Simanzi kortini mzee akisimulia alivyopoteza jamaa 6 Shakahola
MZEE wa miaka 61 ambaye alipoteza wanafamilia sita katika mkasa wa Shakahola, alimlilia Paul Mackenzie mahakamani, akimwambia alimlemaza na kumuacha bila matumaini maishani.
‘Wanangu wawili sasa wamekufa na hawawezi tena kunisaidia kama walivyofanya zamani,’ Bw Titus Ngonyo Ngandi aliambia Mackenzie mbele ya mahakama ya Mombasa.
Bw Ngandi alikuwa akitoa ushahidi dhidi ya Mackenzie na washtakiwa wengine 95 ambao walifunguliwa mashtaka baada ya zaidi ya mili 429 ya wafuasi wa kanisa la Good News International (GNI) kufukuliwa msituni.
‘Ulichonifanyia, Mackenzie, nilihisi kama ulivunja mikono yangu yote,’ alimwambia Hakimu Mkuu, Bw Alex Ithuku.
Bw Ngandi alimpoteza mkewe, Esther Bahati Masha, wanawe Isaac Ngala na Harry Ngonyo, mkaza mwana Emily Wanje, na wajukuu wawili katika matukio hayo ya kusikitisha.
Marehemu Ngala alihudumu kama Kitengo cha Kupambana na Wizi wa Mifugo tangu 2011, huku Bi Masha akiwa mchuuzi mahiri katika Ufukwe wa White Elephant.
Familia hii ilihudhuria kanisa la Calvary Worship Centre Muyeye kabla ya mambo kugeuka.
Mambo yalikuwa mazuri katika familia ya Ngandi hadi mkewe alipojiunga na GNI huko Furunzi.
“Alikuwa wa kwanza kujiunga na kanisa hilo, kisha akawashawishi Ngala na Ngonyo.
Ilikuwa mwaka wa 2018, na ni wakati uo huo ambao Ngonyo aliacha chuo,” aliambia mahakama huku akiongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mashtaka ya Umma, Jami Yamina.
Shida za Bw Ngandi zilianza 2015 aliponunua ardhi ya kilimo huko Kamale na kuhamia huko 2018, akiacha familia yake Muyeye.
‘Ningewatembelea kwa muda mfupi kila mara. Nilikuwa nikiwasiliana na Ngonyo, ambaye alinihakikishia kuwa anaendelea vizuri shuleni,’ alisemaBw Ngandi hakujua kuwa huku akimakinikia ukulima, familia yake ilianza kujiunga na kanisa la Mackenzie, jambo ambalo lilisababisha mabadiliko makubwa katika maisha na imani zao.
Aliporudi nyumbani siku moja, Bw Ngandi alishtuka kumpata Bi Masha akijiandaa kuondoka.
“Niliuliza alikokuwa akienda, naye akaniambia kanisani,” alisema huku akijitahidi kuzuia machozi.
‘Nilitarajia angenikaribisha kama mumewe, lakini alikuwa na haraka,’ aliongeza.
Haraka na tabia ya mke wake ilimshangaza, ikizingatiwa kanisa lao, Calvary, lilikuwa karibu na nyumbani.
“Tabia yake ilibadilika sana baada ya kujiunga na kanisa hilo. Alisali karibu kila wakati, hata saa zisizo za kawaida,” alisema alipokuwa akiongozwa na timu ya waendesha mashtaka waliojumuisha Victor Owiti, Betty Rubia na Hillary Isiaho.
Licha ya majaribio yake ya kuongea naye, alisema ushawishi wa Masha uliongezeka tu alipoendelea kuhubiri, akiwahimiza wanakijiji kuwazuia watoto wao wasiende shule na kuchoma stakabadhi zao za shule na hata vitambulisho.
“Nilianza kuwa na wasiwasi na nikakosana na jamii,’ alieleza, na hatimaye kumlazimisha kumfukuza mkewe kutokana na mvutano aliosababisha.
Mapema mwaka wa 2021, Bw Ngandi alisema alipigiwa simu na jirani na kuarifiwa kuwa boma lake lilibaki bila watu.
“Sikuweza kumpata mke au wanangu kwa simu; walikusanya vifaa vyote vya nyumbani ,” alisema.
Mnamo Machi 2023, Ngonyo alimtembelea babake akionekana dhaifu na kueleza kuwa familia yake ilikuwa katika hali mbaya kutokana na ugumu wa maisha.
Muda mfupi baadaye, Bw Ngandi alipata habari za kuhuzunisha kutoka kwa mwanawe mwingine kuhusu hatima ya familia yao huko Shakahola, ambapo wajukuu wawili walikuwa wamepatikana wamekufa.
“Ngala na Ngonyo walifia msituni. Pia nilizika mke wangu na mkaza mwana wangu mwaka huu,” alisema.