Spika Wetang’ula, almaarufu ‘Papa wa Roma’ alivyomwomboleza Papa Francis
SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, almaarufu kwa jina la utani kama ‘Papa wa Roma’, ameungana na mamilioni ya waumini wa Kikatoliki nchini na duniani kumwomboleza Baba Mtakatifu Francis.
Kupitia taarifa ya risala za rambirambi, Spika Wetang’ula ambaye pia ni mfuasi wa Kanisa la Kikatoliki, alimtaja Papa Francis kama “upeo wa upendo, haki na unyenyekevu.”
“Nimepokea habari za kifo cha Baba Mtakatifu Francis kwa huzuni na simanzi kuu,” alisema.
“Alikuwa mchungaji wa kiroho aliyejitolea maisha yake kumhudumia Mwenyezi Mungu na binadamu kwa jumla.”
Bw Wetang’ula alimsifu Baba Mtakatifu ambaye ni Papa wa 266 wa Kanisa la Kikatoliki na Kiongozi wa Jiji Takatifu la Vatican kama “mtetezi wa walalahoi na waliotengwa katika jamii.”
Alisema “urithi wake utahifadhiwa katika nyoyo za waumini na vizazi vijavyo.”
“Baba Mtakatifu alikuwa kielelezo bora cha mafunzo ya Kristo kuhusu kukumbatia msamaha, huruma na upendo. Alikuwa sauti ya wanyonge kwa kutetea heshima na hadhi ya kila binadamu bila kubagua.”
Bw Wetang’ula alisisitiza msimamo wa Papa kuhusu kushirikisha waumini wote katika maamuzi ya Kanisa la Kikatoliki kuambatana na dhana ya usyonadi.
“Aliashiria nafasi ya Kanisa kama dira ya maadili katika jamii kupitia mwito wa uwajibikaji, uwazi na uadilifu sio tu ndani ya Kanisa bali katika uongozi kimataifa,” alisema.
Alinukuu Yohana 11:25 kuwafariji waumini wa Kikatoliki akisema, “Tunapoomboleza, tunasherehekea pia maisha ya kipekee aliyoishi na urithi wa unyenyekevu, imani na upendo anaotuachia.”
“Tunaridhika na maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo: Mimi ndimi ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye atakuwa hai, ijapokuwa amekufa.”
Kifo cha Baba Mtakatifu aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 88, kilitangazwa Jumatatu asubuhi na mweka hazina wa Vatican, Kadinali Kevin Farrell.
Papa Francis ambaye jina lake halisi ni Jorge Mario Bergoglio, alikuwa kiongozi wa kwanza wa Kanisa la Kikatoliki mwenye asili ya Amerika Kusini na wa kwanza kutoka Ushirika wa Jesuit.
Aliteuliwa kuwa Papa 2013 na atakumbukwa kwa juhudi zake za kuliongoza Kanisa la Kikatoliki kukumbatia mageuzi na huruma.
Aliongoza mageuzi ya kihistoria kupitia nyaraka za ‘Fratelli Tutti’ zinazohimiza undugu na ubinadamu na ‘Laudato’ zinazohimiza ulimwengu kushughulikia mabadiliko ya hali ya anga.
Kulingana na Wetang’ula, kifo cha Papa Francis kimefikisha kikomo enzi muhimu ya utawala wa utiifu, huruma na ukakamavu thabiti kwa Injili ya Kristo.
“Roho yake ipumzike kwa amani ya milele katika utukufu wa Ufalme wa Mungu. Mfano wake uendelee kutuongoza katika njia za Kristo,” alisema.