• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
‘Singo mothers’ sasa wakimbilia Fida kutafuta sapoti ya kulea watoto

‘Singo mothers’ sasa wakimbilia Fida kutafuta sapoti ya kulea watoto

NA FRIDAH OKACHI

BAADHI ya akina mama waliotengana na waume kwa njia moja au nyingine sasa watafuta muungano wa wanasheria wa kike – Fida – kuona namna waliokuwa wapenzi au waume wao wanaweza kutuma sapoti ya watoto kipindi hiki maisha yakifinya wengi.

Mfumkobei na kupanda kwa gharama ya maisha kwa ujumla kunawahangaisha watu wengi, wakiwemo baadhi ya akina mama wasio na waume almaarufu ‘singo mothers’, wakitatizika kutunza watoto wao bila msaada wowote kutoka kwa wenzao walioachana nao.

*Beatrice, mama wa watoto wanne, amebaki kwenye njia panda baada ya mzazi mwezake kuingia mitini na kumuacha akitekeleza majukumu yote.

Kulingana na *Beatrice, alikaa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka saba na kutemwa na mumewe.

“Niliishi naye na kupata watoto watatu. Changamoto za ndoa zilipozidi aliniacha na kukosa kuwashughulikia wanawe,” akasema *Beatrice.

Mama huyo alichukua hatua ya kupiga ripoti kwenye Shirika la Wanawake Wanasheria (Fida Kenya) baada ya mazungumzo ya maelewano kwenye idara ya watoto kugonga mwamba.

“Nilimshtaki ashughulikie wanawe lakini akaanza mchezo wa paka na panya. Hatua ya pili nilielekea kwa Fida na ni miaka sita bado sijapata usaidizi jinsi nilivyotarajia,” alisimulia.

Kwa upande mwingine, alilaumu Fida kwa kudai ilipeleka maelezo ambayo si yake na kuwasilisha mahakamani.

“Nilisikitika nilipofanya uchunguzi wangu na kupata wakili anayenihudumia ameandika maelezo ambayo si yangu. Kulea hawa watoto peke yangu sio mchezo. Bado mzazi mwenza hajapelekewa barua ya kufika mahakamani,” akalalama.

Katika mtaa wa Kwa Ndege, Utawala jijini Nairobi, *Salina ambaye pia alikuwa kwenye ndoa kwa miaka 13, alifukuzwa atoke nyumbani kwake akiwa na watoto watatu.

Anasema mzazi mwenza hashughulikii wanawe.

“Bwanagu ni wakili na yeye mwenyewe ndiye alipeleka hawa watoto katika shule ghali. Mimi binafsi nilikuwa mfanyabiashara lakini kwa sasa sina kazi,” *Salina alisema kwa uchungu.

Takwimu za hivi punde kutoka Shirika la Wanawake Wanasheria (Fida) zikionyesha kuwa matukio ya utelekezwaji wa watoto yanaongezeka kwenye na kurekodi zaidi ya kesi 100 kwa mwezi.

Afisa mmoja wa Fida alisema baadhi ya wanawake huwa na nia mbaya wanapotaka msaada wa mahakama na Fida kwa waume kutoa sapoti.

Alikataa kutajwa akisema hayuko kwa nafasi ya kunukuliwa na vyombo vya habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Fida-Kenya ni Bi Anne W. Ireri. Naye Mwenyekiti wa Fida-Kenya ni Bi Nancy Ikinu.

  • Tags

You can share this post!

Raila kuokoa jahazi makinda wake wa Azimio wakikwama

Jinsi mhasibu alivyozamisha Sh16m kwa shamba hewa

T L