana nao, akiwemo Seneta wa Kiambu Bw Karungo Thang’wa na Mbunge wa Juja Bw George Koimburi.

Bw Gachagua alisema vita dhidi ya vileo vimefanikiwa kwa asilimia 70 hadi sasa.

Aidha, aliitaka idara ya mahakama kuunga mkono vita hivyo.

“Maafisa wa mahakama waelewe kwamba watoto wao pia hawako salama kutokana na biashara za pombe za mauti na mihadarati. Watuunge mkono. Hatukatai kushtakiwa. Lakini ni lazima mahakama itusikize kama serikali, isikize wazazi na wanawake wetu, isikize sauti ya kanisa na jamii kwa ujumla kabla ya kufanya maamuzi,” akasema.

Bw Gachagua alimpa Kamanda wa Kiambu amri ya siku tatu kusaka wahuni waliomshambulia OCS Misoi.

“Pia katika kipindi hicho ningetaka umalize hiyo pombe ninakia iko Ngoingwa na Makongeni, mitaa ambayo iliyoko viunga vya Mji wa Thika. Tulikubaliana kwamba ukilemewa na kazi hakuna cha kuhamishiwa kwingine. Tutakufutia kazi uliko kwa sasa,” akasema.

Bw Gachagua alisema kwamba magenge ya mihadarati na pombe yamelemewa na ndiyo sababu sasa yanazindua mashambulizi dhidi ya maafisa.

 

  • Tags

You can share this post!

Watu 8 wakamatwa wakiuziwa pombe ndani ya choo...

Makachero wanasa washukiwa watatu wa wizi wa kimabavu

T L