• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Siku ya Maji Duniani: ‘Hakuna anayeachwa nyuma’

Siku ya Maji Duniani: ‘Hakuna anayeachwa nyuma’

Na SAMMY WAWERU na MASHIRIKA

MACHI 22 ni siku maalum ya kimataifa iliyotengwa kuadhimisha umuhimu wa maji duniani, kila mwaka.

Mada kuu mwaka 2019 ni: “Hakuna anayeachwa nyuma”.

Muungano wa kimataifa (UN) ndio mwasisi wa siku hii, malengo yake yakiwa kuangazia kuwepo kwa maji safi. Inatumika kuhamawisha haja ya kulinda vyanzo vya maliasili hii muhimu, ambapo mataifa huandaa hafla za aina mbalimbali.

Baadhi huendesha kampeni hii kwa njia ya masomo, sarakasi, michezo ya kuigiza, nyimbo, na hata maandamano ya amani. Kuna mataifa yanayotumia siku hii kufanya mchango ili kupata fedha za kufadhili miradi ya maji.

UN iliadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza mwaka wa 1993. Watu wanahimizwa kuelewa bayana shida zinazochangia maji kupungua na hata kukosekana. Pia, wanatakiwa kujua athari zinazotokana na uchafuzi wa maji, kutozingatia usafi wa mazingira, uharibifu wa vyanzo vya mito, na mabadiliko ya hali ya anga.

Kitendawili ni; 2019, ulimwengu unapoadhimisha siku hii, Wakenya wanajivunia kuwa na maji safi na ya kutosha?

Kwa muda wa wiki kadhaa, makali ya ukame katika kaunti 13 yamekuwa vichwa vya vyombo vya habari. Idadi ya watu isiyojulikana, wanahofiwa kuwa wamefariki katika maeneo yanayotajwa kukithiri kiangazi.

Maji ni uhai

Maji ni uhai, na Kenya ni baadhi ya nchi ambazo kilimo ndio uti wake wa mgongo. Kinategemewa kama kapu la lishe, na kukosekana kwa maji ni ishara kuwa wananchi watahangaishwa na baa la njaa.

Hali inayoshuhudiwa kwa sasa ni somo kwa serikali kuu na zile za kaunti kuhakikisha wamekaza kamba juhudi za kuangazia upungufu wa maliasili hii katika kila kona ya taifa.

Uvunaji wa maji ya mvua, msimu wa mvua hasa mafuriko, ni njia mojawapo kutatua ukosefu wa maji.

Viteka maji

Uchimbaji wa mabwawa na vidimbwi, ni baadhi ya njia hizo.

Mwanasiasa Kipruto Arap Kirwa, ambaye amewahi kuhudumu kama waziri wa kilimo serikali ya Rais (mstaafu) Mwai Kibaki, anasema kwa kufanya hivyo kitendawili cha upungufu wa maji kitateguliwa, hasa wakati wa ukame.

“Msimu wa mvua, hasa ya masika, maji mengi hupotea. Kila eneo likiwa na mabwawa na vidimbwi, yatatekwa ili yatumike kufanya kilimo na matumizi mengine nyumbani wakati wa kiangazi,” anasema.

Mbali na mbinu hizo, wananchi wanahimizwa kutumia matenki kuvuna maji. Maeneo ya mashambani, hasa yanayofanya kilimo huyatumia kupanda mimea.

Maeneo ya mijini kama vile Nairobi, upungufu wa maji ungali kero kuu kwa wakazi. Dennis Mugendi, mmiliki wa nyumba za kukodi eneo la Zimmerman, Nairobi, anasema licha ya kujihami kwa hifadhi ya maliasili hii, yanayosambazwa na kampuni iliyotwikwa jukumu yangali haba.

“Hupewa kwa awamu, hata siku tulizotengewa hayaji ipasavyo,” adokeza Bw Mugendi.

Bi Lilian Maina, mmiliki wa ploti Kiambu, anasema amelazimika kuchimbia wapangaji wake shimo la maji plotini, ingawa ni ya kufanya usafi wa mavazi na nyumba pekee. Kampuni ya Nairobi Water & Sewerage, ndiyo husambaza maji Kiambu na Nairobi, na kwa muda wa zaidi ya miaka mitano, wakazi wa maeneo hayo wanaendelea kuhangaika.

Gabriel Ntombura ni mchuuzi wa maji Nairobi na Kiambu, na analalamika kwamba wakati mwingine yanakawia kwa muda wa wiki mbili kusambazwa. Kauli yake inawiana na ya Sammy Ng’ang’a, ambaye alianza uchuuzi wa maji 2014.

“Msimu wa kampeni viongozi hutuahidi kutatua suala la maji. Wanapochaguliwa, huonekana msimu mwingine wa kuomba kura,” anasema Bw Ng’ang’a.

Mtungi wa maji safi lita 20 unauzwa zaidi ya Sh30, katika kaunti hizi mbili.

Hali inayoshuhudiwa Nairobi na Kiambu, si tofauti na ya Nyeri, Murang’a, Machakos, Kirinyaga, Nakuru, Embu, na miji mingine nchini. Ikumbukwe kwamba maji yanapokosekana kina mama, watoto na wenye mahitaji maalumu hasa walemavu ndio hutaabika.

You can share this post!

Kamishna wa Kiambu awaonya wakandarasi wazembe

BI TAIFA IJUMAA, MACHI 22, 2019

adminleo